Wajumbe wa Bunge Maalum la katiba wakipinga jambo ndani ya bunge juzi wakati Kamati namba tatu na nne za kijadili vifungu vya rasimu ya Katiba walipokuwa wakiwasilisha ripoti zao Bungeni Dodoma juzi.
Dodoma. Bunge Maalumu la Katiba linaahirishwa
leo baada ya kukutana kwa siku 67 bila kupitisha hata ibara moja kati ya 240
zilizomo katika Rasimu ya Katiba.
Badala yake Bunge hilo likiongozwa na
Samuel Sitta “Mzee wa Kasi na Viwango” linaahirishwa hadi Agosti, mwaka huu
likiendelea kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita zenye jumla ya Ibara 19,
zinazohusu masuala yanayojenga msingi wa aina ya Muungano unaopendekezwa.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika
rasimu iliyowasilishwa bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wake, Jaji Joseph
Warioba ilipendekeza muundo wa shirikisho lenye serikali tatu, pendekezo ambalo
limeligawa Bunge hilo vipande viwili.
Kutokana na mgawanyiko huo, kauli zenye
utata, kejeli, matusi, dhihaka na ubaguzi ni mambo yaliyoshika hatamu katika
mjadala wa sura hizo mbili, huku viongozi wa Bunge; Sitta na Makamu wake, Samia
Suluhu Hassan wakilaumiwa kwa kushindwa kudhibiti hali hiyo.
Mwanzoni mwa wiki hii, Mjumbe wa Bunge
hilo, Ezekiah Oluoch alimshutumu Sitta kwamba ameshindwa kudhibiti nidhamu
katika Bunge na kwamba ndiye chanzo cha kuondoka kwa wajumbe wapatao 200 ambao
ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Mwenendo wa Bunge Maalumu ulikuwa na
dalili zote za kuonyesha kungetokea matatizo ndani yake kutokana na mipasho
ambayo ilikuwa ikitokea kwa wajumbe pamoja na lugha ambazo siyo za staha wakati
wa kutengeneza kanuni,” alisema Oluoch na kuongeza:
“Kwanza matumizi ya lugha zisizo na
staha, mwenyekiti anaruhusu wajumbe kuchangia hoja kwa kupeana mipasho bila
kujali hoja iliyopo mezani kinyume na kanuni,” alisema Olouch.
Hata hivyo, Suluhu alisema amekuwa
akiendesha Bunge hilo kwa umakini mkubwa na kwamba kila anaposikia lugha chafu
amekuwa akiwabana wajumbe kwa kuwaamuru kufuta kauli au kuomba radhi kwa
matamshi. “Sipendezwi na lugha chafu, kwa hiyo mojawapo ya mambo ambayo huwa
najitahidi kusikiliza kwa makini kila michango inapotolewa na wajumbe bungeni
ni kubaini kama wametumia lugha zisizostahili, kisha kuchukua hatua kwa mujibu
wa kanuni zetu,” alisema Suluhu.
Alikiri kwamba wapo baadhi ya wajumbe
ambao wamekuwa wakigoma au kukataa kuomba radhi na kwamba masuala yao hupelekwa
kwenye Kamati ya Maadili ambayo ina mamlaka ya kuchukua hatua zaidi kwa mujibu
wa kanuni za Bunge hilo.
Matakwa ya Kanuni
Sehemu ya Tano ya Kanuni za Bunge
Maalumu inatoa mwongozo wa mambo yanayokatazwa na yale yanayopaswa kufuatwa
wakati wa mjadala.
Kanuni ya 46 imeorodhesha mambo
yasiyoruhusiwa ambayo ni pamoja na kusema uongo, kutoa taarifa zisizokuwa za
kweli, kuzungumza jambo lolote ambalo halipo kwenye mjadala na kutumia majina
ya marais na waasisi wa Taifa kwa dhihaka.
Pia inazuia matumizi ya lugha ya kuudhi,
kubagua, kunyanyapaa au inayodhalilisha watu wengine, kuzomea, kupiga kelele za
aina yoyote zinazoweza kuvuruga mjadala au mwenendo bora wa shughuli za Bunge
hilo.
Licha ya makatazo hayo, wajumbe wamekuwa
wakikiuka kanuni bila kuchukuliwa hatua na hali hiyo imekuwa chanzo cha
mivutano, zomeazomea, kelele na mambo mengine hadi kundi la Ukawa kususia kikao
wakieleza kutokuridhishwa na mwenendo wa Bunge.
Kuufyata na kuufyatua
Baadhi ya kauli tata zilizojitokeza ni
pamoja na ile iliyotolewa na Asha Bakari Makame kwa mjumbe mwenzake, Ismail
Jussa kuwa anafanana na watu wenye mabusha nyuma ambao ndiyo huufyata.
Makame ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti
wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), alikwenda mbali zaidi na kumwambia Jussa
kuwa ana matatizo ya kiafya na si mwanamume kamili, kwani ameshindwa kuoa na
hana watoto wakati ana umri mkubwa.
“Huyu Jussa anasema kwamba tumeufyata,
hapa tuwekane sawa, maana ya kuufyata ni mtu kuwa na mabusha pale yanapokuwa
nyuma ndiyo kuufyata kwa hiyo yeye ndiyo ameufyata, ana busha huyu,” alisema
Bakari.
Naye Profesa Ibrahim Lipumba alichafua
hali ya hewa pale alipowafananisha wajumbe wa Bunge Maalumu na kundi la mauaji
nchini Rwanda, Intarahamwe.
“Tumechoka kusikiliza matusi. “Tumechoka
kudharau mawazo ya wananchi, tumechoka ubaguzi hatuwezi kuwa sehemu ya kundi la
Intarahamwe linalohamasisha ubaguzi ndani ya Tanzania hili hatulikubali.
Tunawaachia, watu wote tunaotaka Katiba ya wananchi tunawaachia Intarahamwe
mwendelee na Bunge lenu.”
Mjumbe mwingine ni Mwanakhamis Kassim
Said aliyesema: “Mimi nilikuwa namwomba baba yangu mdogo Seif (Maalim Seif
Sharif Hamad) awarejeshe watu wake humu (bungeni) kwa sababu mpira unachezwa
huku ndani. Hatutakii mema humu, tena ana choyo na husuda. Namwomba baba mdogo
atuache, alichokitaka amekipata, king’ora anazunguka saa 24 Dar es Salaam,
Unguja. Mheshimiwa Mwenyekiti Baba mdogo kila mara yuko kwenye pipa (ndege)
mara Uingereza, mara Canada mara wapi? Hicho ndicho anachokitaka amekipata.”
Mjumbe mwingine, Mohamed Seif Khatibu
alisema: “Nimejifunza kuwa baadhi ya wanasiasa wa upinzani ni vinyonga. Lakini
Maalim Seif ni kinyonga, wakipita kwenye mvua wanakuwa na rangi ya mvua, kwenye
jua wanakuwa na rangi ya jua, baharini wanakuwa na rangi ya bahari.”
Tuhuma za rushwa
Mjumbe Ezekiah Wenje alisema baadhi ya
mawaziri wamewahonga wajumbe wa kundi la 201 ili waunge mkono msimamo wao,
lakini alipotakiwa kufuta kauli hiyo alikataa na suala lake kufikishwa kwenye
kamati ya kanuni.
“Kuna wajumbe wengine walikwenda hadi
kwa waziri mkuu ambako walikula, walikunywa hadi saa 7:00 usiku, wengine
walikwenda kwa Gaudensia Kabaka (Waziri wa Kazi na Ajira) na walikula na kunywa
na kupewa bahasha.”
Kuingia msituni
Kapteni John Komba alitangaza kuingia
msituni iwapo Bunge Maalumu la Katiba litapitisha muundo wa serikali tatu, huku
akimshutumu Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na
timu yake ni waasi kama Adamu na Eva waliomuasi Mungu kutokana na kile
walichokifanya cha kupendekeza serikali tatu. Mwingine katika orodha ni Bernard
Membe aliyesema, Tume ya Mzee Warioba itakuja kukumbukwa kwa kuratibu mauaji ya
Muungano na Bunge nalo litakuja kulaaniwa kwa kubariki mauaji hayo.
Watoto wa shetani
Mjumbe Paul Makonda alisema: “Shetani
alikuja duniani kuiharibu dunia, kuiangamiza na kuteketeza kila kilichostahili
kuungana… watoto wake ni Mheshimiwa Jussa, watoto wake ni Mheshimiwa Mbowe,
watoto wake ni Mheshimiwa Lipumba… Hawa ni watoto wa shetani”.
Mwingine: Waride Bakari Jabu alisema:
“Chiku Abwao mimi namshangaa sana anayesema bora Muungano uvunjike lakini
Tanganyika iwepo. Tunafahamu asili yake mwenyewe ni Mkongo mumewe ndiye
Mtanganyika, namwambia Muungano huu utakuwepo na utaendelea kuwapo.”
Mjumbe Tundu Lissu alisema: “Tanganyika
haikuuawa na makubaliano ya Muungano, bali iliuawa kwa amri za Nyerere….
Mwalimu Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote ya kikatiba ya kutunga amri na kuua
Tanganyika.”
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment