Wakati Ligi Kuu soka ya Wanawake ikitarajiwa kuendelea kesho Ijumaa Januari 20, 2017 kwa michezo mitano, wachezaji 19 kati 25 bora walioteuliwa katika mradi wa kuibuka na kukuza vipaji vya soka wa Airtel (Airtel Rising Stars), wametawala katika klabu zinazoshiriki michuano hiyo, inayoendelea.
Wachezaji hao wanaocheza kwa mafanikio makubwa ni Agatha Joel, Fabiola Fabian, Eva Jackson, Zainabu Mrisho, Fumu Mohamed, Stella Wilbert, Christina Samwel, Shamimu Hamisi, Oppa Msolidi na Yustina Mboje ambao wamesajiliwa na Klabu ya Evergreen ya Temeke, Dar es Salaam.
Wengine ni Zubeda Mohamed, Asphat Kasindo, Grace Yusuf na Fatuma Yusuf waliosajiliwa na Mlandizi Queens ya mkoani Pwani wakati Zainabu Mohamed, Mwantumu Ramadhani na Anna Andrea waliosajiliwa na Mburahati Queens ya Dar es Salaam.
Pia wamo Elizabeth Julius aliyesajiliwa na JKT Queens na Violeth Thadeo ambaye anachezea Panama ya Iringa. Wachezaji ambao hawana klabu hadi sasa ni Fadhil Esmail, Faraja Hamad, Hawa Juma, Hadlifa Mussa na Zainab Mrisho pamoja na Eva Michael.
Kwa sasa nyota hao pamoja na wachezaji wengine sita wako kambini kwa ajili ya kliniki na kuboresha vipaji vyao kabla ya kuiitwa kwenye timu za taifa ambazo zitaingia kwenye ratiba ya michuano mbalimbali barani Afrika.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Airtel Tanzania linashukuru klabu ambazo zimewasajili wachezaji hao ambao waling’ara katika soka kuanzia mikoani hadi ngazi ya Taifa.
Mechi mbili zinazotarajiwa kuchezwa kesho kwa upande wa Kundi A Mburahati Queens itacheza na Mlandizi kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam wakati mechi za Kundi B itakuwa ni kati ya Baobab ya Dodoma na Panama ya Iringa katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Mpwapwa na hii ni baada ya Uwanja wa Jamhuri kufungwa kutokana na ukarabati unaoendelea.
Mechi za leo Alhamisini ni kati ya JKT Queens dhidi ya Evergreen utakaofanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam wakati Fair Play inacheza na Viva Queens ya Mtwara kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Mechi nyingine itakuwa ni kati ya Victoria Queens ya Kagera itakuwa mgeni wa Majengo kwenye Uwanja wa Namfua ulioko Singida pia Marsh Acedemy ya Mwanza itacheza na Sisterz ya Kigoma kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
..…………………………………………………………………………........................
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment