Na Daniel Mbega,
Mbarali
MWEKEZAJI
katika Shamba la Mpunga la Kapunga wilayani Mbarali, kampuni ya Kapunga Rice
Project Limited (KRPL), ameikodisha Serikali ya Kijiji shule aliyoijenga.
Wakati
mwekezaji anaikodisha shule hiyo, hatma ya shule ya umma iliyojengwa na
serikali mwaka 1991 katika eneo la mradi ambayo mwekezaji huyo ameifunga tangu
mwezi Mei 2013 mpaka sasa bado haijajulikana.
Mwekezaji
huyo aliifunga shule hiyo kwa maelezo kwamba iko kwenye eneo lake alilouziwa na
serikali mwaka 2006.
Hata
hivyo, shule iliyojengwa na mwekezaji kwenye eneo lake lenye ukubwa wa hekta 3.5
jirani na kitongoji cha Site One badala ya lile aliloelekezwa na wanakijiji,
imekodishwa kwa kipindi cha miezi 30 tu (miaka miwili na nusu) kuanzia Julai 8,
2013 hadi Desemba 31, 2015 huku serikali ya kijiji ikitakiwa kulipa Shs. 1 kwa
mwaka kama gharama ya ukodishwaji huo.
Mkataba
wa maridhiano ya ukodishaji uliosainiwa na mwekezaji Wally Vermaak, Mwenyekiti
wa Serikali ya Kijiji cha Kapunga Ramadhan Nyoni na Mwanasheria wa Halmashauri
ya Wilaya ya Mbarali Mikidadi Athumani siku ya Ijumaa Julai 5, 2013 unaonyesha
mkanganyiko wa maelezo yake.
Miongoni
mwa vipengele vinavyokanganya ni kile kinachoeleza kwamba mkataba huo utakoma
Desemba 31, 2015 wakati kingine kinasema ni mkataba wa kudumu hadi pale
serikali itakapotoa hati tofauti za ardhi, ambapo kimsingi mwekezaji huyo kwa
miaka nane sasa anasema eneo lote ni lake na kuwataka wanakijiji wa Kapunga
waondoke.
Aidha,
ili kupata haki ya kumiliki eneo hilo la shule, mkataba huo unasema Halmashauri
ya Kijiji cha Kapunga na Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ndio washughulikie
mgawanyo huo wa hati miliki.
Emmanuel
Kasekwa, mkazi wa Kapunga, ameshangazwa na taarifa kwamba mwekezaji
amewakodisha shule bila kujua hatma ya fidia ya shule ya umma.
“Kama
alitaka kufidia shule baada ya kuifunga ile ya umma kwenye eneo lake, kwa nini
atukodishe hii? Tena kwa nini alikataa kuja kujenga hapa kijijini akaijenga
kwenye eneo lake? Serikali ituambie kuhusu ile shule ya umma inafidiwaje.”
alisema.
Mkuu wa Wilaya hajui
Hata
hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Gullamhussein Kifu, alikanusha taarifa kwamba
mwekezaji huyo ameifunga shule ya msingi na akasema mwenye uwezo wa kufanya
hivyo ni serikali.
Kifu
alisema hana taarifa ya mwekezaji kuikodisha kwa serikali ya kijiji shule ya
msingi aliyoijenga ndani ya eneo lake, lakini alipoulizwa inakuwaje anashindwa
kujua hilo wakati mkataba umesainiwa na Mwanasheria wa Halmashauri, alisema:
“Kama hamna ushahidi msipende kuwazushia watu, inaweza kuleta matatizo makubwa.”
Uchunguzi
unaonyesha kwamba, mwekazaji aliikabidhi shule hiyo Julai 5, 2013 ambapo Mkuu
wa Wilaya akiwa ameongozana na Mwanasheria wa Wilaya ndiye aliyepokea funguo za
shule na kumkabidhi mwenyekiti wa Kijiji cha Kapunga.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ramadhan Nyoni,
alikiri kwamba aliyepokea funguo hizo ni Mkuu wa Wilaya, Gullamhussein Kifu na
akamkabidhi yeye.
