“Pamoja na polisi kutaja sababu za kuzuia mikutano ya hadhara Arusha, tutawashauri , wafanye tathmini kuruhusu mikutano ya mbunge ili atimize wajibu wake wa kibunge
Arusha. Hatimaye Jeshi la Polisi wilayani Arusha
limeruhusu mikutano ya hadhara ya Mbunge wa Arusha (Chadema), Godbless Lema
baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo kuingilia kati.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas alithibitisha
jana kuruhusiwa kwa mikutano hiyo licha ya kuizuia awali baada ya kujiridhisha
na hali ya kiusalama.
Uamuzi wa polisi unakuja baada ya Lema kushikilia msimamo wa
kuendelea na mikutano akisema sababu zilizotolewa na polisi hazikuwa na
mashiko.
Polisi ilizuia mikutano ya Lema aliyetoa taarifa Aprili 17,
mwaka huu, baada ya CCM kuomba kufanya mikutano siku mbili baada ya taarifa
yake, ikitaja siku na maeneo hayohayo ya mbunge huyo.
Awali, Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) Arusha, Giles Muroto
aliyezuia mikutano hiyo, pia alitaja hofu ya mlipuko wa bomu kama sababu
nyingine ya kuzuia mikutano ya Lema.
Jana asubuhi, Mkuu wa Mkoa wa Arusha alikaririwa na kituo cha
Radio 5 cha Arusha akiliagiza jeshi la polisi kutathmini hali ya usalama na
kumruhusu Lema kutimiza wajibu wake wa kibunge kwa kukutana na wapiga kura wake
kupitia mikutano ya hadhara.
“Pamoja na polisi kutaja sababu za kuzuia mikutano ya hadhara
Arusha, tutawashauri , wafanye tathmini kuruhusu mikutano ya mbunge ili atimize
wajibu wake wa kibunge,” alikaririwa Mulongo.
Hata hivyo, Mulongo alikiri Jiji la Arusha kuwa katika hali tete
na hofu kutokana na tukio la mlipuko wa bomu kwenye Baa ya Arusha Night Park,
Aprili 13, mwaka huu.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment