Pichani kutoka kushoto Martha
Steo,Tamasha Kalukanya na Janepha Japhet Sahani wakiwa katika picha ya pamoja
Kituo cha Afya Ilolangulu Uyui mkoani Tabora. (Picha na Hastin Liumba).
Na Hastin
Liumba,Uyui
"HIVI sasa
nina wakati mgumu sana napita makanisani na misikitini kuomba misaada ili
niweze kutunza watoto wangu hawa wanne...
Hali hii
imetokana na kukimbiwa na kutelekezwa mume wangu na alinitelekeza baada mimi
kupimwa virusi vya ugonjwa wa UKIMWI na kuonekana nimeambukizwa VVU.
"Niko kwenye
wakati mgumu sana hivi sasa natamani kama nisingezaliwa naumia sana nikiangalia
watoto hao nitawapeleka wapi na ndugu na mume wamenitenga."
Hayo ni
maneno ya Martha Steo (29) mkazi wa Kijiji cha Ilolangulu, Wilaya ya Uyui mkoani
Tabora akiueleza ujumbe wa shirika lisilo la kiserikali la EGPAF ukiongozwa na Mratibu wa Mawasiliano Mercy Nyanda na waandishi wa habari.
Shirika la
EGPAF limekuwa likitoa sapoti ya kutokomeza maambukizi ya VVU toka kwa mama
wajawazito kwenda kwa mtoto chini ya ufadhili wa US Centers for Disease (CDC)
na United States Agency for Intetion Development (USAID) toka nchini Marekani.
Steo anaeleza
alipata maambukizi ya VVU mwaka 2014 pale alipopata ujauzito na kupimwa Kliniki
ya Ilolangu.
Alisema
baada ya kupimwa na kukutwa na VVU alipata ushauri na kuanza kutumia dawa na
alifanikiwa kujifungua salama na mtoto wake hana maamubukizi ya VVU.
Alisema
baada ya kukutwa ana VVU alimweleza mume wake naye aje kituo cha afya apime ili
kama ameambukizwa VVU naye aungane naye kwenye tiba.
Alisema
wazazi wa mume wake hawako mbali na anakoishi yeye lakini amejaribu kufanya nao
mazungumzo ili wamsaidie kutunza watoto lakini wamegoma.
‘Wazazi wa
mume wangu hawako mbali na ninapoishi lakini wamegoma kabisa kunisaidia kutunza
watoto wangu…….. wamenitenga.’alisema Steo.
Aidha Steo
anasema alipata taarifa mume wake na Baba yake walikwenda kupima VVU lakini
majibu ya mume wake hayajui na anajisikia vibaya kuona mtoto wake ametelekezwa
na baba yake bila kosa lolote.
Anasema
maabukizi ya VVU ni yetu wazazi lakini leo hii mtoto anahukumiwa bila kosa
lolote kwa kunyimwa haki zake kama mtoto inaumiza sana.
Anatoa wito
kwa mama wajawazito kujitokeza kupima afya zao ili kama wana maambukizi ya VVU
waanze tiba kumkinga mtoto aliyeko tumboni.
Naye Tamasha
Musa Kalukanya (32) mkazi wa kijiji cha Ideke kata ya Mabama wilaya ya Uyui
mkoani Tabora naye alikutwa na mkasa wa kukimbiwa na mume wake baada ya kukutwa
ameambukizwa VVU.
Kalukanya
anasema alikutwa na VVU mwaka 2013 baada ya kupimwa akiwa na ujauzito na alipopimwa
na kukutwa ana VVU mara moja alianza kutumia dawa ili kumkinga mtoto wake
asiambukizwe VVU.
Anasema yeye
alikuwa akiishi na mume wake lakini mara baada ya kugundulika ana VVU mume wake
alimkimbia na kumtelekeza.
Alisema
alijaribu kuwasiliana naye kwenye simu alimjibu kuwa yupo wilaya ya Kahama
mkoani Shinyanga.
“Niliwasiliana
naye akaniambia yupo Kahama na nilijaribu kumshauri na nilimweleza kuwa
nimeambukizwa VVU……hakujibu chochote alikata simu.”alisema.
Anaeleza
toka nilipomueleza nina VVU lakini mtoto nimejifungua na yuko salama hadi leo
hii nikipiga simu haipatikani inaonyesha amebadili namba hataki tuwasiliane.
Hivi sasa
anasema anaishi maisha magumu sana kwani anafanya biashara ya viazi na kulima
mahindi ili yamsaidiie kutunza familia.
Anasema
ndugu na jamaa zake na mume wake wamemtenga kana kwamba ugonjwa VVU alionao
wanauna kama mkosi kwao.
Alisema
anaiomba jamii kuondokana na dhana hiyo kwani kilimtokea hakukiomba na aliwasihi
kinamama wenzake hasa wajawazito kujitokeza mapema kuhudhuria kliniki ili waweze
kutambua afya zao.
Alisema
kitendo cha wajawazito kuchelewa kuhudhuria mapema kliniki kunaweza kuhatarisha
afya zao na mtoto aliyeko tumboni.
Anasema kuwa
VVU si jambo la ajabu huo ni ugonjwa kawaida kama magonjwa mengine wajitokeze
kupima afya zao.
Jane Ibasa
(30) mkazi wa kata ya Ilolangulu wilaya ya Uyui mkoani Tabora amedai
ameambukizwa VVU toka mwaka 2014.
Ibasa
anasema yeye binafsi aligundulika kuwa na VVU baada ya kupimwa kliniki ya
Ilolangulu akiwa mjamzito.
Alisema
alipopima na kukutwa na VVU alianza tiba na Mungu alimsaidia kujifungua mtoto
ambaye hana maambukizi.
Alisema
baada ya vipimo alimweleza mume wake juu ya afya yake na alimshawishi kuja
kupima na mume wake alipima na kwa maajabu ya Mungu hakuwa na maambukizi ya
VVU.
Alisema mume
wake amepima kwa hatua zote tatu na ameendelea kutoa majibu ambayo yanaonyesha
hana mambukizi yenye VVU.
Alisema mume
wake mara baada ya kupimwa na kukutwa hana maambukizi ya VVU alimweleza hana
mpango wa kumuacha wataishi wote.
“Najisikia
amani sana baada ya mume wangu kunieleza ataendelea kuishi name milele hadi
kifo kiwatenganishe…..sikutegemea nilijua nitatengwa na kutelekezwa kama ilivyo
kwa wenzangu.”alisema.
Mratibu wa
mawasiliano wa shirika lisilo la kiserikali la EGPAF Mercy Nyanda alitoa wito
kwa wajawazito kujenga tabia ya kuwahi kupima afya zao hatua zote nne kliniki
ili waweze kutambua afya zao.
Nyanda
anasema mama wajawazito watalinda afya zao watoto wao endapo watakuwa
wameambukizwa VVU kwa kupata tiba stahiki.
No comments:
Post a Comment