“Baada
ya kunikabidhi akaniambie niende nikasaini mkataba huo kwa niaba ya serikali.
Nikasaini tukiwa pamoja na Mwanasheria wa Wilaya, lakini sikujua vipengele
vilikuwa vinasemaje kwa sababu mkaataba umeandikwa kwa lugha ya Kiingereza,”
alisema mwenyekiti huyo.
Walitaka sekondari
Aidha,
inaelezwa kwamba, baada ya kukabidhiwa shule hiyo, Halmashauri ya Kijiji
iliitisha mkutano Julai 18, 2013 na suala la shule hiyo lilikuwa agenda ya tatu
ambapo walipendekeza itumike kama shule ya sekondari ya Kata ili kuwasaidia
wanafunzi kutoka vijiji vya Kata ya Itamboleo.
“Imeazimiwa
kuwa shule aliyokabidhi mwekezaji iwe shule ya sekondari ambayo itanufaisha
Kata ya Itamboleo ambayo ina vijiji vya Kapunga, Itamboleo, Mbalino na
Matebete, hata hivyo (wananchi) wameona haiwezi kuwa shule ya msingi kwa kuwa
eneo lake ni hatari kwa watoto wadogo kiusalama kwani kuna mfereji wa maji,”
yalisema maazimio ya kikao hicho, ambayo nakala yake ilipelekwa kwa Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya kwa Kumb. Na. MB/KIJ/936/DED/Vol. 1/06.
Mgogoro wa shule
Mgogoro
kuhusu shule ya msingi Kapunga unakwenda sanjari na mgogoro wa ardhi ya kijiji
hicho tangu serikali ilipouza lililokuwa Shamba la NAFCO Kapunga mwaka 2006 kwa
Kampuni ya Export Trading Co. Ltd.
Taarifa
za uchunguzi zinaeleza kwamba, baada ya mwekezaji kuuziwa shamba hilo kwa
thamani ya Shs. 2.311 bilioni, aliwafukuza walimu wote
waliokuwa wakiishi katika nyumba zilizojengwa na shirika.
Hali hiyo
iliwafanya walimu hao kwenda kupanga Chimala, umbali wa kilometa 26 kutoka
shuleni na kulazimika kutembea kwa miguu ama kukodi bodaboda kila siku.
Williard Sengele (58) ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kapunga,
anasema yeye na familia yake ya watu sita walilazimika kuishi kwenye chumba cha
darasa tangu Desemba 6, 2006 hadi Januari 6, 2007 kutokana na kukosa mahali
pengine pa kuishi kabla ya kupata nyumba ya kupanga Chimala.
Anasema tangu wakati huo, walimu karibu wote wamekuwa wakitembea
umbali wa kilometa 52 kila siku kwenda na kurudi shule, hali ambayo imeleta
changamoto kwa baadhi ya vipindi kutofundishwa ipasavyo.
“Walimu wengi wamekuwa wakichelewa kwa sababu wanaishi Chimala,
ambako walihamia baada ya kufukuzwa mwaka 2006 kutoka kwenye nyumba walizokuwa
wakiishi wakati NAFCO ikimiliki shamba la mpunga la Kapunga,” anasema Sengele.
Shule hiyo ilijengwa na NAFCO mwaka 1991 baada ya kuanza
uzalishaji kwenye shamba hilo. Shirika
hilo liliihamisha shule hiyo iliyosajiliwa rasmi mwaka 1977 ikiwa na Hati Na.
MB 08/1/022 kutoka kijijini hadi kwenye eneo la shirika ikiwa ni njia ya
kuwapatia makazi bora walimu ambao walikuwa wakiishi kwenye nyumba zilizoezekwa
kwa nyasi kijijini. Kufuatia uhamisho huo, majengo ya zamani ya shule pamoja na
nyumba za walimu yakabomolewa.
Mwekezaji
agoma
Wakati alipoifunga shule ya umma kwenye eneo lake, mwekezaji huyo
aligoma kusikiliza ushauri wa viongozi wa kijiji wa kwenda kujenga shule hiyo
mahali ilipokuwepo awali kabla ya kuhamishiwa kwenye eneo la mradi kwa maelezo
kwamba hata wanakijiji wanatakiwa kuhama.
Hali hiyo iliwakasirisha wanakijiji hao ambao waliamua kuchanga
fedha na nguvukazi na kujenga vyumba 9 vya madarasa, ofisi mbili za walimu,
vyoo pamoja na nyumba mbili za walimu.
Tayari shule hiyo inafanya kazi tangu ilipofunguliwa Julai 8,
2013.
Mgogoro
uliopo
Tangu kuuzwa kwa shamba hilo, mgogoro wa
ardhi unaendelea kufuatia mwekezaji kusema hata Kijiji cha Kapunga kimo ndani
ya eneo lake ambalo amekabidhiwa hati yenye namba 6249 ikionyesha kwamba eneo
hilo lina ukubwa wa hekta 7,850.
Hata hivyo, wananchi wanapinga madai
hayo na kuilaumu serikali kwamba iliuza shamba, kijiji na huduma za jamii kwa
makosa kwa vile shamba lililokuwa linamilikiwa na NAFCO ni hekta 5,500 tu
ambazo Halmashauri ya Kijiji iliridhia kulitoa kwa serikali katika kikao
kilichofanyika Novemba 14, 1985.
Inaelezwa
kwamba, mradi huo uliofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) ulilenga
kujenga miundombinu ya shamba la NAFCO la hekta 5,500 na shamba la wakulima
wadogo lenye ukubwa wa hekta 800, wakati ambapo eneo la kijiji ni hekta 1,070.
Kwa kuwa
mradi wote ulikuwa ukijulikana kama Mradi wa Umwagiliaji Kapunga (KRIP) ukiwa
na hati moja tu, serikali ilipouza shamba la NAFCO haikujishughulisha
kutengeneza hatimiliki ya shamba hilo na badala yake kutoa hatimiliki ya jumla,
ambayo ilihusisha kijiji, shamba la wakulima wadogo na lile la NAFCO.
“Hali hii ikafanya
kijiji kiuzwe pamoja na huduma zote za jamii, mwekezaji hataki kuamini ukweli
kwamba hata eneo ambalo lilitangazwa kwenye zabuni ni hekta 5,500 na siyo 7,850
kama anavyong’ang’ania,” anasema Brighton Ngella, mkazi wa Kapunga.
Sera ya Taifa ya Uwekezaji
inaelekeza kwamba, mwekezaji anapaswa kuendeleza huduma za jamii kama shule na
zahanati katika maeneo yanayozunguka mradi wake.
Sergei Bekker, meneja
uzalishaji wa Kapunga Rice Project Limited, aliwahi kumweleza mwandishi wa
habari hizi kwamba wangejenga shule katika eneo la Site One na kuihamisha ya
sasa katika eneo hilo ili kuisaidia jamii.
“Hatuwezi kujenga shule kwenye
Kijiji cha Kapunga kwa sababu ni ardhi yetu. Tulitaka kujenga kule Matebete,
lakini serikali imesema wananchi wale wanapaswa kuhamishwa kwani ni eneo la
TANAPA. Wakazi wa Kapunga hawataki kututambua kama wawekezaji na hili ndilo
tatizo linalochelewesha mradi wa ujenzi wa shule,” alisema.
Katika ziara
yake ya Januari 2014, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa
Anna Tibaijuka, alisema mwekezaji huyo anapaswa kurejesha hekta 1,870 kwa
wananchi bila masharti yoyote.
No comments:
Post a Comment