Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Khamis Kigwangallah akizungumza
wakati wa majadiliano ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Twaweza uitwao
'Je,Watanzania wanafikiri nini hasa juu ya Katiba?' jijini Dar es Salaam jana.
Kulia ni Mkuu wa Twaweza Rakesh Rajani
Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Taasisi ya
Twaweza umebainisha kuwa wananchi wanaunga mkono kwa kiwango kikubwa Rasimu ya
Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji
Joseph Warioba.
Ripoti ya utafiti huo uliofanyika Februari, mwaka huu kwa njia
ya simu za mkononi na watu kuulizwa kuhusu mchakato wa Katiba, inaeleza kuwa
kama wananchi wangeipigia kura rasimu hiyo mwezi huo, Katiba hiyo ingepitishwa
kwa asilimia 65 Zanzibar na asilimia 62 Tanzania Bara.
Akiwasilisha ripoti hiyo jana, Mtafiti wa Twaweza, Elvis Mushi
alisema kati ya watu waliohojiwa upande wa Tanzania Bara, asilimia 20 wangepiga
kura ya hapana, kwa upande wa Zanzibar watu ambao wangesema hapana wangekuwa
asilimia 19.
“Watu ambao walisema hawana uhakika na hawajui lolote kwa upande
wa Zanzibar ni asilimia 19 na Tanzania Bara asilimia 15,” alisema.
“Zaidi ya asilimia 60 ya wapiga kura kutoka Tanzania Bara na
Zanzibar walisema wana nia ya kupiga kura ya kuikubali Katiba (rasimu) kama
ilivyo sasa.”
Muundo wa Serikali
Kuhusu muundo wa Serikali, Mushi alisema: “Asilimia 80 ya
Wazanzibari wanaunga mkono muundo wa serikali tatu. Kwa Tanzania Bara wanaounga
mkono serikali tatu ni asilimia 43.”
Alisema takwimu hizo ni tofauti na zilizotolewa miezi minane
iliyopita ilipotolewa Rasimu ya Kwanza ya Katiba, ambayo asilimia 51 ya
wananchi wa Tanzania Bara walipendekeza muundo wa serikali tatu.
Alisema baada ya kutolewa kwa Rasimu mbili za Katiba (ya kwanza
na ya pili), Wazanzibari wanataka uhuru zaidi wa kujitawala au muungano wa
serikali tatu, huku wananchi kutoka Tanzania Bara wakigawanyika nusu kwa nusu
juu ya muundo wa serikali wanaoutaka.
Mafuta na gesi
Kuhusu mafuta na gesi kutokuwa masuala ya muungano, bali chini
ya mamlaka ya Serikali za Tanganyika na Zanzibar, Mushi alisema suala hilo
lilikubaliwa na wananchi wa Tanzania Bara kwa asilimia 42 na Zanzibar asilimia
74.
Alisema Watanzania sita kati ya 10 (asilimia 60) wanaosikiliza
mjadala kuhusu Rasimu ya Katiba, wanawaamini wabunge kuwa wanawakilisha
masilahi yao bungeni, wanaunga mkono uwazi na uwajibikaji kama ilivyopendekezwa
katika Rasimu ya Katiba.
Mambo mengine ambayo yameungwa mkono na wananchi ni utaratibu wa
kudhibiti na kuwawajibisha wabunge, uwepo wa mgombea binafsi na mgawanyo wa
madaraka.
Utafiti huo umefanyika huku kukiwa na mvutano mkali katika Bunge
Maalumu la Katiba kuhusu muundo wa muungano na kusababisha wajumbe wa Bunge
hilo wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia kutokana
na CCM kuunga mkono muundo wa serikali mbili ambao ni tofauti na Rasimu ya
Katiba iliyopendekeza muundo wa serikali tatu.
Mushi alisema maoni ya wananchi ni muhimu yakazingatiwa bila
kujali nini kinaamuriwa na wawakilishi kwenye Bunge la Katiba, kwa sababu
baadaye watapiga kura ya maoni kupitisha Katiba.
Maoni ya kwanza ya utafiti huo yalikusanywa Tanzania Bara kati
ya Februari 12 na Machi 4, mwaka huu na taasisi hiyo ilipata majibu ya kaya
1,547 na mengine yalikusanywa kati ya Julai 16 na Julai 30 mwaka jana na kaya
1,708 zilitoa majibu.
“Kwa upande wa Zanzibar, utafiti kwa kutumia simu ya mkononi
ulifanyika Februari 24 na Machi Mosi, mwaka huu na kaya 445 zilitoa majibu,”
alisema
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment