Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania Ibrahimu
Kaduma aliyemtembelea Makamu wa Rais na kumuelezea mikakati ya kuanzisha Chuo cha Joseph Business School.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia) akizungumza na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania Ibrahimu
Kaduma aliyemtembelea Makamu wa Rais na kumuelezea mikakati ya kuanzisha Chuo cha Joseph Business School kushoto ni Meneja Mradi Dkt Charles Sokile.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na ujumbe wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania uliomtembelea ofisini kwake, Ikulu jijini Dar es Salaam.
..............................................................
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameuhimiza uongozi
wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania kuharakisha mchakato wa
kuanzisha Chuo cha Joseph Business School hapa nchini chuo ambacho kitatoa
mafunzo mbalimbali ya biashara, maadili ya uongozi na ugunduzi wa mawazo ya
biashara ili kusaidia mamia ya Watanzania kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.
Makamu wa
Rais ametoa kauli ofisini kwake Ikulu Jijini Dar es Salaam leo alipokutana na
kufanya mazungumzo na Viongozi wa Taasisi
ya Kingdom Leadership Network Tanzania ambao walimtembelea Makamu wa Rais kumweleza
hatua ambazo wamefikia katika uanzishaji wa Chuo hicho.
Makamu wa
Rais Samia Suluhu Hassan amesema wazo la uanzishaji wa Chuo hicho ulitolewa na
Dkt Bill Winston ambaye ni Mwanzilishi wa Winston Ministries mwaka jana katika
Maombezi ya Taifa ambaye yeye alikuwa mgeni rasmi katika maombi hayo, anasema
aliupokea kwa furaha mpango huo kwa sababu chuo hicho kitasaidia watanzania
wengi kupata elimu na ujuzi wa kuimarisha biashara zao wakati taifa likielekea
kwenye uchumi wa Viwanda.
Amesema
hatua za uanzishwaji wa Chuo hicho hapa nchini ni fursa pekee na nzuri kwa
Watanzania kujifunza ubunifu na ugunduzi katika biashara, maadili ya uongozi
katika biashara ili kuongeza ufanisi katika biashara zao kwa ajili ya manufaa
yao na taifa kwa ujumla hasa katika ulipaji wa kodi.
Kwa Upande
wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania Ibrahimu
Kaduma na Meneja Mradi Dkt Charles Sokile wamemhakikishia Makamu wa Rais kuwa hatua
ambazo wamefikia kwa sasa katika uanzishaji wa Chuo hicho ni nzuri ambapo mpaka
sasa wamepata majengo kwa ajili ya ofisi na maeneo ya kufundishia na hatua za
usajili wa chuo hicho zipo katika hatua za mwisho.
Wamesisitiza
kuwa wanataka kushirikiana ipasavyo na Serikali katika uanzishaji wa chuo hicho
ambacho kitatoa elimu ya biashara hasa ugunduzi wa mawazo ya biashara nchini kama
hatua ya kutekeleza kwa vitendo dhana ya kuelekea kwenye uchumi wa viwanda
nchini.
No comments:
Post a Comment