Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa kwanza kulia), akisisitiza jambo wakati wa
mkutano wake na ujumbe kutoka nchini Denmark, ukiongozwa na Waziri wa nchi
anayeshughulikia Sera, Bw. Martin Hermann, walipokutana Makao Makuu ya Wizara
ya Fedha na Mipango Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Nchi
anayehusika na masuala ya Sera, Bw. Martin Hermann (kulia) akiwa na ujumbe wake
wakati wa mazungumzo kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip
Mpango (hayupo pichani), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar
es salaam, ambapo nchi hizo zimekubaliana kuendeleza ushirikiano utakaojikita
katika masuala ya uwekezaji na biashara kwa faida ya pande zote mbili. Kushoto
ni Balozi wa Denmark hapa nchini Bw. Einar Jansen.
Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto), akisisitiza jambo wakati wa mkutano
wake na ujumbe kutoka nchini Denmark, ukiongozwa na Waziri wa nchi
anayeshughulikia Sera, Bw. Martin Hermann, (hayupo Pichani) walipokutana Makao
Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam. Kulia ni Katibu Mkuu
wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James.
Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw.
Doto James, wakifuatilia kwa umakini mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha na
Mipango Dkt. Philip Mpango na Waziri wa Nchi anayeshughulika na masuala ya Sera
wa Denmark, Bw. Martin Hermann (hawapo pichani), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha
na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Nchi
anayehusika na masuala ya Sera kutoka Denmark, Bw. Martin Hermann (kushoto)
akimkabidhi Dkt. Mpango, nyaraka za kampuni zinazoonesha nia ya kuwekeza
Tanzania katika Sekta ya Gesi na Mafuta wakati akiongoza ujumbe wa nchi hiyo
katika mazungumzo kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip
Mpango (kulia), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na
Mipango Dkt. Philip Mpango (katikati) akiangalia nyaraka alizokabidhiwa na
Waziri wa Nchi wa Serikali ya Denmark anayehusika na Sera, Bw. Martin Hermann,
wakati wa mazungumzo kati yao yaliyojikita katika masuala ya kuimarisha
ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili. Kulia ni Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Doto James na kulia kwa Waziri Dkt. Mpango, ni Naibu
Katibu Mkuu Dkt. Khatib Kazungu.
Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa pili kushoto) akiwa na wageni wake kutoka
Serikali ya Denmark wakiongozwa na Waziri wa Nchi anayehusika na Sera, Bw.
Martin Hermann (kushoto), baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati yao ambapo
masuala kadhaa yamejadiliwa ikiwemo kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kijamii
hususan katika uwekezaji na biashara, mazungungo yaliyofanyika Makao Makuu ya
Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto) akipeana mkono wa shukurani na mgeni
wake kutoka Serikali ya Denmark, Waziri wa Nchi anayehusika na Sera, Bw. Martin
Hermann (kushoto), baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati yao yaliyogusa
Nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii hususan katika uwekezaji na biashara,
mazungunzo yaliyofanyika makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar
es salaam.
Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (kushoto) akiwasindikiza wageni wake kutoka
nje ya jengo la Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam
baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati ya ujumbe wa Serikali ya Denmark na
Tanzania uliolenga kuimarisha uhusiano katika masuala ya uwekezaji na biashara.
(Picha na Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini, WFM)
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam
SERIKALI
ya Denmark imeahidi kuwashawishi wawekezaji wakubwa kutoka nchini humo kuja
kuwekeza hapa nchini katika sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Viwanda, Bandari, Gesi
na Mafuta.
Ahadi
hiyo imetolewa Jijini Dar es salaam na Waziri wa Nchi wa Serikali ya Denmark
anayeshughulikia Sera, Bw. Martin Hermann, alipokutana na kufanya mazungumzo na
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Makao Makuu ya Wizara hiyo.
Bw. Hermann
alielezea kufurahishwa kwake na namna Serikali ya Awamu ya Tano ilivyojipanga
kuwatumikia wananchi wake kwa kuwaletea maendeleo ya haraka ya kiuchumi pamoja
na kuimarisha uwajibikaji, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, na kusema kuwa
nchi yake inaunga mkono juhudi hizo.
Alisema
kuwa nchi yake itasaidia juhudi hizo kwa kuzishawishi kampuni kubwa zenye
mitaji na uwezo wa kiteknolojia kutoka sekta binafsi ili zije ziwekeze hapa
nchini na hivyo kushiriki katika kukuza uchumi wa nchi.
Amesisitiza
pia umuhimu wa serikali kuwekeza juhudi kubwa katika kuendeleza kilimo kwa kuwa
sekta hiyo inaweza kuchochea na kutoa mchango mkubwa na wa haraka wa ustawi na
maendeleo ya wananchi.
Aidha,
Bw. Hermann, ambaye aliambatana na Balozi wa Denmark hapa nchini, Bw. Einar
Jensen, amesifu utendaji mzuri wa Rais Mhe. Dkt. John Magufuli katika mapambano
dhidi ya vitendo vya ufisadi ikiwemo rushwa na kuishauri Serikali kuweka mfumo wa
vita hiyo utakaokuwa endelevu.
Kwa
upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, alisema Serikali
inathamini mchango mkubwa wa Denmark katika kukuza uchumi na maendeleo ya Taifa
kwa ujumla kwa kusaidia miradi ya maendeleo na ushauri wa kisera.
“Katika
kipindi cha zaidi ya miaka 50 ya uhusiano kati ya nchi hizi mbili tumeshuhudia
Serikali ya Denmark ikichangia maendeleo yetu katika nyanja zinazokwenda
sambamba na vipaumbele vya maono ya mipango yetu ya maendeleo katika sekta za
fedha, miundombinu, kilimo, afya na elimu”alisisitiza Dkt. Mpango.
Dkt.
Mpango aliishauri nchi hiyo kwamba mwelekeo wa uhusiano huo sasa uwe katika
kushirikiana kiuchumi kwa kuhamasisha uwekezaji na biashara kati ya pande hizo
mbili.
Alifafanua
kuwa amejaribu kutafuta takwimu za kiwango cha uagizaji na uingizaji wa bidhaa
kati ya Tanzania na Denmark lakini cha kusikitisha hakuna biashara hiyo jambo
ambalo amesema inabidi lilisisitizwe katika mfumo mpya wa ushirikiano kwa kuwa
kuna fursa nyingi zinazoweza kusaidia pande zote mbili kiuchumi.
Alisisitiza
kuwa mwelekeo huo ni muhimu utiliwe mkazo sambamba na jitihada za Serikali za
kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuwekeza hapa nchini huku akitoa
wito kwa kampuni za Denmark zilizopo hapa nchini pia kuvuta kampuni nyingine
kutoka nchini mwao kuja kuwekeza Tanzania.
Dkt.
Mpango, amewakaribisha wawekezaji hao kuwekeza katika katika sekta za ufugaji
wa samaki, ujenzi wa viwanda vya kuchakata samaki, ufugaji wa ng’ombe wa kisasa
na viwanda vya kusindika nyama na maziwa, hatua itakayo saidia kukuza mitaji,
kuongeza tija katika sekta hizo na
ajira kwa kundi kubwa la vijana.
Kuhusu
ushauri uliotolewa na Waziri wa nchi wa Denmark anaye shughulikia Sera, Bw.
Martin Hermann wa kujenga mfumo endelevu wa kupambana na rushwa na ufisadi,
Dkt. Mpango amesema kuwa Serikali imeanzisha mahakama maalumu ya mafisadi
ambayo anaamini ni moja ya ujenzi wa mifumo hiyo endelevu ya kupambana na
vitendo hivyo.
No comments:
Post a Comment