Marehemu mzee Dennis Liwewe. |
Jamii ya Wanamichezo
hususan Soka nchini Zambia inaomboleza Kifo cha Mtangazaji Gwiji wa soka nchini
humo Mzee Dennis Liwewe ambaye aliwahi kuwa Mwandishi wa habari wa Michezo wa
BBC, idhaa ya Kiingereza katika Kipindi cha Focus on Africa.Erick David Nampesya
ameandaa makala kuhusiana na kifo cha Mtangazaji huyo Nguli.
Serikali
ya Zambia imetangaza siku tatu za Maombolezo kwa heshima ya Nguri huyo wa
Utangazaji ambaye alikuwa na utangazaji wenye hamasa kwa soka la Zambia ambao
ulisababisha asafiri zaidi ya mara 96 katika nchi arobaini na mbili duniani
akiwa na Timu ya taifa ya soka ya Zambia.
Liwewe
alishirikishwa na Kundi la Sakala Brothers nchini humo katika wimbo wa
kuipongeza Timu ya Taifa ya soka ya Zambia mwaka juzi baada ya kutwaa Ubingwa
wa Afrika nchini Gabon akiwahimiza kutobweteke na kuzidi kukaza msuli kwa
maendeleo ya soka la Zambia.
Mzee
Dennis Liwewe ambaye alifariki hapo juzi akiwa na umri wa miaka 78, alifanya
kazi ya Utangazaji soka kwa Zaidi ya miaka 50,kabla ya kustaafu mwaka 1993 kwa
ushauri wa madaktari kutokana na mshtuko wa moyo alioupata kufuatia ajali ya
ndege iliyouwa wachezaji wote wa timu ya taifa ya Zambia mwezi April 28,mwaka
1993,ambapo yeye alinusurika ajali hiyo baada ya kuchelewa ndege hiyo iliyokuwa
ikielekea nchini Senegal.
Utangazaji
wake wenye hamasa na uzalendo mkubwa ulimfanya atambulike na kuheshimiwa nchini
Zambia ambapo alichukuliwa mmoja wa watu wenye umaarufu mkubwa,ambapo alikuwa
na urafiki mkubwa na Viongozi wakuu nchini humo wakiwemo Marais wa zamani wa
nchi hiyo.
Katika
Wimbo huu Puteni Chimwela Mzee Dennis Liwewe anahimiza wadau wa soka nchini humo
kuunganisha nguvu kwa pamoja na kufanya juhudi ili kuleta maendeleo ya mchezo
huo unaopendwa na wengi duniani kote.
Dennis
Liwewe alihusisha maisha yake ya kila siku na mchezo wa soka ambapo katika moja
ya utani alivyojenga uhusiano na mkewe ambaye sasa ni mjane Bi Sylvia aliwahi
kuufananisha na hali 18 za mechi kali ya soka ambapo alisukuma mashambulizi
makali akitumia mtindo wa 5-3-2 ili kumshawishi Bi Sylvia,ambapo hata hivyo
ngoma ilikuja kugonga besela siku moja baada ya mkewe kususia mtoko aliokuwa ameandaa
yeye na marafiki zake,Lakini akaongeza kuwa alijipanga upya na ngoma kuanza
kuzunguka uwanjani na hatimaye Sylvia akawa ndani ya himaya yake kwa maisha ya
ndoa iliyoendelea kudumu hadi wiki hii Kipo kilipowatenganisha kutokana na
matatizo ya Ini
Na hivi
karibuni akiwa mgonjwa alimweleza mwandishi wa habari wa BBC aliyemtembelea
nyumbani kwake mjini Lusaka,akisema kuwa angenyayuka kitandani kwa mtindo wa
4-4-2,na kuongeza kuwa kama ingelazimu dakika za nyongeza kabla ya mikwaju ya
Penalt basi alikuwa tayari katika kuendelea kupigania uhai wake,lakini kwa
mapenzi ya Mungu Kipenga kilipulizwa hapo juzi jumanne kabla ya dakika za
nyongeza.
Kwa
Heri Mzee Dennis Liwewe
CHANZO, BBCSWAHILI
No comments:
Post a Comment