Wafuasi wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kislam, Shekh Ponda Issa Ponda, wakiwa nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa mkoa wa Morogoro baada ya kuzuiwa kuingia ndani ya chumba cha mahakama.
Na Ashton Balaigwa, Morogoro
Kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kislamu, Shekh Ponda Issa Ponda, jana ilikwama kuanza kusikilizwa huku mawakili wa pande mbili za mashtaka na utetezi wakivutana kuhusiana na mshtakiwa kupewa dhamana.Kesi hiyo iliyoko mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, Mary Moyo, ilitajwa jan huku kukiwa na mabishano kuhusu kuanza rasimi kusikilizwa pamoja na mtuhumiwa kupewa dhamana.
Wakili kiongozi wa jopo la utetezi, Juma Nassoro, alitaka kesi hiyo ianze kusikilizwa kwa madai kuwa taratibu za awali zilishakamilishwa kwa upande wa mashtaka na kumuomba hakimu kuipangia tarehe ya kuanza kusikilizwa badala ya kutajwa.
Alidai kuwa kama kuna nyongeza au mabadiliko kwa upande wa mashtaka unaweza kufanyika huku kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa.
Katika ombi lake la pili, aliiomba mahakama kulifuta shitaka la mshtakiwa kwenda kinyume na amri ya Hakimu Mkazi wa Kisutu, Dar es Salaam iliyotolewa Mei 9, 2013 ambayo ilitoa adhabu ya kifungo cha nje cha mwaka mmoja na kumtaka mshtakiwa asifanye jambo lolote la uvunjifu wa amani badala yake ahubiri suala la amani.
Wakili huyo aliambia Mahakama kuwa mshtakiwa alikata rufaa Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam kupinga hukumu hiyo na kuwa hukumu iliyotolewa Novemba 27, mwaka huu na Jaji Augustine Shangwa, alifuta hukumu ya mahakama ya Kisutu ambalo ndio msingi wa shtaka namba moja ya kesi iliyopo Mahakama ya Mkoa wa Morogoro.
Wakili huyo alidai kuwa kutokana na hukumu ya Jaji Shangwa, shtaka namba moja halina uhalali, hivyo mahakama inapaswa kuliondoa au kutoa muongozo.
Katika ombi lake la tatu wakili huyo alidai kuwa kutoka na mazingira yaliyobakia kwa sasa haki halisi na maslahi ya haki ya kimahakama yanatoa haki kwa mshtakiwa kupewa dhamana na hivyo kuiomba mahakama kuangalia haki ya mshtakiwa kupata dhamana kwa kuzingatia hukumu ya Jaji Shangwa.
Wakili mwingine wa utetezi, Bathoromew Tarimo, alidai kuwa mteja wao yupo rumande tangu Agosti 2013 licha ya upande wa mashtaka kukamilisha ushahidi, hivyo mshtakiwa anayo haki ya kupatiwa dhamana na kesi yake kuanza kusikilizwa.
Hata hivyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili mkuu wa Serikali kanda ya Mashariki, Benard Kongola, akishirikiana na Wakili wa Serikali mkoa wa Morogoro, Sunday Hyera, walipinga maombi yote matatu.
Kongola alidai kuwa maamuzi ya mahakama moja hayawezi kuingilia uhuru wa mahakama nyingine na kwamba hati ya mashtaka ipo moja na ina makosa matatu na kupinga kwamba haijabomoka kama alivyodai Tarimo.
Alisisitiza kesi iendelee kutajwa kwa kuwa upande wa mashtaka wamechelewa kuipata hukumu ya Jaji Shangwa ili waipitie na kuanza kuandaa mashahidi kwa ajili ya kutoa ushahidi wa kesi hiyo na kudai kuwa hoja ya upande wa utetezi haina mashiko.
Hakimu Moyo alisema hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi zina msingi,l akini anakubaliana na hoja zilizotolewa na upande mashtaka kwa kuwa hata Mahakama hiyo haijapata nakala ya hukumu ya Jaji Shangwa licha ya upande wa utetezi kumkabidhi nakala muda mfupi kabla ya kesi hiyo kuanza.
Alisema anapaswa kuipitia kwa kina hukumu hiyo ili kuwa muongozo wa uendeshaji wa kesi hiyo na kukubalina na hoja ya upande wa mashtaka kuwa kesi hiyo iendelee kutajwa huku mshtakiwa akiendelea kubaki rumande na kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Januari 5, mwakani.
Shekh Ponda alifikishwa mahakamani hapo majira ya saa 3.15 asubuhi akiwa ndani ya gari ndogo yenye namba za kiraia huku akisindikizwa na magari ya Polisi huku wafuasi wake wachache waliruhusiwa kuingia katika chumba cha mahakama. Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Leonard Paul alikuwa miongoni mwa walikuwa wakisikiliza kesi hiyo .
Waumini waliobaki nje ya uzio walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za dini yao na baadaye kuendesha sala pembezoni mwa uzio wa mahakama mpaka kesi ilipoharishwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment