Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
Wakiongea kwenye mkutano wao wa hadhara eneo la Uledi, wananchi hao walisema wamechoshwa na ulaghai wanaofanyiwa na mkurugenzi mtendaji wa Manispaa Tabora Sipola Liana.
Mwenyekiti wa kamati ya watu saba iliyoundwa Aman Shaban Mbwambo alisema kamati yake imechoshwa na danadana za mkurugenzi huyo hivyo ni vyema wakaonane na waziri Lukuvi ili kila kitu kiwe wazi.
Akifafanua zaidi mwenyekiti huyo alisema mara ya mwisho walikwenda kwa mkurugenzi Sipola Liana ili wapewe kibali cha kukamilisha zoezi la kupiwa ardhi yao na kampuni iiitwayo Ardhi Plan lakini majibu yake hayakuridhisha.
Alisema mkurugenzi huyo walipombana alijibu yeye ameandikiwa barua na mwajiri wake toka wizarani ikimtaka kusitisha zoezi hilo la upimaji unaofanywa na kampuni ya Ardhi Plan.
Aliongeza baada ya mabishano marefu mkurugenzi huyo alitishia kuita polisi kwani kamati ilidaiwa inafanya fujo ofisini kwake jambo ambalo hakufanya hivyo.
Aidha anabainisha mkurugenzi huyo walishindwa kuelewana naye hivyo waliondoka kwenda kuonana na mkuu wa mkoa wa Tabora Ludovick Mwananzila ambaye naye alishangazwa na hali iliyopo.
“Mkuu wa mkoa alimuagiza katibu msaidizi ofisi ya RAS ardhi Longono Kazimoto kushughulikia suala hilo na kumpa taarifa hatma yake ilipofikia juu ya mgogoro huo.”alisema.
Hata hivyo Longino Kazimoto alikuja na ajenda yake kuwa wananchi hao waachane na kampuni ya Ardhi Plan ili waletewe kampuni nyingine jambo ambalo walipingana nalo na kuondoka.
Anasema hadi sasa wameshatoa zaidi ya hekari 417 ikiwa ni eneo ambalo watapitisha huduma za jamii kama eneo la ujenzi wa hospitali ya wilaya,shule na barabara lakini taarifa walizonazo kuna kigogo anataka kumegewa zaidi ya hekari 200 kinyemele.
Wakiongea kwenye mkutano wao wananchi hao waliamua kuchangishana fedha kuiagiza kamati hiyo yenye watu saba kwenda kwa waziri William Lukuvi awasaidie kupata haki zao kwenye maeneo wanayomiliki.
Masoud Juma alisema anasikia uchungu sana kuona haki zao zinapindishwa kwenye maeneo yao kwa manufaa ya kigogo mmoja anayetaka kumegewa zaidi ya hekari 200.
Alisema wamechishwa na hali hiyo hivyo anaona hali hiyo itapelekea wananchi hao kuhamasisha siku moja kupambana na wanaokwamisha haki zao kwani siku zote duniani serikali yoyote kamwe haiwezi kushinda vita na wananchi wake.
Simon Lamekc mjumbe wa kamati hiyo ya watu saba alisema endapo wataona haki inacheleweshwa watafikia mahali wataanza ujenzi wa nyumba zao.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tabora Moshi Abdulrahaman Nkonkota alisema yupo nyuma ya wananchi hao kuona haki inatendeka kwani uongozi wa halmashauri ya manispaa Tabora wamekuwa sehemu ya kero ya ardhi za wananchi kwenye wilaya yake.
Anasema kero za viwanja kwa sasa ambayo imepelekea watumishi kadhaa idara ya ardhi wamesimamishwa kazi ni Malabi,Malolo na Uledi.
Mkuruenzi manispaa Tabora Sipola Liana alikiri mgogoro huo kuwepo na unashughulikiwa.
Katibu msaidizi ofisi ya RAS Tabora kitengo cha ardhi Longino Kazimoto alikiri kuwepo mgogoro na kudai kama kamati hiyo inakwenda kumuona wazri wa ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi William Lukuvi ni sawa kwani watapata majibu sahihi na wataridhika kwani huko ndiko mwisho.
Mkuu wa mkoa wa Tabora Ludovick Mwananzila hakupatikana kuelezea sakata hilo kwani katibu muhtasi wake alisema bosi wake amesafiri.
No comments:
Post a Comment