Nicholaus Mgaya
Dar es Salaam. Uongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) umetakiwa kujiuzulu kwa tuhuma za kushindwa kuliongoza kifaida shirikisho hilo, huku Katibu Mkuu wake akiwekwa kikaangoni akidaiwa kuhusika na hali hiyo na kung’ang’ania madaraka licha ya muda wake wa kustaafu kufika.
Kauli hizo zilitolewa jana jijini Dar es Salaam na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Tucta waliokutana kujadili hatma ya shirikisho baada ya kutolewa kwa ripoti ya mkaguzi wa hesabu za mapato na matumizi iliyoonyesha kasoro kadhaa.
Wakizungumza kwa jazba nje wa ukumbi wa mkutano, baadhi ya wajumbe walimlaumu Katibu Mkuu, Nicholaus Mgaya kuwa ndiye aliyelifikisha shirikisho hilo hapo lilipo na kwamba umri wa kustaafu umefika lakini anataka kuendelea kukaa madarakani.
Mjumbe wa Kamati Kuu Taifa, WilliamMboma alisema ingawa Tucta ina majengo mengi nchini, imekuwa ikikusanya mapato kidogo kwa mwezi, wakati jengo moja lililopoArusha lina uwezo wa kukusanya zaidi ya Sh600 milioni.
“Ghorofa la Arusha tu endapo mapato yatasimamiwa tungeweza kupata zaidi ya Sh600 milioni kwa mwezi lakini leo hii tunaambiwa kuwa majengo yote Tanzanianzima tunakusanya Sh13 milioni, inawezekana fedha zinaingia hazijulikani zinakokwenda,” alisema Mboma.
Alibainisha kuwa ripoti ya hesabu za mapato na matumizi ya Tucta iliyofanywa na kampuni ya Ernst & Young inaonyesha kuwa shirikisho hilo limeshindwa kukusanya fedha kutoka katika vyanzo vyake.
Pia alisema kuwa Tucta imekuwa ikishindwa kutekeleza maagizo mbalimbali yanayoagizwa na Baraza Kuu, hivyo katika kikao hicho walipendekeza Kamati Kuu itoke nje ili wajadili hatma ya shirikisho, lakini walizuiwa kutekeleza uamuzi huo.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Idrisa Washington alisema kikao hicho kimekuwa na msuguano baina ya wajumbe kwa kuwa hiyo ni hali ya kawaida wakati watu wanapotaka kuleta mabadiliko yenye kuleta maendeleo. “Katika dunia ya demokrasia kila mtu ana mawazo yake, haya ni masuala mazito, kuna pande mbili, shirikisho na Serikali mwisho wa siku lazima kuwa na mvutano,” alisema Washington.
Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la Tucta, Musa Mnyeti alisema mgogoro ndani ya shirikisho hilo ulianza mwaka jana baada ya Katibu Mkuu, Nicholas Mgaya kutuhumiwa kutumia madaraka yake vibaya.
“Alitumia madaraka vibaya kwenye Chuo cha wafanyakazi Mbeya, alipendelea watu wa kwenda kusomaAfrika Kusini na Italia, pia alifanya upendeleo kwa namna mkuu wa chuo aliyemaliza muda alivyotakiwa kupata stahili zake,” alisema Mnyeti.
Mjumbe mwingine wa Baraza, Lameck Mahewa, alisema kikao hicho kilipaswa kuwa wazi kwa waandishi kuingia, lakini katika hali isiyofahamika, waliambiwa wakae nje wasubiri hadi kitakapomalizika.
“Msajili wa vyama na shirikisho anatakiwa kutazama upya namna Tucta inavyoendeshwa, mikataba imefichwa haipo wazi, mibovu inayowanufaisha wachache,”
Waandishi wa habari walipopata nafasi ya kuingia kwenye ukumbi huo, walimwaomba Katibu Mkuu, Mgaya kuzungumzia masuala yaliyojiri kwenye kikao hicho, lakini alisema yeye siyo msemaji wa Tucta na kwamba hakumwita mwandishi yeyote.
Akizungumza nje ya ukumbi wa mkutano huo, Kaimu Rais wa Tucta, Nortimuga Masikini alisema hakuna maazimio yoyote yaliyofikiwa na kwamba hakuna suala lolote lililooneka kuleta mvutano.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment