Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Prof. Adolf Mkenda (kushoto), akiwa pamoja na Mkuu wa wilaya ya Momba mkoani
Songwe, Bw. Juma Irando (katikati), na maafisa kadhaa wa Wizara ya Fedha na
Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara naUwekezaji, wakitoka katika Ofisi za
Mkurugenzi wa Mji wa Tunduma kuelekea mpakani mwa Tanzania na Zambia eneo la
Tunduma na Nakonde.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina
Khamis Shaaban (aliyeshika mkoba), Mkuu wa Wilaya ya Momba mkoani Songwe, Bw.
Juma Irando (aliyeshika mikono yake), Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara
na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda (Aliyesimama nyuma ya Mkuu wa wilaya),
wakisikiliza maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania-Tunduma, Bw. Magori Cosmas (wa pili kulia), kuhusu maandalizi
ya kuanzisha rasmi Kituo cha Pamoja cha Mpakani Tunduma/Nakonde katika nchi za
Tanzania na Zambia.
Afisa Mifumo ya Kompyuta wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA,
Bw. Yasin Kilima (aliyeshika simu katikati), akitoa ufafanuzi wa namna TRA
ilivyojiandaa kuweka mifumo itakayo saidia kurahisisha kazi ya utoaji huduma wa
pamoja na wenzao wa Zambia, mbele ya Ujumbe ulioongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban (wa pili kulia laiyevaa
miwani), wakati walipotembelea mpaka wa Tanzania na Zambia kujionea maandalizi
ya kuanzishwa rasmi kwa Kituo cha Pamoja cha Mpakani unaotarajiwa kuanza
Februari mosi, 2017.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Prof. Adolf Mkenda (kushoto), akisisitiza jambo wakati timu kutoka Wizara ya
Fedha na Mipango na wizara yake walipotembelea na kukagua miundombinu ya Ofisi
ya Uhamiaji Kituo cha Mpakani cha Tunduma.
Mkuu wa Wilaya ya Momba, mkoani Songwe, Bw. Juma Irando,
akiongea jambo wakati timu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara
ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, ilipofanya ziara katika Kituo cha mpakani
cha Tunduma/Nakonde kuangalia maandalizi ya uanzishwaji wa Kituo cha Pamoja na
Mpakani baada ya kusainiwa kwa mikataba kati ya Tanzania na Zambia, na kutakiwa
kuanza rasmi mwanzoni mwa Februari, 2017.
Kaimu Afisa Uhamiaji Mfawidhi wa Kituo cha mpakani
Tunduma/Nakonde, Bw. Tabaran Mzee (kulia), akiueleza ujumbe kutoka Wizara ya
Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji namna idara yake
ilivyojiandaa kuanza kutoa huduma ya pamoja mpakani kati ya maofisa kutoka
Zambia na Tanzania ambao watakuwa wakitumia ofisi moja kuwahudumia watu
wanaotumia mpaka huo kuvuka kwenda kila upande wa nchi (Tanzania na Zambia)
Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara
ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, wakiwa pamoja na maofisa wa mamlaka ya
Mapato kutoka Zambia wakiangalia hali ya biashara na uwekezaji katika Mpaka wa
Tunduma na Nakonde ikiwa ni maandalizi ya kuanza rasmi kwa utoaji wa huduma wa
pamoja kati ya nchi hizo mbili ili kuboresha mazingira ya biashara baada ya
kusainiwa kwa mikataba ya kuanzishwa kwa huduma hiyo katika mpaka huo
Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara
ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, wakiwa pamoja na maofisa wa Mamlaka ya
Mapato kutoka Zambia (ZRA) walipotembelea upande wa pili wa mpaka huo-Nakonde
ili kujionea maandalizi ya kuanza rasmi kwa Kituo cha Pamoja cha Mpakani kati
ya Tanzania na Zambia baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya kuanzishwa kwa
huduma hiyo Februari mosi, 2017
Kituo cha Forodha cha Nakonde Upande wa Zambia
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Zambia-Nakonde, Bw. Nase Lungu,
(aliyenyoosha mkono), akitoa maelezo namna ofisi yake ilivyojipanga kuhudumia
wateja wao kupitia utaratibu mpya wa kushirikiana kwenye jengo moja kati ya
maafisa wa Forodha wa Tanzania na Zambia, wakati Ujumbe kutoka nchi hizo mbili
walipotembelea mpaka huo kujionea maandalizi yalipofikia kabla ya kuanza rasmi
kwa utaratibu huo Februari Mosi, 2017
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Prof. Adolf Mkenda (katikati), akisalimiana na mmoja wa madereva wanaoendesha
malori kwenda Zambia, kabla ya kusikiliza kero zao mbalimbali, ambapo
malalamiko makubwa yalikuwa ni kutumia muda mrefu mpakani mwa Tunduma/Nakonde
kunakowatia hasara na kuchelewesha biashara
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Prof. Adolf Mkenda (wa pili kulia), akitoa maelekezo namna ambavyo maofisa wa
TRA Tanzania na Zambia wanavyopaswa kushughulikia kero za madereva na wananchi
wanaotumia mpaka wa Tanzania na Zambia (Tunduma na Nakonde) ili kuboresha
biashara mpakani hapo
Ujumbe wa Tanzania na maafisa wa Zambia walipotembelea na
kukagua miundombinu ya utoaji huduma pamoja baada ya kutiwa saini kwa mikataba
ya kuanza kwa Kituo cha Pamoja cha Mpakani, (Tunduma/Nakonde), huduma
inayotarajiwa kuanza rasmi Februari Mosi, 2017
Ujenzi wa Kituo cha Pamoja Mpakani upande wa
Tanzania-Tunduma, ukiendelea kwa kasi na una tarajiwa kukamilika baada ya miezi
16 ijayo
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)
Na Benny Mwaipaja, WFM, Songwe
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
Prof. Adolf Mkenda, amewaonya mawakala wa forodha katika mpaka wa Tanzania na
Zambia wa Tunduma/Nakonde kuacha Mara moja tabia ya kuwachelewesha madereva wa
malori yaendayo masafa marefu kwa makusudi ili wapewe
rushwa.
Prof. Mkenda ametoa onyo hilo katika mpaka huo wa
Tunduma na Nakonde, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya madereva
wa malori waliodai wamekuwa wakicheleweshwa kuvuka mpaka huo kwa zaidi ya siku
tatu hadi tano.
Wadereva hao wameeleza kuwa mawakala wa forodha
wamekuwa wakiwaambia kuwa nyaraka zao zinazohusika na mizigo wanayosafirisha
zimekuwa zilicheleshwa na kituo cha Forodha upande wa Zambia.
Hata hivyo Meneja wa Mamlaka ya Mapato Zambia
(ZRA), Kituo cha Nakonde, Bw. Nase Lungu, amekana kuhusika na ucheleweshaji huo
na baada ya ukaguzi wa moja ya nyaraka hizo ilibainika kuwa upande wa Zambia
unatoa nyaraka hizo kwa wakati lakini zimekuwa zikifichwa na Mawakala wa
Forodha upande wa Tanzania.
Wakitoa ufafanuzi wa tuhuma hizo, madereva hao
wamesema kuwa mawakala wa forodha kwa muda mrefu wamekuwa wakiwaeleza kuwa
mtandao wa intaneti wa Upande wa Zambia unaotumika kuchakata nyaraka zao uko
chini, hivyo walitakiwa kutoa shilingi 10,000 kwa kila nyaraka ili
"kurahisisha" kazi hiyo kwa kuwapa kitu kidogo maafisa wa forodha wa
Zambia.
"Mawakala wengine wa forodha wana nyumba zao
za kulala wageni hapa Tunduma kumbe wanatulazimisha kukaa hapa ili tulale
kwenye nyumba hizo hali inayotutia hasara na wanatumia kutokujua kwetu
kutudanganya kwamba mtandao uko chini wakijua hatuna uwezo wa kufuatilia huko
Zambia" alieleza kwa masikitiko dereva mmoja
Baada ya kubaini uwepo wa vitendo hivyo, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda, ameagiza
Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA upande wa Tunduma kuandika kibao chenye namba za
simu za Mkuu wa TRA mpakani hapo zitakazotumiwa na madereva wanaocheleweshwa
kwa makusudi kutoa malalamiko yao.
"Tunataka madereva mtumie siku moja tu
kukamilisha nyaraka zenu ili muendelee na safari yenu vinginevyo tutadumaza
biashara kati ya Zambia na Tanzania na pia tutaifanya Bandari yetu ya Dar es
salaam kushindwa kuleta tija" aliongeza Prof. Mkenda
Alisema kuwa wakala wa forodha atakayebainika
kufanya mchezo huo mchafu wa kuwarubuni madereva na kuwachelewesha kupeleka
mizigo nchini Zambia, watanyang'anywa leseni zao za biashara.
Meneja Msaidizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania, mikoa ya Songwe na Mbeya, Bw. Jomimassa Nsindo, amesema kuwa ofisi
yake itashirikiana na madereva kukomesha vitendo hivyo ambavyo amesema
vinaharibu uchumi na biashara mpakani hapo.
Naye Mkuu wa wilaya ya Momba, mkoani Songwe, Bw.
Juma Irando, alisema kuwa ataitisha kikao cha Madereva, Mawakala wa Forodha na
Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA katika Mpaka huo wa Tunduma/Nakonde mapema, ili
kuweka msimamo wa serikali na kuwaeleza wahusika wanaokiuka taratibu hatua
watakazochukuliwa.
Prof. Mkenda na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban, walikwenda katika mpaka huo wa
Tunduma na Nakonde, kuangalia maandalizi ya uanzishwaji wa Kituo cha Pamoja cha
Mpakani kati ya Tanzania na Zambia, unaotarajiwa kuanza Februari mosi, 2017,
baada ya kusainiwa kwa mikataba kati ya nchi hizo mbili, juzi.
No comments:
Post a Comment