Na Daniel Mbega
KAMA kuna kitu
ambacho Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikipigania kwa nguvu zote mpaka
anaingia kaburini ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (Muungano wa Tanzania)
ambao leo umetimiza miaka 50 tangu kusainiwa kwa nyaraka zake.
Katika miaka ya
mwisho ya uhai wake hili lilionekana dhahiri ambapo alilifanya kwa vitendo, si
maneno peke yake. Hatua ya kwanza ilikuwa ile ya mwaka 1994 alipozima hoja ya
Mbunge wa Chunya, Njelu Kasaka, ya kudai serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.
Hakuishia hapo,
akatoa kitabu cha ‘Uongozi wetu na hatma
ya Tanzania’ kilichochapishwa nchini Zimbabwe mwaka 1994 ambapo pamoja na
maneno makali aliyotumia, pia alitumia tenzi kuwananga wale waliokuwa
wakiupinga ama kuubeza Muungano na kutishia mustakabali wake.
Mwaka uliofuata
wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi alifikia mahali akasimama
kidete, akisaidiana na wanachama wengine wa CCM (pengine waliopata nguvu kuona
Nyerere yupo nyuma yao), wakazima jaribio la rais wa Zanzibar wa wakati ule Dk.
Salmin Amour Juma aliyetaka kuifanyia marekebisho Katiba ya Serikali ya
Mapinduzi ili apate nafasi nyingine ya kugombea urais kwa mara ya tatu ifikapo
mwaka 2000.
Wakati wa
uchaguzi mkuu wa CCM wa mwaka 1997 Mwalimu alilazimika kwenda mwenyewe
Chimwaga, Dodoma ingawa hakuwa amealikwa, na kwenda kuzima majaribio kadhaa
yaliyokuwa yameandaliwa na ‘vijana’ wa chama hicho kutaka kumng’oa Makamu
Mwenyekiti wa CCM Bara, John Samuel Malecela, na badala yake wakapanga
wamchague Waziri Mkuu wa wakati huo, Fredrick Sumaye. Akafanikiwa.
Mambo haya yote
yalimuudhi na kumkera sana Mwalimu kwa sababu aliamini, japokuwa hakuwa kwenye
wadhifa wowote – si wa chama au serikali – kwamba kama asingesimama kidete ustawi
wa Muungano, ambao ulikuwa umeanza kutishiwa tena kama ilivyokuwa miaka ile ya
1980.
Ndiyo. Kisa cha
kujiuzulu kwa Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi katika nyadhifa za Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Muungano, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mwaka 1984,
kulitokana na hoja za Muungano, ambazo mwaka huu – miaka 30 baadaye –
tumeshuhudia zikiwalazimu wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaojiita UKAWA
wakisusia vikao hivyo kwa maelezo kwamba CCM ‘imepora rasimu’ kwa maslahi yake.
Binafsi naona
hoja za Jumbe zilikuwa sahihi kabisa kama ilivyokuwa kwa hoja ya Njelu Kasaka
na wafuasi wake wa G55, ingawa nao baadaye walibadilika kama kinyonga hasa
baada ya kupewa vyeo mbalimbali serikalini. Mpaka leo hii si mtoa hoja au mtu
yeyote wa kundi hilo
aliye tayari kuitaja tena hoja ya serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.
Lakini pamoja na
kujiuzulu kwa Jumbe, hoja zile bado ziko fikrani mwa Wazanzibari mpaka kesho,
kwani itakumbukwa wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 1990
uliomweka madarakani Dk. Salmin Amour Juma, Wazanzibari walikuwa wamepanga
kuitisha maandamano na kugomea uchaguzi huo kwa maelezo kwamba Zanzibar
inakandamizwa na Bara na wananchi wa visiwa hivyo hawapati baadhi ya haki zao
za msingi zilizomezwa ndani ya Muungano.
Ingawa tatizo
hili limekuwa likitajwa kwamba linatokana na historia ya visiwa hivyo; Unguja
na Pemba, lakini bado linagonganisha vichwa vya wengi, hata wale Wazanzibari wa
Unguja ‘wenye nafasi’. Unguja ndiko kwenye maendeleo zaidi kuliko Pemba , ambako ndiko karafuu inakozalishwa kwa wingi.
Wananchi wa Pemba ni maskini sana kiasi kwamba huwezi kuamini kama ni sehemu ya Tanzania ukiwalinganisha na wenzao
wa Unguja.
Waunguja
hawazungumzii kasoro za Muungano kwa kisingizio cha kulinda maslahi ya Chama
cha Mapinduzi kwa sababu wengi wao ni wafuasi wa CCM na kule Pemba asilimia 99
ni wafuasi wa chama pinzani cha CUF. Kwa hiyo wanadhani kwamba wakiupinga
Muungano na kasoro zake watawapa nguvu wapinzani, fikra ambazo kwa namna moja
ama nyingine ni potofu.
Zanzibar, tangu
uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, hakuko shwari kwa sababu Dk.
Salmin anaelezwa kwamba hakushinda kwa haki na CUF walikwenda mpaka kwenye
jumuiya za kimataifa kupiga kelele kwamba waliibiwa kura zao. Hata uchaguzi wa
mwaka 2000 na ule wa mwaka 2005, bado kilio cha CUF kimeendelea kuwa kile kile.
Katika uchaguzi
wa mwaka 1995, kwa mfano, uchaguzi ulirudiwa Zanzibar, na inasemekana kwamba
viongozi kadhaa wa CCM na wanasiasa wakongwe walikwenda usiku Unguja na kurejea
alfajiri Dar es Salaam katika kile kilichoelezwa na wachunguzi wa mambo ya
siasa kwamba ‘kuunusuru Muungano’.
Baadhi wanasema
kwamba ikiwa CUF itaruhusiwa na wananchi kutawala Visiwani, basi utakuwa ndio
mwisho wa Muungano, ambao Mwalimu alipiga kelele na kusema asingekubali kuona
Muungano unakufa wakati yeye akiwa hai.
Alikuwa sahihi
kabisa. Kwa sababu kitendo cha kushuhudia ‘mtoto wake mpendwa’ Azimio la Arusha
aliyezaa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea ‘anauawa’ rasmi mwaka 1991 kwa Azimio
la Zanzibar, hakika asingekuwa tayari kuona ‘mwanawe wa pekee’ ambaye ni
Muungano anakufa yeye akitazama.
Siri ya Muungano
huu wanaoijua ni Nyerere na Karume tu, wote wanaosema wanaijua wanajaribu
‘kukonyeza gizani’. Yaani wanakisia na si kile kitokacho moyoni.
Leo hii CCM
imeendelea kusimama kidete kuhakikisha kwamba ‘mwana pekee’ wa Mwalimu hakati
roho kama baadhi wanavyoombea.
Pengine inahofia
kwamba kukubali mapendekezo ya kamati ya mwafaka, ambayo ni kuwa na serikali ya
mseto, kutakuwa ni hatari kama kupika mchele uliichanganyika na chuya! Ni jambo
linaloonekana kuwa gumu kama kupanda mlima
Kilimanjaro ukikimbia.
CCM yenyewe
inajitetea kwamba hoja ya Muungano wa Tanzania inasimama juu ya msingi wa sera
ya chama hicho, ambayo inaelezwa kwamba ina ncha mbili; yaani kuulinda na
kuudumisha Muungano wenyewe kwa upande mmoja na muundo wa Muungano huo kuwa wa
Serikali mbili kwa upande wa pili.
CCM inaushabikia
Muungano na kupania kuulinda na kuudumisha kwa sababu kwanza inaamini kuwa
Muungano huo ni wa watu wenyewe na pili, uliasisiwa na vyama wazazi wake, yaani
TANU na ASP. Binafsi sijui kama Muungano ulikuwa wa watu wenyewe, kwa sababu hakuna
mtu aliyepata nafasi ya kuuridhia wakati huo kabla ya kufikia hatua ya kusaini
nyaraka za Muungano, ambazo mpaka leo hii hazipo na hazijulikani zilipo.
Ni kweli kwamba CCM
yenyewe ni matokeo ya Muungano huo na chachu ya kuziimarisha kwani tendo la
kuviunganisha vyama vya TANU na ASP kuunda CCM lilitokana na utashi wa
kukamilisha hatua za kuunda Muungano. Daima CCM inaunga mkono muundo wa
Muungano wa Serikali mbili kwa sababu kwanza ndio ulioamuliwa na waasisi wa
Muungano, Mwalimu Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Japokuwa CCM
inajinasibu kwamba muundo wa serikali mbili umeridhiwa na Watanzania wengi,
binafsi nasema siyo sahihi hata kidogo. Kwa kuchukua vigezo vya mwaka 1994
walivyofanya kukusanya maoni kwa wanachama, lazima mtu yeyote anaweza kuhisi
kwamba matokeo yaliyotangazwa yalikuwa ni kwa maslahi ya chama na wale
wanaoushabikia Muungano na si maslahi ya Watanzania walio wengi.
Lakini kama
kweli Muungano huu unapaswa kuwa na mtazamo halisi wa utashi wa wananchi wote,
kuna mambo mengi ya kufanya ili kufikia hatua hiyo ambayo haiwezi kuwa kero
tena; iwe Muungano unakuwepo au unavunjika.
Kwanza;
Watanzania wengi wangependa kuziona nyaraka za kwanza kabisa za Muungano ambazo
zilisainiwa bila kuwepo kwa ridhaa ya wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Pili; serikali
ya CCM inapaswa kutambua kwamba suala la Muungano siyo la chama peke yake, bali
ni la Katiba ya Nchi na wananchi kwa ujumla. Chama kinaweza kutawala kwa
kipindi fulani, na kama hoja za kuundwa kwake zinainufaisha zaidi CCM, lazima
itambue kwamba ipo siku hata yenyewe itakuwa pembeni kama ilivyotokea kwa ZAPU,
KANU na vinginevyo. Suluhisho pekee lilikuwa katika kuhakikisha kwamba mjadala
katika Bunge Maalum la Katiba unaendeshwa kwa haki na siyo ngonjera, mipasho na
matusi ambayo tumeyashuhudia kwa baadhi ya wajumbe. Wajumbe wengi, hasa kutoka
CCM, wamekuwa ‘mabingwa’ wa kutukana na kuwakashfu wale wote wanaounga mkono
mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya
Jaji Joseph Warioba.
Tatu; wananchi
wa pande zote wanapaswa kutoa maoni yao katika harakati za kuifanyia
marekebisho Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili watoe mapendekezo
yao na muundo bora wanaodhani unafaa kama serikali moja, mbili au tatu badala
ya kuegemea kwenye kura za kichama ambazo waliopiga ni wana CCM, waliohesabu ni
wanaCCM wenyewe na CCM ndio waliokuwa wakipinga serikali moja na tatu.
Nne; kero za
Muungano zinatakiwa kutatuliwa kiutendaji badala ya kisiasa kwa sababu hali
hiyo ndiyo inayosababisha migongano na mwishowe hata wapinzani wanaonekana kama
wakorofi wakati siyo sahihi.
Kwa kuyafanyia
kazi haya, ambayo ndani yake yamebeba hoja nyingi za msingi, kuna uwezekano wa
kuona mwelekezo sahihi wa Muungano huu ambao leo umetimiza miaka 50.
Tofauti na hapo,
CCM itakuwa haitendi haki kumlinda ‘mwana pekee’ wa Mwalimu Nyerere hata kama
habebeki. Itafikia mahali juhudi zao zitakuwa kama
kuitundikia dripu maiti, hatua ambayo itawafanya wachekwe na mataifa mengine.
MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI
AFRIKA!
0656 331974
No comments:
Post a Comment