Mkuu wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Itimila mkoani Simiyu, kimelitaka Jeshi la Polisi kusitisha msako wa waganga wa jadi wanaopiga ramli chonganishi.
Hatua hiyo imekuja huku Jeshi la Polisi katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, likiwa katika msako mkali wa kuwakamata waganga wa namna hiyo.
Mbali ya kulitaka jeshi hilo kusitisha shughuli hiyo, pia CCM imetaka waganga hao wa jadi wapewe muda wa kutosha ili wapatiwe leseni za kutambulika kwa kazi zao.
Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Mohamoud Mabula, wakati wa mkutano wa waganga wa jadi uliofanyikia katika viwanja vya Shule ya Sekondari Lagangabilili wilayani humo mwishoni mwa wiki.
Mabula alimtaka Mkuu wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo, aliyehudhuria mkutano huo, kusitisha shughuli hiyo kwa maelezo kwamba baadhi ya waganga hao wa jadi wamekamatwa kutokana na kukosa leseni lakini hawajihusishi na upigaji wa ramli.
Hata hivyo, alisema anatambua umuhimu wa agizo la Rais Jakaya Kikwete, lakini kuhusu uendeshaji wa operesheni hiyo anaipinga kutokana na waganga wengi kutopewa muda wa kujiandikisha ili kupatiwa leseni.
"Operesheni hii inataka kutukumbusha operesheni kimbunga kwa wahamiaji haramu na kukamata majangili. Operesheni hizi zimeondoka na viongozi wengi wachapakazi, sasa hatutaki Chama kurudia makosa. Tunataka operesheini zifanyike kwa amani na siyo kuwashtukiza watu,” alisisitiza Mabula.
Alieleza kuwa maagizo ambayo yamekuwa yakitolewa na viongozi wao ngazi za juu kwa upande wa serikali, huwaweka katika wakati mgumu viongozi wa Chama ngazi za mkoa na wilaya kutokana na maagizo hayo kutekelezwa kwa nguvu.
“Sisi kama Chama, tumeanza kupata malalamiko kutoka kwa wapigakura wetu. Wanasema CCM inataka kuwafukuza waganga wa jadi…kwa hili hatukubali tulalamikiwe tunachohitaji msako ufanyike lakini kwa amani na watafutwe wapiga ramli tu na siyo waganga wote,” alisema.
Kauli hiyo ya kiongozi huyo wa CCM, ilipokewa kwa shangwe na waganga wa jadi zaidi ya 200 waliohudhuria mkutano huo.
"Niko tayari kwenda jela kwa niaba ya waganga katika wilaya hiyo ikiwa operesheni hiyo haitasitishwa," aliongeza Mabula.
Aidha, alisema atapambana hadi ngazi za juu kuhakikisha kwamba waganga wanaofanya kazi yao kwa kufuata misingi ya sheria na kanuni za nchi, hawaonewi kwa kisingizio cha kupiga ramli chonganishi.
RPC ATII AMRI
Baada ya kauli hiyo ya CCM, Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Mkumbo, alisimama na kutangaza kuwa operesheni hiyo imesitishwa katika Wilaya ya Itimila.
Aidha, Kamanda Mkumbo alitoa mwezi mmoja kwa kila mganga kuhakikisha anapatiwa leseni.
Hata hivyo, alisema baada ya muda huo kumalizika, operesheni hiyo itaendelea.
“Tumesitisha operesheni hii kama alivyosema Mwenyekiti na tunatoa mwezi mmoja...lakini baada ya muda huo, tutaanza msako.
Ninachowaomba waganga nyote nendeni kwa viongozi wenu mkajiandikishe ili taratibu za leseni zifanyike," alisema Kamanda Mkumbo.
SHIMAUTITA WAUNGA MKONO MSAKO
Hata hivyo, Shirika la Maendeleo la Utafiti Tiba Asili Tanzania (Shimautita), limeungana na serikali kutaka operesheni ya kuwatafuta wapiga ramli chonganishi wasakwe.
Katibu Mkuu wa shirika hilo, Dk. Aaron Machokosi, alisema kuwa kutokana na hali ilivyo hivi sasa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe, operesheni hiyo imekuja wakati mwafaka.
“Tunaipongeza serikali kwa uamuzi wake huo. Ni lazima waganga wa jadi kufuata misingi ya sheria na kanuni za nchi…tunachowataka waganga wote nchi nzima wajiandikishe katika sehemu husika ili kupata leseni,” alisema Machokosi.
Aidha, Machokosi alimshangaa Mwenyekiti wa CCM kuagiza kusitishwa kwa zoezi hilo ikiwa ni pamoja na Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, kutii amri hiyo.
Alisema agizo hilo lilitolewa na Kiongozi wa nchi, hivyo linatakiwa kufanyiwa kazi bila ya mzaha.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment