Meneja Mkuu wa Tigo, Diego Gutierrez (kushoto) akipongezana na Mkurugenzi wa Ushirikiano na Ukuaji wa Kimataifa wa Facebook, Nicola D’Elian Dar es Salaam jana, mara baada ya kuzindua huduma ya Facebook bila malipo kwa lugha ya Kiswahili kupitia mtandao wa Tigo.
Dar es
Salaam. Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo
Tanzania imezindua mpango wa kutoa bure huduma za mtandao wa kijamii wa
Facebook kwa lugha ya Kiswahili.
Huduma hiyo inayotolewa kwa mara ya
kwanza, itawanufaisha wateja wake wote nchini na wale wa nchini nyingine za
Afrika Mashariki.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa
ushirikiano huo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Tigo, Diego Gutierrez
alisema ushirikiano huo utawawezesha wateja wanaotumia mtandao wa Tigo kuperuzi
kwenye Facebook kupitia simu zao za mkononi bila gharama zozote na kwa lugha ya
Kiswahili badala ya Kiingereza.
“Ni fursa ya pekee itakayowawezesha
watumiaji wetu wapatao milioni mbili kuungana na wenzao wanaotumia mtandao huo
wa kijamii ndani na nje ya nchi bila kikomo,” alisema Gutierrez na kuongeza:
“Hii ni mara ya kwanza kwa mtandao
wowote mkubwa wa kijamii kupatikana kwa lugha ya Kiswahili… lugha ambayo
inatumika kwa Watanzania na watu wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.”
Mkurugenzi huyo alisema mtandao wa
kijamii wa Facebook umekuwa chachu kubwa ya utumiaji wa data na kwa kulitambua
hilo, wameamua kuwaletea wateja wao ladha mpya ya kutumia mtandao huo kwa lugha
yao asilia ili kunufaika zaidi kulioko kutumia mtandao kwa lugha ya kigeni.
“Hii ndiyo maana halisi ya maisha ya
kidigitali (digiti)… huduma hii mpya itafungua milango mipya ya kielimu,
biashara na kiuchumi kwa watumiaji wa mtandao wetu duniani.”
Tanzania ni nchi ya pili kupata fursa ya
kuzinduliwa kwa huduma hiyo. Paraguay ilikuwa ya kwanza kupata huduma sawia na
hiyo ambayo ilizinduliwa Desemba mwaka jana na watuamiaji wa mtandao wa Tigo
walianza kutumia huduma hiyo kwa lugha yao ya Kiguarani.
Mkurugenzi wa Mtandao wa Facebook wa
Ushirikiano na Ukuaji wa Kimataifa, Nicola D’Elia alisema ushirikiano huo ni wa
kwanza nchini kwa kushirikiana na kampuni hiyo ya simu kuwapatia Watanzania
wengi uwezo wa kuwasiliana kwa lugha yao na kupata huduma za data bure.
CHANZO, MWANANCHI
No comments:
Post a Comment