Na Fidelis Butahe na Andrew Msechu, Mwananchi
Dar es Salaam. Hatima ya mawaziri na watendaji waliotajwa katika sakata la uchotwaji wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow itajulikana Jumatatu ijayo wakati Rais Jakaya Kikwete atakapohutubia taifa kupitia mazungumzo na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Hotuba hiyo ya Rais Kikwete inafanyika ikiwa imepita wiki moja iliyopangwa kukamilisha uchambuzi na kutoa uamuzi dhidi ya wahusika.
Hatua hiyo ya kusogeza mbele muda wa Rais Kikwete kuzungumzia suala hilo inazidi kuwaweka tumbo joto mawaziri na viongozi wengine wanaotuhumiwa kuhusika katika sakata hilo.
Taarifa za awali zilizotolewa na vyombo kadhaa vya habari zilieleza kuwa Rais Kikwete angezungumza jana alasiri, lakini Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilikanusha na kutoa taarifa nyingine, ikieleza kuwa atazungumza Jumatatu.
“Rais Kikwete atazungumzia masuala mbalimbali ya kitaifa, yakiwamo yale ambayo yamekuwa yanasubiri uamuzi wake tangu alipokuwa anajiuguza kufuatia upasuaji aliofanyiwa mwezi uliopita,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo, baadaye Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Salva Rweyemamu alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa tayari Rais Kikwete ameshatoa uamuzi wake kuhusu suala la escrow na kwamba atautangaza Jumatatu.
Baadhi ya mambo yaliyotokea nchini wakati Rais Kikwete akiwa Marekani alikokwenda kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa tezi dume, ni pamoja na sakata la escrow ambapo Bunge lilipitisha maazimio manane, likiwamo la kumtaka Rais Kikwete kuwachukulia hatua mawaziri na watendaji wa Serikali waliotajwa kuhusika katika wizi wa mabilioni hayo.
Rais Kikwete atatoa hotuba hiyo zikiwa zimepita siku nne tangu alipokatisha ziara ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika Falme za Kiarabu kwa kile alichokieleza kwamba ni kuitwa nyumbani kwa shughuli maalumu, kitendo kilichotafsiriwa kuwa ni kwa ajili ya kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu sakata la escrow.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata ndani ya Serikali zinasema kuwa utendaji wa kazi wa baadhi ya mawaziri, wakuu wa wilaya na hata baadhi ya watendaji walioko chini yao umeshuka kutokana na kila mmoja kutojua jinsi uamuzi wa Rais Kikwete utakavyokuwa.
Desemba 9 mwaka huu, Ikulu ilitoa taarifa ya kuwa Rais Kikwete ameshaanza kusoma Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Umma (PAC) na maazimio ya Bunge kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow na atatoa uamuzi ndani ya wiki moja ijayo.
Katika taarifa hiyo, Rais Kikwete alielekeza kuwa Ripoti ya CAG iwekwe hadharani kwenye vyombo vya habari vinavyofikia watu wengi kwa ajili ya umma kuisoma na kujua nini hasa kimesemwa na kupendekezwa, jambo ambalo hadi sasa halijafanyika.
Juzi, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema, “Rais Kikwete bado ana nia ya kuzungumza na atafanya hivyo wiki hii kabla ya Jumamosi (leo). Hakusema siku atakayozungumza, alisema atazungumza wiki hii.”
Alisema Rais Kikwete pia atafanya uteuzi wa wakuu wa wilaya kabla ya mwaka huu kuisha kutokana na baadhi ya wakuu wa wilaya kufariki dunia, kustaafu na wengine kurejea jeshini. “Nadhani wanaweza kufikia 10 hivi,” alisema.
Kuhusu ripoti ya CAG, Sefue alisema iliagizwa ofisi ya CAG iweke ripoti hiyo katika mtandao wake, sijafuatilia ila nadhani wameweka maana ninaiona ikichapwa katika vyombo vya habari.”
Katika kuonyesha kuwa hotuba hiyo ya Jumatatu imebeba ujumbe mzito, jana mchana Ikulu ilikana taarifa zilizotolewa awali kuhusu mkutano wa Rais Kikwete na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, uliotarajiwa kufanyika jana alasiri, kwa maelezo kwamba Ofisi ya Rais haikuwa imetoa taarifa za mkutano huo.
Taarifa hiyo ya awali ilitangazwa na kuthibitishwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abilahi Mihewa akieleza kwamba Rais Kikwete atazungumza na wazee wa mkoa huo katika Ukumbi wa Blue Pearl Ubungo jijini Dar es Salaam jana.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana usiku zinaeleza kuwa kikao kizito kilikuwa kikifanyika Ikulu, huku nyingine zikieleza kuwa jambo lolote kubwa kuhusu sakata hilo linaweza kutokea leo au kesho kutokana na uamuzi wa Rais unaweza kuwa hitimisho la sakata hilo.
Salva Rweyemamu
Rweyemamu alionyesha kushangazwa na taarifa hizo alizoziita za ‘mtandaoni’ ambazo zilichapishwa na baadhi ya magazeti (siyo Mwananchi) na kutangazwa na baadhi ya redio na televisheni, kwamba Rais angefanya mkutano huo jana.
Wakati hayo yakitokea, kuchelewa kwa uamuzi dhidi ya watuhumiwa hao kumetajwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa mtihani kwa watuhumiwa kutokana na kutojua hatua zitakazochukuliwa dhidi yao.
Mbali na mawaziri na watendaji, vile vile wakuu wa wilaya nao wameendelea kuwa njiapanda kutokana na tamko la Rais Kikwete kuwa amewapangua na wengine kutengua uteuzi wao, upangaji wa vituo vipya ukabaki kumsubiri Waziri Mkuu.
Wasomi
Wakizungumza na gazeti hili Profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chris Maina alisema, “Uamuzi ulitakiwa kutolewa mapema kwa sababu ripoti zote tatu ziliwataja wahusika na makosa waliyoyafanya. Jambo hili halikuhitaji uchunguzi wala fikra mpya.”
Alisema wahusika walitakiwa kujiuzulu baada ya kutolewa kwa ripoti hizo na si kusubiri kuwajibishwa kwa kuwa suala hilo linahitaji uaminifu zaidi kuliko uamuzi wa kisheria.
“Huwezi kuwa kiongozi wakati wananchi wana mashaka na wewe, busara ni kung’atuka tu. Unawezaje kwenda ofisini wakati unatuhumiwa,” alisema.
Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema, “Rais hawezi kuchukua uamuzi wa kushinikizwa na mataifa mengine yaliyotishia kutotoa msaada kwa sababu ya suala hili, ila kifupi ni kwamba makosa ya wachache yasihesabiwe kama makosa ya Watanzania wote.”
Alisema udhaifu unaowakabili Watanzania unatakiwa kushughulikiwa na Watanzania wenyewe na siyo kushinikizwa na watu wengine. “Naamini Rais atachukua hatua, lakini pia anaweza asichukue hatua yoyote kwa sababu rais hashinikizwi na mtu na hakuna pa kumshtaki. Tusubiri tuone uamuzi utakaotolewa,” alisema.
Profesa Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuendelea kuwapo kazini kwa watuhumiwa wa wizi wa mabilioni hayo unatokana na nchi kuwa na Katiba inayompa rais madaraka makubwa.
“Bunge lilitoa uamuzi wake ambao ulipewa baraka pia na Serikali, lakini badala ya wahusika kuchukuliwa hatua inaagizwa ufanyike uchunguzi mwingine.
Mamlaka makubwa ya rais yanaminya uamuzi wa vyombo vingine,” alisema. Alisema hivi sasa Bunge kazi yake ni kushauri na kupendekeza, kwamba anayeshauriwa ana uwezo wa kukataa au kukubali ushauri husika.
“Bunge linatakiwa kupewa meno ili liwe na uwezo wa kuamrisha jambo,” alisisitiza.
Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Faraja Christoms alisema, “Utendaji wa Rais Kikwete una falsafa ya ‘huu ni upepo utapita’. Inatakiwa kila linapotokea tatizo rais azungumze na kutoa uamuzi, hii itasaidia kuongeza uwajibikaji kwa watendaji wa Serikali.”
Alisema ukimya ukizidi unaweza kuondoa imani ya wananchi kwa Serikali yao, wanaweza kudhani kuwa kuna watu wanaohusika ambao wako nyuma ya watuhumiwa waliotajwa kuchota mabilioni ya escrow na ndiyo maana hakuna hatua zilizochukuliwa hadi sasa.
Alisema ukimya katika sakata la escrow ni moja ya sababu ya CCM kupata upinzani mkali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama alisema: “Tusubiri kuona nini kitafuata, ni muhimu kwa hatua kuchukuliwa yanapotokea mambo yanayogusa masilahi ya nchi.”
Maazimio ya Bunge
Baada ya mjadala wa Tegeta Escrow, Bunge liliazimia kwamba:
1. Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria, kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, watu wote waliotajwa na taarifa maalumu ya kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Escrow na watu wengine watakaogundulika kuhusika katika vitendo hivyo vya jinai kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea.
2. Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao.
3. Kamati husika za Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa 18 wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa kamati husika za kudumu za Bunge.
4. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde Tume ya kijaji ya uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
5. Serikali iandae na kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria iliyoiunda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahususi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.
6. Mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi, ziitaje Stanbic Bank (Tanzania) Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika, kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
7. Bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za shirika hilo.
8. Serikali itekeleze Azimio la Bunge la kuitaka iwasilishe mikataba husika bungeni au kwenye Kamati zake kwa lengo la kuliwezesha kutekeleza vyema wajibu wake wa kuisimamia na kuishauri Serikali mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile, kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti ya Serikali ya mwaka 2015/16.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment