Na Daniel
Mbega
YAMETOKEA
tena ndani ya Chadema, kama ilivyokuwa mwaka 2010. Viti Maalum vya ubunge
vimeleta nongwa na vimezidi kudhihirisha wazi hakuna demokrasia ndani ya chama
hicho cha upinzani.
Pengine
walichofanikiwa mwaka huu ni ‘kuwalipa fadhila mashushushu’ wao waliokuwa ndani
ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwapatia ubunge wa viti maalum.
Lakini
kidonda bado kibichi japo kinaonekana kukauka. Ndani kinafukuta. Na daima
kidonda kiko kwako, kwa mwenzio hakiumi!
Naam.
Nilisema mwaka 2010 mara tu baada ya kukamilika kwa zoezi la uteuzi wa wabunge
wa viti maalum, kwamba kulikuwa na undugunaizesheni katika uteuzi ule. Kama
kawaida, wapo waliopinga kwamba andiko langu lilikuwa ‘la kinafiki’ kama
ambavyo watasema hata sasa.
Wakati ule
nilisema kulikuwa na figisu nyingi tangu katika uchaguzi wa kwanza wa viti
maalum kupitia chama hicho, kwa sababu ilidaiwa kulikuwa na hujuma huku baadhi
ya wagombea wakidaiwa kuwachukua mamluki ili wawachague.
Uongozi wa
juu ukaingilia kati na kusitisha zoezi hilo kwa maelezo kwamba wateule wa viti hivyo
wangepatikana kulingana na matokeo ya kura za ubunge katika uchaguzi mkuu kwa
kuangalia wanawake ambao walijitokeza kwenye majimbo na kushindwa, ambao ndio
wangepewa kipaumbele cha kwanza.
Kwa
kifupi, njia ya kura ilishindikana kutokana na kuibuka kwa makundi ya
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Naibu Katibu Mkuu (wakati huo), Zitto
Kabwe, wakati wa uchaguzi wa wabunge hao kupitia wajumbe wa Baraza la Wanawake
wa Chadema (Bawacha).
Ndipo
hatimaye wakaamua kumtumia mtaalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
‘school mate’ wangu wa enzi zile Pugu Sekondari, Prof. Kitila Mkumbo,
mwanaharakati mahiri tangu tulipokuwa na mijadala ya kupitisha mfumo wa vyama
vingi mwaka 1992.
Kulikuwa
na vigezo kadhaa ambavyo vilipaswa kuzingatiwa kwenye uteuzi huo, miongoni
mwake ni mchango wa muombaji katika kukijenga na kukiimarisha chama tangu mwaka
2005 hadi 2010, kiwango cha elimu cha muombaji (kuanzia Shahada ya Uzamivu,
Shahada ya Uzamili, Shahada ya Kwanza, Stashahada, Kidato cha Sita, cha Nne au
Darasa la Saba) na pia mchango wa muombaji katika kampeni za uchaguzi 2010.
Yakapatikana
majina 105 ya wateule hao ambayo orodha yake iliwasilishwa kwenye Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC) Septemba 30, 2010 na Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema John
Mnyika.
Waliopewa
kipaumbele, na ambao walipitishwa, walikuwa wake, watoto na ndugu wa vigogo na
viongozi wa chama hicho, wakiwemo pia wabunge wote wa viti maalumu wa Chadema
waliomaliza muda wao, na waliokuwa wakigombea katika majimbo ya uchaguzi ambao
walirudishwa katika orodha hiyo na kupewa nafasi za juu.
Waliomaliza
muda wao na kurejea tena Bungeni kupitia viti maalum ni Lucy Owenya (mtoto wa aliyekuwa
Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo), huyu alikuwa wa kwanza kwenye
orodha hiyo.
Wengine ni
dada-binamu wa Zitto Kabwe, Mhonga Said Ruhwanya (alikuwa namba 3), Grace
Kiwelu (alikuwa wa 9 - ambaye ni mkwewe Ndesamburo), Anna Maulida Komu (13),
Susan Anselem Lyimo (10), Rose Kamil Sukum (19 - ambaye ni mke wa zamani wa Dk.
Willibrod Slaa).
Halima
Mdee alishika nafasi ya tano kwenye orodha hiyo, lakini yeye alipenya moja kwa
moja baada ya kushinda kwenye Jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam. Walioshindwa
kwenye majimbo ni pamoja na Rose Kamili (Hanang’), Leticia Musobi Nyerere
(Kwimba), Regia Mtema (Kilombero), Anna Komu (Kigamboni), na Mwanamrisho Abama.
Wengine
waliopita walikuwa Christina Lissu Mughwai (dada wa Tundu Lissu), Joyce Mukya
(mzazi mwenzake na Mbowe), Paulina Slaa Narcis, Easther Matiko, Anna Mallac,
Paulina Gekul, Conjesta Rwamlaza, Susan Kiwanga, Christowaja Mtinda, Joyce
Mukya, Naomi Kaihula, Chiku Abwao, Raya Hamisi, Philipa Mturano, Mariam Msabaha,
Rachel Mashishanga, mwanahabari Rebecca Mngodo, na Cecilia Pareso.
Ndiyo. Ni
wale wale wenye nasaba na ujamaa na viongozi wa juu wa Chadema, ambao kwa kiasi
kikubwa ndio waliokuwa wakitajwa hata katika uchaguzi kwamba walikuwa
wanapendelewa.
Sinema
bado inaendelea. Baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Tume ya
Taifa Uchaguzi (NEC) ilitangaza mgawanyo wa wabunge wa viti maalum kwa CCM,
Chadema pamoja na Chama cha Wananchi (CUF), ambapo CCM ilipata wabunge 64,
Chadema 36 na CUF 10.
Baada ya
mgawanyo huo, vyama mbalimbali vya kisiasa vilifanya michakato yao ya ndani na
kutangaza majina ya wabunge husika watakaoviwakilisha vyama vyao.
Malalamiko
yakaibuka zaidi kwa Chadema, ambapo mpaka sasa baadhi ya wanachama
bado wanahoji vigezo vilivyotumika kupata majina ya wateule. Tuhuma za
kuwepo kwa urafiki na undugu zimeelezwa na wanaolalamika.
Baadhi ya
majina ambayo yamesikika yakilalamikiwa ni pamoja na Anna Gideria, ambaye
aliteuliwa huku akiwa bado Katibu wa UVCCM Wilaya ya Mbulu mkoani
Manyara. Kwa hiyo alilazimika kujiuzulu kwanza nafasi ya ukatibu na
kukabidhi barua yake kwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Manyara, Regina Ndege kabla
hajapokea uteuzi mpya.
Minong’ono
inaeleza kuwa Gideria alipoteza imani na CCM baada ya jina la Waziri Mkuu wa
zamani, Frederick Sumaye, kukatwa katika kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea
Urais kwa tiketi ya CCM na kufuatia kitendo hicho cha Sumaye kukatwa, aliomba
likizo ya mwezi mmoja – kumbe ‘akatoroka’ pamoja na Sumaye kwenda Chadema.
Tukio hilo liliwashtua
wanaChadema wilayani Mbulu hususan waliokuwa wakimuona Gideria kama
kiongozi na mpambanaji wa CCM na hivyo kuteuliwa kwake kulionekana kuwakatisha
tamaa wanaChadema wilayani humo wanaojiuliza kwanini wachukuliwe wanaCCM huku
wakiwaacha wapambanaji wa Chadema ambao walikuwa wakikipigania chama usiku na
mchana.
Kwa upande wa
Zanzibar, vyombo vya habari viliripoti
juu ya Bawacha Zanzibar kushusha bendera za chama hicho na kufunga ofisi za
katika mikoa ya Unguja na Pemba, kupinga uteuzi wa wabunge Viti Maalum baada ya
Zanzibar kukosa hata nafasi moja japo wanasema ilikuwa ipate walau nafasi tano.
Alinukuliwa
Makamu Mwenyekiti wa Bawacha Zanzibar, Hamida Abdallah Aweshi, akisema kuwa
wamechoka na maamuzi yaliyofikiwa na kwamba Makao Makuu ya Chadema walikataa
kusikiliza kilio chao.
Katika mikoa ya
Mbeya na Songwe, Bawacha ilitangaza kutounga mkono uteuzi wa wabunge hao kwa
madai kuwa haukuzingatia usawa na haki kwa wanachama. Mwenyekiti wa Bawacha
anayewakilisha mikoa hiyo, Happiness Kwilabya alisema wanawake wa Chadema
wamekatishwa tamaa kwa kiasi kikubwa na uteuzi wa wabunge hao uliofanywa bila
kuzingatia haki na sawa.
“Tumesikitishwa
na uteuzi usioeleweka umetumia vigezo gani sijui. Tunakusudia kukutana ili
kutoa tamko letu rasmi,” alisema na kuhoji: “Je, ni haki kwa Mkoa wa Songwe
ambao una wabunge watatu wa Chadema kutokana na mchango mkubwa wa wanawake,
kukosa mbunge wa viti maalum?”
Kauli
iliyotolewa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati za Wagombea Ubunge wa Chadema na
Umoja wa Katika ya Wananchi (Ukawa) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jacob Kalua
kuwa wanawake wa Chadema waliokuwa mstari wa mbele kukisadia chama,
hawajateuliwa na badala yake wamepewa nafasi watu ambao hawakushiriki popote,
iliongeza ukakasi na kutoa taswira hasi kwa Chadema.
“Hapa Mbeya
ameteuliwa mmoja, lakini ushiriki wake kwenye chama unazidiwa na wanawake
wengine walioomba nafasi hiyo waliopo hapa. Kwa upande pia wa mkoani Songwe
kuna majimbo matatu ya Chadema hajateuliwa mwanamke hata mmoja. Je, hii ni
halali?” alikaririwa akihoji Kalua.
Wakati Mbeya
wakihoji, wenzao wa mkoa Rukwa walifika mbali zaidi kufuatia kujiuzulu
kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa, Kapteni Zeno Nkoswe, kutokana
na kutoridhika na uteuzi wa wanawake mkoani humo.
Nkoswe alisema
sababu ya kuachia ngazi ilitokana na hali ya sintofahamu ya wanachama wa mkoa
huo waliokuwa wakimhoji mara kwa mara juu ya uteuzi uliofanywa wa mtu ambaye
wanasema alikuwa akikipigia debe chama cha TLP.
Uteuzi mwingine
uliolalamikiwa ni ule wa Zubeda Sakuru kwa Mkoa wa Ruvuma. Walalamikaji
walihoji uhalali wa kuletewa Mbunge wa Viti Maalum kutoka Tanga kwani inaelezwa
kwamba, Sakuru aliihadaa Chadema kuwa kwao ni Ruvuma wakati ni mwenyeji wa
Tanga.
Naibu Katibu
Mkuu Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema mchakato wa kuwatafuta wabunge hao
huanzia ngazi za chini katika majimbo na kwamba wanachama walihusishwa huku
akisema wanaotoa hoja za upendeleo ni wa kupuuzwa.
Haya ni majibu
mepesi kwa maswali magumu. Na kama majibu hayo aliyoyatoa ni sahihi Je,
ilikuwaje Katibu wa UVCCM Wilaya ya Mbulu, Anna Gideria akateuliwa na Chadema
kuwa mbunge wa viti maalum huku wapambanaji wa muda mrefu wakiachwa? Au alikuwa
‘shushushu’ wao ndani ya CCM?
Hili ni suala
nyeti kwa Chadema, na kama halikupatiwa ufumbuzi, ‘kansa’ hiyo inaweza
kuwaangamiza kabisa mwaka 2020.
0656-331974
CREDIT: RAIA TANZANIA, DEC. 11, 2015
No comments:
Post a Comment