Rais Jakaya Kikwete
akifurahi muundo wa jengo la tatu la abiria katika kiwanja cha ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana alipokwenda kuweka jiwe
la Msingi. Kushoto ni Mkurugenzi wa Mradi, Mohamed Millanga.
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ameagiza kuimarishwa
kwa udhibiti katika viwanja vya Ndege vya Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) na
Kilimanjaro (Kia), kutumiwa kupitisha dawa za kulevya kwenda nje na kuingia
nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi
wa jengo la tatu la abiria JNIA, Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema
hajaridhishwa na kasi ya udhibiti wa dawa za kulevya katika viwanja hivyo.
Alisema inashangaza dawa za kulevya zinapita katika viwanja
hivyo na watendaji wote wapo na zinakwenda kukamatiwa Afrika Kusini.
“Sijaridhishwa, unasikia kila siku mtu amekamatwa Afrika Kusini
na dawa za kulevya, sijui mwanamuziki gani, siridhishwi hata kidogo,” alisema.
Rais Kikwete alimtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
(TAA), Mhandisi Suleiman Suleiman kuhakikisha mianya hiyo inazibwa vinginevyo
ataanza kumwadabisha yeye kisha wengine watafuata... “Nitaanza na wewe
mkurugenzi na mwenyekiti wako wa bodi. Mtu anakuja hapa, sijui mwanamuziki
gani, mara yoo...yoo... kwa kuwa mnamfahamu anapita, hatuwezi kuwa namna hiyo.”
Aliagiza apewe orodha ya majina ya maofisa wanaodhaniwa
kujishughulisha na biashara hiyo naye atawaondoa kwa kuwa sheria inamruhusu...
“Rais hashtakiwi, nitawaondoa, nipeni majina kwa kuwa kinachotokea hivi sasa
kinaonyesha wote tunafanya biashara ya dawa za kulevya, wengine inatuumiza sana
tunaonekana wote ndicho tunachofanya.”
Alibainisha kuwa haingii akilini kusikia kuna kitu kinakwamisha
udhibiti wa dawa hizo katika viwanja hivyo ikiwamo Sheria ya Ununuzi wa Umma...
“Miaka miwili hiyo sheria gani kwa kitu cha Sh2.5 milioni... je, ingekuwa Sh600
milioni si ndiyo kungegeuzwa gulio?” alihoji.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alifafanua baadaye
kuwa Rais alikuwa anazungumzia kuchelewa kufungwa kwa mfumo wa kubaini dawa za
kulevya uwanjani hapo, kutokana na mchakato mrefu wa sheria hiyo.
Jengo la abiria
Rais Kikwete alisema atahakikisha Hazina inatoa fedha
zinazotakiwa kuharakisha ujenzi wa jengo hilo la abiria ambalo litakuwa na
maegesho ya ndege 18 kwa wakati mmoja, litakalohudumia abiria milioni sita kwa
mwaka badala ya milioni 2.5 wa sasa.
Mradi huo ambao unatekelezwa na Kampuni ya Ujenzi ya Kimataifa
ya BAM ya Uholanzi, utagharimu Sh518 bilioni na Serikali iliahidi kutoa
asilimia 50 ya fedha hizo sawa na Sh89 bilioni huku kiasi kingine kikitolewa na
Serikali ya Uholanzi.
Hata hivyo, hadi sasa fedha hizo hazijatolewa jambo ambalo
liliwahi kulalamikiwa na Mkurugenzi wa TAA kwamba linakwamisha ujenzi huo.
Jengo hilo
litakuwa na mifumo yote ya mawasiliano, usalama na uendeshaji na maegesho yenye
uwezo wa kuhudumia ndege za aina zote, zikiwamo Airbus 380.
Awali, Suleiman alisema uwanja huo utakamilika kwa wakati
kutegemeana na upatikanaji wa fedha na hivyo kuondoa msongamano wa abiria
katika uwanja wa sasa (Terminal II) ambao licha ya kuhudumia milioni 2.5, uwezo
wake ni kuhudumia abiria milioni 1.2 kwa mwaka.
Kabla ya Rais Kikwete kuzindua ujenzi huo, aliweka jiwe la
msingi katika ujenzi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi
Muhimbili katika eneo la Mloganzila nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza katika eneo hilo, Rais Kikwete aliagiza Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhakikisha inatayarisha haraka iwezekavyo ramani ya
ujenzi wa kituo hicho cha mafunzo kwa madaktari kinachotarajiwa kuwa kikubwa
zaidi kwa Afrika Mashariki na Kati.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment