Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday, 19 March 2015

MAMA BARAKA ASEMA: SIKUPENDA KUZAA ALBINO NI KAZI YA MUNGU

 Bi Prisca Shaaban akiwa amembeba mwanawe Luciana (3) wakati akiwa hospitali ya rufaa Mbeya anakopata matibabu ya jeraha la kichwa pamoja na kumwangalia mwanawe Baraka (6) aliyekatwa kiganja cha mkono na watu wasiofahamika.
Na Hawa Mathias
Ni kama ndoto lakini  ni kweli nimepatwa na sitofahamu kuhusu hatima ya maisha ya watoto wangu watatu wenye ulemavu wa ngozi (albino). Sijui nikimbilie wapi ili niokoe maisha yao. Mungu simama pamoja na watoto wangu kwani nao wana haki ya kuishi.”
Hiyo ni kauli ya Prisca Cosmas ambaye sasa yupo katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, akimuuguza mtoto wake Baraka Cosmas (6) , mwenye ulemavu wa ngozi aliyekatwa kiganja cha mkono siku chache zilizopita.
Tukio la Baraka kukatwa kiganja lilitokea usiku wa manane kuamkia Machi 6 katika Kijiji cha Kipeta , Bonde la Ziwa Rukwa, wilayani Sumbawanga Vijijini .
 Prisca, ambaye ni mama wa watoto wanne anasimulia kwa uchungu kuwa siku ya tukio, licha ya mtoto wake kukatwa kiganja, naye  alipigwa rungu kichwani lililosababisha apoteze fahamu pamoja na kupata jeraha kubwa.
Mama huyo anasema kuwa katika uzazi wake ana watoto wanne wakiwamo watatu wenye ulemavu wa ngozi.
Anabainisha kuwa mbali na Baraka watoto wengine wenye ulemavu huo ni Hosia Cosmas (4) na Jafari Cosmas (2).
“Ukatili huo ulitokea saa 7 usiku. Nilikuwa nafungua mlango kwenda kujisaidia. Nilipofungua mlango, ghafla nilisikia sauti ya mtu ikimuamuru kukaa kimya, hali ambayo ilinishtua.
Katika uvamizi huo nilijitahidi kupambana kumwokoa mwanangu, lakini ilishindikana. Yote namwachia Mungu,” anasema Prisca na kuongeza:
“Sikupenda kuzaa watoto walio na ulemavu wa ngozi ni mipango ya Mungu, inaniuma sana na natambua mimi ni wa kuishi maisha ya hofu kila siku. Kuna wakati naomba giza lisiingie.”
“Nipo njiapanda, sijui watoto hawa wenye ulemavu nitawalea vipi? Naomba msaada wa ulinzi kutoka kwa Serikali, majirani na wasamaria,” anasema Prisca na kusisitiza: “Nina hofu hata kurejea nyumbani kwangu kwani naamini watu hao wabaya watarudi kuhatarisha maisha yetu.”
Prisca ni mkazi wa Kijiji cha Kipeta, aliolewa na mwanaume anayemtaja kwa jina la Cosmas. Yeye ni mke wa kwanza kwa mwanaume huyo, ambaye sasa ameoa mke wa pili.
Kauli za viongozi
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya anasema kuwa tukio hilo ni la aibu kwa Mkoa hata Taifa na kwamba ni lazima wahusika watasakwa popote walipo.
Anaeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete alishatoa agizo, hivyo wakuu wa mikoa lazima wahangaike kwa kutumia Kamati za Ulinzi na Usalama wanazoziongoza katika mikoa yao kukomesha uonevu huo.
“Wakati umefika kwa wakuu wa mikoa wote na kamati za ulinzi na usalama kukutana na kujadili nini kifanyike ili kutokomeza vitendo hivyo vya kikatili dhidi ya wenzetu wenye ulemavu wa ngozi albino,’’ anasema.
Akiwa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Manyanya anasema kuwa ni jambo la kushangaza kuendelea kwa matukio hayo kwani hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alishatangaza mapambano dhidi ya matukio ya mauaji, kukatwa viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi.
“Ndugu zangu, watu wanaofanya vitendo hivi mnawajua, wanakaa katika mitaa, vijiji na vitongoji. Sasa ni wakati wa kuondoa hofu, mtangulizeni Mungu muwafichue na sisi Serikali hatutavumilia vitendo hivi,’’ anasema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro anasema kuwa wakati sasa umefika kwa wananchi kutambua kwamba ni jukumu la wote kupambana dhidi ya wahalifu na kwamba ushirikiano wa dhati unahitajika zaidi .
Chama cha Albino Mbeya
Katibu wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi, Mkoa wa Mbeya, William Simwali anaishauri Serikali kutafuta njia ili kumsaidia mwanamke huyo kulea watoto wake watatu.
Anashauri Serikali kuwajengea kituo maalumu cha kuishi watu wenye ulemavu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Anasema kuwa licha ya Serikali kupiga marufuku waganga wanaopiga ramli, lakini bado wapo wanaendesha shughuli zao kwa vificho akaongeza kwamba Serikali kupitia polisi haina budi kufanya msako wa nyumba kwa nyumba ili kuwabaini na kuwafikisha wahalifu hao kwenye mikono sheria.
Kikwete ateta na viongozi
Wiki mbili zilizopita Rais Kikwete aliwaeleza viongozi wa Albino waliomtembelea Ikulu jijini Dar es Salaam ambao walioongozwa na Mwenyekiti wao, Ernest Kimaya kuwa; “Mauaji haya yanaisikitisha Serikali na kuifedhehesha sana”.
“Msidhani hatufanyi lolote, tunafanya juhudi kubwa na mbalimbali lakini imefikia wakati tuongeze juhudi hizo,” alisema Kikwete.
Katika kikao hicho viongozi hao, walisoma risala ambayo imetoa kilio chao na mapendekezo yao kwa Serikali na hatimaye ikaafikiwa kuwa na haja ya kuunda kamati ya pamoja ambayo itajumuisha Serikali, viongozi wa Albino, viongozi wa waganga wa jadi na wadau wote wakuu katika suala hili ili kupata mapendekezo na mkakati wa pamoja ambao hatimaye mauaji haya kukomeshwa kabisa nchini.
Rais Kikwete alisema mauaji hayo hayafanywi na Serikali bali watu ambao wako katika jamii kwa kushirikiana na waganga wa jadi na watu wengine wenye tamaa mbalimbali katika jamii hivyo na kwamba ni lazima yakomeshwe.
“Kwenye familia, jamii na hatimaye vyombo vya ulinzi na usalama na hilo ndiyo jukumu kubwa ambalo Serikali inapaswa kulisimamia na tutalisimamia kwa ushirikiano wa pamoja,” aliahidi.
“Mauaji haya yanaisikitisha Serikali na kuifedhehesha sana, msidhani hatufanyi lolote, tunafanya juhudi kubwa na mbalimbali lakini imefikia wakati tuongeze juhudi hizo”alisema Rais
Rais alisisitiza kuwa kamati hiyo ya pamoja itaweka mikakati ya kuwabaini wale wote wanaohusika kuanzia wakala, waganga na hatimaye wale wanaonufaika na viungo vya walemavu hao.
Pia, aliahidi kuwa Serikali itasaidia familia na wahanga wa vitendo vya mauaji kwa hali na mali ili waweze kujimudu na pia kuwapa ushauri nasaha ili kuondokana na majonzi yanayosababishwa na vitendo hivyo kwani vinawaletea waathirika na watu wanaoishi nao mfadhaiko na msongo wa mawazo katika jamii.
Viongozi hao walitoa kilio chao kwa Serikali kuziangalia na kuzimulika taasisi zisizo za kiserikali ambazo pamoja na kujipambanua kuwa zinatetea haki za Albino nchini bado hazina mkakati wa pamoja na hazipo wazi kwa walengwa hapa nchini.
CREDIT: BBC

No comments:

Post a Comment