
Na Hastin Liumba,Tabora
CHAMA kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU) kimeanza kuchukua hatua za kubadili mfumo wa uwajibikaji kwa lengo la kurudisha heshima na imani kwa wakulima wa zao hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Tabora mwenyekiti wa WETCU Mkandala Makandala alisema hatua zinazochukuliwa zitaongeza uwajibikaji, uwazi, matumizi bora ya fedha, mipango inayotekelezeka na yenye tija pamoja na huduma ya moja kwa moja kwa wakulima.
“Hatua hizi zimetulazimu kuangalia upya muundo na mfumo wa rasilimali watu ili kuhakikisha watumishi wanatekeleza majukumu yao kulingana na dira tuliyojiwekea.”alisema
Mkandala alizitaja hatua zilichukuliwa na chama hicho kuwa ni pamoja na kuimarisha idara ya uhasibu kwa kuajiri watumishi wenye sifa na kuwapatia vifaa vya kisasa ili kuhakikisha matumizi bora ya fedha na utunzaji sahihi wa kumbukumbu.
Alisema hatua hiyo itasaidia kukabiliana na suala la matumizi mabaya ya fedha, utunzaji mbovu wa kumbukumbu jambo ambalo halikuwepo kabla ya kuchaguliwa kwake kushika wadhifa huo, na hivyo kusababisha malalamiko mengi dhidi ya chama hicho.
Mwenyekiti huyo alibainisha WETCU imechukua hatua za kuwafanya wafanyakazi wake kutambua mwajiri wao mkuu ni mkulima wa tumbaku hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na maarifa na kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.
“Watumishi wetu wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia muda na weledi wakati wa kutoa huduma kwa wakulima wanapokuwa ofisini au wanapowatembelea mashambani.”alisema.
Mkandala aliongeza chama hicho pia kimeweka mkakati wa kutoa mafunzo ya aina mbalimbali kwa watumishi wake kwa lengo la kuwaongezea maarifa yatakayo wafanya kuwajibika zaidi kwa kutoa huduma bora kwa wakulima.
”Mpango huu wa mafunzo utaenda hadi kwa viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika ambao ni katibu meneja, mtunza fedha na mtunza stoo kutoka kila chama cha msingi.” aliongeza.
Kiongozi huyo wa WETCU alibainisha mafunzo hayo yana lengo la kukabiliana na wimbi la ubadhirifu wa fedha na mali za wakulima jambo ambalo limezua migogoro isiyokwisha na ambayo imevidhoofisha vyama hivyo vya msingi.
Katika hatua nyingine Mkandala alisema WETCU imeweka mpango wa kulipa madeni yote yanayodaiwa na vyama vya msingi ili kuondoa kero kwa wakulima ambayo imedumu kwa muda mrefu.
Mkandala aliwaonya baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi wanaotumia madeni hayo kama sababu ya kuendeleza vitendo vya wizi na ubadhirifu wa fedha za wakulima na kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua.
“Baadhi ya vyama vya msingi tumevilipa kwa asilimia 100, hata hivyo baadhi ya viongozi katika vyama hivyo wamekuwa wakiwadanganya wakulima kuwa bado wanaidai WETCU jambo ambalo limeleta mkanganyiko kwa wakulima.” alisema.
No comments:
Post a Comment