Arusha. Wanafunzi 344 waliomaliza darasa la saba mwaka huu mkoani hapa wamebainika kuwa hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu. Ofisa elimu wa mkoa, Nestory Mloka alitoa taarifa hiyo juzi katika kikao cha elimu kilichoitishwa kwa ajili ya kuchambua matokeo ya mtihani wa darasa la saba na kuwapangia shule wahitimu waliofaulu.
Mloka alisema kati ya walihitimu hao ambao hawajui kusoma na kuandika, wavulana ni 163 na wasichana 181.
Alisema Wilaya ya Ngorongoro yenye wakazi wengi wafugaji wa jamii ya Kimasai, ndiyo ina idadi kubwa ya wanafunzi hao wenye tatizo hilo wanaofikia 230.
“Idadi ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika kwa Wilaya ya Ngorongoro ni kubwa kuliko sehemu nyingine zote za Mkoa wa Arusha,” alisema Mloka.
Hata hivyo, alisema wanafunzi 23,250 wamefaulu mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2014, sawa na asilimia 67.69 ya waliofanya mtihani.
Mloka alisema wanafunzi wote waliofaulu wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule mbalimbali.
Alisema wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ni kati ya wanafunzi 34,348 waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2014 mkoani Arusha.
“Kati ya wanafunzi 34,348 waliofanya mitihani, wavulana walikuwa 16,474, wakati wanafunzi wa kike walikuwa 18,454,” alisema Mloka.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment