Na Salim Mohammed, Mwananchi
Korogwe. Wakulima na wafanyabiashara wa matunda wilayani Korogwe wanalazimika kuuza mazao yao kwa bei ya chini ili yasiharibike kutokana na kukosa soko.
Walisema hayo jana katika Mji mdogo wa Mombo na kuomba wawekezaji kujenga kiwanda cha kusindika matunda wilayani hapa.
Walisema kuuza matunda yao kwa bei ya hasara, kunarudisha nyuma kasi ya maendeleo na kusababisha baadhi yao kuachana na kilimo.
“Kama unavyoona hapa matunda ni mengi sana hadi tunapata hofu ya kutuozea mikononi... zikipita siku mbili kama hujamaliza mzigo, lazima yataharibikia,” alisema Jumanne Ramadhani.
“Tunalazimika kuuza kwa bei yoyote ile... hatuna soko rasmi la kuuzia matunda na tuko juu juu na kutokuwa na uhakika wa kuuza kutegemea mteja mmoja mmoja siyo biashara.”
Mkulima wa mapeazi, Miraji Shemdoe alisema wakulima wamepunguza kasi ya kilimo hicho na kusababisha sehemu kubwa ya mashamba kuwa pori.
Aliitaka Serikali kukisikiliza kilio chao cha muda mrefu kwa kuwa wamekuwa wakipewa matumaini, lakini hadi leo hakuna walichosaidiwa na matokeo yake wengi kujikuta kwenye umaskini.
Shemdoe alisema wakulima wa Lushoto na Korogwe wana nafasi nzuri ya kujikwamua na umaskini kutokana na ardhi yao kutotegemea mvua za misimu.
“Tumejaliwa kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba, lakini soko ndiyo shida. Wakulima wengi wamebadilisha aina ya kilimo na siyo matunda tena,” alisema Shemdoe.
Alisema kama kungekuwa na soko la uhakika, wakulima wangeshawishika kulima matunda kwa wingi na Serikali kupata mapato yatakayosaidia huduma mbalimbali za kijamii.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment