Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umelitaka Bunge kuiwajibisha Serikali ikiwa Rais Jakaya Kikwete atashindwa kutekeleza maazimio ya Bunge ikiwamo kumng’oa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Wakizungumza hapa jana, viongozi hao walisema endapo Rais atashindwa kumwajibisha Profesa Muhongo, basi wabunge wao watawasilisha hoja na kushawishi wengine kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu na umoja huo utaitisha maandamano nchi nzima.
Mwenyekiti mwenza wa umoja huo, Profesa Ibrahim Lipumba alihoji kwa nini Rais Kikwete anasita kumwondoa Profesa Muhongo wakati Bunge lilishatoa maazimio.
Alisema Bunge linalowakilisha wananchi zaidi ya milioni 45 liliazimia uteuzi huo utenguliwe lakini akaelezea kushangazwa kwake na hatua ya Rais kusema bado anachunguza.
“Hivi Rais anachunguza nini, haliamini bunge? Kama anavyoteua mawaziri pia ana madaraka ya kutengua nafasi zao, sasa anasita nini wakati azimio la Bunge limemwelekeza. Kama Rais Kikwete atashindwa kumwajibisha Muhongo atakuwa ameshindwa kutekeleza moja ya maazimio ya Bunge na Ukawa utaliomba Bunge kuiwajibisha Serikali.”
Alisema hotuba aliyoitoa Jumatatu wakati akiwahutubia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, haijakidhi matarajio ya wengi kwani kuna maazimio hayajatekelezwa.
Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF, alisema Rais amekataa kutekeleza azimio la kutaka mitambo ya IPTL itaifishwe na kutoa sababu ambazo hazina mashiko.
“Tangu mitambo ya IPTL imefungwa Taifa limepata hasara kubwa kwa sababu umeme unaouzwa ni wa gharama kubwa kuliko mitambo yoyote ya umeme inayotumika katika bara la Afrika, Taifa limeingia hasara kubwa, Rais aitaifishe,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema katika hotuba hiyo Rais Kikwete alionyesha kuipendelea IPTL na kuikandamiza Tanesco wakati akielezea kuwa fedha za escrow zilikuwa mali ya IPTL.
Alitaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika na ufisadi wa Akaunti ya Tegeta Escrow na wengine walionufaika nazo.
“Sheria ya maadili itungwe upya ili iweke uwazi wa mtu yeyote kuona taarifa ya mali za viongozi.”
Mbatia na Dk Slaa
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia aliwataka viongozi wa dini kuliombea Taifa katika kipindi hiki ambacho mihimili ya dola inapingana.
“Tuna matatizo makubwa, malori ya fedha yanachotwa benki kwa siku moja lakini Usalama wa Taifa hawashtuki, viongozi wa dini liombeeni Taifa, tuna mtikisiko,” alisema Mbatia.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema amesikitishwa na hotuba ya Rais kwa kutowataja wahusika waliochota Sh73 bilioni katika Benki ya Stanbic wakati kuna Idara ya Usalama wa Taifa.
“Hivi kweli Serikali yenye Usalama wa Taifa haiwafahamu waliochota fedha hizo?” alihoji Dk Slaa.
LHRC yashangazwa
Wakati viongozi hao wakisema hayo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeeleza kusikitishwa kwake na utekelezaji wa maazimio manane ya Bunge juu ya sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo - Bisimba alisema katika taarifa yake kuwa hotuba ya Rais Kikwete kupitia kwa wazee wa Dar es Salaam Jumatatu iliyopita, iliikumbatia kampuni ya IPTL na kutupa maazimio mengi ya Bunge kutokana na kutochukuliwa hatua zilizotarajiwa.
Licha ya kwamba tayari Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema ameshajiuzulu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kufutwa kazi na Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakimu Maswi kusimamishwa kazi, Dk Bisimba alisema Rais hakuchukulia suala hilo kwa uzito na kwa kiwango kinachotakiwa.
Alisema badala yake, hotuba ya Rais ilijaa masihara katika kashfa nzito inayoipa kibarua kigumu Serikali katika kupambana na rushwa.
Alimtaka Rais Kikwete apokee heshima aliyopewa na Bunge ya kufanya uamuzi na kwamba kutofanya hivyo kutamshushia heshima kwa Watanzania.
Dk Bisimba alisema masuala ya escrow, umiliki wa PAP/IPTL, tuhuma za rushwa na kodi za Serikali yalikuwa yameshafafanuliwa na Kamati ya Bunge na Hesabu za Serikali (PAC) lakini kwa bahati mbaya, Rais aliyarudia upya na kuegemea upande wa IPTL.
“Rais katika hotuba yake alikuwa anapangua kila hoja kiasi kwamba alitoa hitimisho la kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti ile hazikuwa za Serikali, bali za IPTL, jambo ambalo si sahihi.”
Alisema kauli ya kutaka uchunguzi uendelee juu ya masuala hayo inaibua utata wa uchunguzi ufanywe na nani tena zaidi ya Bunge kupitia CAG na Takukuru na kwamba matokeo yake apewe nani?
Mdee: Tibaijuka abanwe zaidi
Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee alisema Rais Kikwete anatakiwa kumchukulia hatua zaidi Profesa Tibaijuka ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wa umma.
Kauli hiyo ya Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chadema) inatokana tuhuma za ukosefu wa maadili kwa waziri huyo baada ya akaunti yake binafsi kuingiziwa Sh1.6 bilioni katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow, ambazo alisema zilikuwa za kusaidia shule.
Akizungumza na gazeti hili jana Mdee alisema: “Suala hili halitakiwi kuishia kwa kumvua uwaziri.
Mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu anatakiwa kuchukua hatua zaidi ya hapo ili kuwa fundisho wa watumishi wengine.
“Rais Kikwete ndiye anayeweza kuifanya nchi hii ikaendelea zaidi na yeye mwenyewe anaweza kuwafanya viongozi wake wakawa wawajibikaji na waadilifu lakini ukisema mtu anakosea unamfukuza kazi, tutakuwa tunafanya mambo ya kuigiza. Rais azingatie ipasavyo maazimio ya Bunge kama yanavyosema.”
Alipoulizwa atamkumbuka kwa lipi waziri Profesa Tibaijuka katika wizara hiyo, Mdee alisema, “Katika kipindi chote akiwa waziri wa ardhi sina cha kumkumbuka kwani migogoro ya ardhi ndiyo kwanza imeongezeka, wakulima na wafugaji kila kukicha ni mapigano, tunahitaji mtu atakayeiongoza wizara hiyo ipasavyo na kupunguza migogoro ya ardhi inayogharimu uhai wa wananchi.”
Imeandikwa na Raymond Kaminyoge, Nuzulack Dausen na Ibrahim Yamola, Mwananchi
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment