Na Tausi Ally, Mwananchi
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru Johnson Lukaza na mdogo wake Mwesigwa Lukaza baada ya kuwaona hawana hatia katika kesi ya wizi wa wa Sh 6.3 bilioni za akaunti ya madeni ya Nje (EPA) iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akitoa hukumu hiyo jana Kiongozi wa jopo la Mahakimu watatu wanaoisikiliza kesi hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu, Edson Mkasimongwa alisema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi saba wa upande wa mashtaka na utetezi wa washtakiwa hao anaona upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka pasipo kuacha shaka.
Mashtaka matano yaliyokuwa yakiwakabili hao ni pamoja kula njama, kughushi, kuwasilisha hati za uongo za makubaliano ya kuhamisha deni kati ya kampuni yao ya Kernel Ltd na kampuni Marubeni ya nchini Japan na kujipatia kiasi hicho cha fedha cha Sh 6.3 bilioni kwa njia ya udanganyifu.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mkasimongwa amesema wamewaachia huru washtakiwa hao katika makosa hayo yote kwa sababu ushahidi wa upande wa mashtaka haukujitosheleza kwa kuwa ulishindwa kuthibitisha kama ni kweli Novemba 2,2003 washtakiwa hao walighushi hati ya makubaliano ya kuhamisha deni la Sh 6.3 bilioni baina ya kampuni ya Kernel Ltd na Marubeni ya nchini Japan ilikuwa ni ya kughushi.
Jaji Mkasimongwa anasema ushahidi unaonesha kampuni hiyo ya Marubeni ya nchini Japan ilikubali kupokea kiasi hicho cha fedha na kwamba washtakiwa wao walipata asilimia tu ya 20 ya fedha hizo na upande wamashtaka hakuwahi kulibishia hilo.
Katika kesi hiyo, Johnson Lukaza ambaye ni Mwenyekiti wa makampuni ya Proin na ni Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UB) pamoja na mdogo wake Mwesiga walikuwa wanatetewa na Wakili Alex Mgongolwa aliyekuwa akisaidiwana na Wakili Alex Mshumbusi.
Baada ya hukumu hiyo kutolewa ndugu wa washtakiwa hao waliaza kulia mahakamani hapo pamoja na mshtakiwa Mwesiga wakiwa hawa amini kilichotokea huku wakisema asante Yesu, asante Yesu.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment