Na Mwandishi Wetu, BrotherDanny5 Blog
Arusha: WADAU wa huduma za usafiri wa daladala jijini Arusha wamepitisha rasmi azimio la kuanzisha usafiri wa daladala wa njia ndefu Januari 15 mwakani ili kuondoa msongamano wa daladala katikati ya jiji.
Azimio hilo limetolewa Desemba 19 kwenye kikao cha wadau hao kilichoshirikisha Mamlaka ya usimamizi na udhibiti wa usafiri wanchi kavu na majini,Sumatra,Baraza la huduma za wasafiri ,Sumatra CCC, Halmashauri ya jiji la Arusha.
Wadau wengine ni jeshi la polisi kikosi cha usalama bara barani, na Chama cha wamiliki wa mabasi yatoayo huduma za usafiri mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, AKIBOA, ambao ni wamiliki wa daladala ,pamoja na wasimamizi wa bara bara za daladala jijini Arusha .
Wadau hao walikuwa wakijadili marekebisho ya mapendekezo ya njia na nauli ambazo zitatozwa kulingana na umbali yaliyowasilishwa na Sumatra kwa mara ya pili baada ya kikao cha kwanza kilichofanyika Desemba 12 ukumbi namba 40 kuahirishwa kutokana na mahudhulio hafifu ya wadau ambapo wajumbe waliokuwepo waliagiza taarifa hiyo ikaboreshe.
Akiwasilisha taarifa hiyo ya maboresha, kwenye kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa halmashauri ya jiji la Arusha,afisa mfawidhi wa Sumatra mkoa wa Arusha, Johns Makwale, amesema taarifa hiyo inatokana na mapendekezo ya wadau waliyoyatoa katika vikao mbalimbali baada ya kuona kuna haja ya kuwepo kwa njia ndefu.
Kwa vipindi tofauti mwaka huu kumekuwepo na vikao mfululizo vya wadau kutafuta ufumbuzi wa kupunguza msongamano katikati ya jiji la Arusha .
Katika mapendekezo ya wadau sanjari na azimio hilo baadhi ya njia zilizokuwa zikitumika kwa ajili ya daladala zitafutika na kuwepo na njia mpya ambazo zimependekezwa.
Kuanzishwa kwa njia ndefu ni mwanzo wa kuondoka kwa mabasi madogo ya abiria aina ya Toyota hiace,na kutoa fursa kuingia mabasi ya kati aina ya Coaster kuweza kutoa huduma za usafiri kwa abiria kwa kuwa zina uwezo wa kuhimili safari ndefu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kikao hicho,Diwani Paulo Matsoni, wa kata ya Moshono , amesema katikati ya mji kumekuwa na msongamano wa dalada ambazo zimekuwa ni kero kwa watumiaji wengine wa bara bara hivyo kuanzishwa kwa njia hizo ndefu kutapunguza msongamano.
Matsoni ambae pia ni mwenyekiti wa kamati ya mipango miji jiji la Arusha,ameongeza kuwa halmashauri itashirikiana na wadau wengine kutoa elimu kupitia vyombo vya habari kwa wananchi kuhusu mabadiliko hayo ambayo yanalenga kuboresha huduma hiyo na kuondoa msongamano wa daladala kati kati ya jiji .
No comments:
Post a Comment