Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema
Habari za hivi punde zinasema kwamba Jeshi la Polisi limetumia mbwa na virungu kuwatawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walioandamana kuelekea Makao Makuu ya Jeshi hilo.
Wanachama hao kutoka Dar es Salaam na mikoa ya jirani walikuwa wamehamasishwa
na viongozi wa chama hicho kukusanyika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam wakati mwenyekiti wao Freeman Mbowe atakapohojiwa.
Hata hivyo, jeshi hilo lilikwishaonya mapema kwamba raia yeyote asisogee kwenye eneo hilo.
Jana Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, aliwataka vijana kuhakikisha wanaandaa mazingira ya kuhakikisha mwenyekiti wao anakwenda polisi salama na kwa amani.
Dk. Slaa alisema: “Kesho tunakwenda saa tano, tumeandaa mawakili wetu wote waliopo ndani ya chama, tunataka polisi wajiandae kwa hoja, vijana andaeni mazingira kuhakikisha kiongozi wenu anaenda kwa amani na katika hali hii ningependa twende hata mahakamani.”
Msafara huo utaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu pamoja na mwanasheria wa chama hicho kutoka Makao Makuu, Peter Kibatala na Makamu Mwenyekiti Bara, Profesa Abdallah Safari, Mabere Marando na Halima Mdee.
Mara baada ya mkutano wa Chadema na waandishi wa habari kumalizika, Jeshi la Polisi nalo liliitisha mkutano na waandishi wa habari na kutoa onyo kwa wananchi watakaojaribu kufuata wito wa chama hicho.
Katika mkutano huo, Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, alisema yeyote atakayejihusisha na maandamano hayo atachukuliwa hatua za kisheria kwani ni batili na Jeshi la Polisi haliyatambui.
“Maandamano hayo ni batili kwa sababu kuu mbili, kwanza Bunge la Katiba lipo kwa mujibu wa sheria na hakuna sheria yoyote iliyokiukwa, kwahiyo kitendo cha kufanya maandamano kushinikiza kuvunjwa kwa Bunge hilo ni kinyume na sheria na jeshi letu haliwezi kuruhusu," alisema Chagonja.

No comments:
Post a Comment