UMOJA WA WAZANZIBAR WANAOISHI TANZANIA BARA (UWTB)
P.O. BOX 1019 DAR ES SALAAM TELL: 0718344443/0762812681
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TUNALAANI UKAWA KUSUSIA BUNGE
Ndugu
waandishi, sisi Wazanzibari tunaoishi Tanzania Bara tumestushwa,
tumehudhunishwa na tumekerwa mno na kitendo cha Wabunge wa vyama vya
upinzani vya NCCR, CUF na CHADEMA kutoka nje ya Bunge maalum la Katiba
linaloendelea mjini Dodoma na kususia vikao vya Bunge hilo.
Ikumbukwe
kuwa Bunge hili limeandaliwa kwa fedha nyingi za walipa kodi wa Taifa
hili kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa Tanzania inapata Katiba mpya
itakayoleta maendeleo kwa wananchi. Kwa mujibu wa sheria, kanuni na
taratibu zilizowekwa kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba, mahali
pekee pa kujadili na kupitisha hoja mbalimbali za kutunga Katiba hiyo ni
Bungeni.
Sasa inashangaza na kustaajabisha
kuona Wabunge hao wakiacha kutumia fursa hiyo ya kutumia Bunge kutoa
maoni yao, badala yake wanatoka na kuzurura Mitaani huku tayari wakiwa
wameshalipwa mamilioni ya fedha za wananchi. Je, kitendo hiki si usaliti
kwa wananchi? Tunalaani kitendo hiki kwa nguvu zote na kutaka wananchi
wote wa Bara na Visiwani kulaani kitendo hiki. Sisi tunaamini kuwa
Katiba mpya haiwezi kupatikana kwa maandamano na mikutano ya hadhara,
bali ni kwa kutumia Bunge Maalum linalogharamiwa na wananchi. Hivyo
tunawataka Wabunge hao warejee haraka Bungeni ili wasitucheleweshe
kupata Katiba mpya kwa ubinafsi wao.
Sababu
walizozitoa kwa ajili ya kususia vikao vya Bunge hilo eti wanatukanwa na
kubaguliwa, hazina mashiko. Kwa sababu kama ni matusi ndiyo ingekuwa
sababu za kususia vikao vya Bunge hilo, basi Wabunge wote wangesusia
pale Wabunge wa Upinzani walipowatusi na kuwakashfu Waasisi wa Taifa
letu Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Karume. Lakini hata baada ya
wao kuwatusi Waasisi hao, Bunge hilo liliwavumilia na kuendelea na wala
hakuna aliyesusa.
Kuhusu muundo wa Serikali,
sisi Wazanzibari tunaoishi na kufanyia shughuli zetu Tanzania Bara, bado
tunasisitiza kuwa muundo peke utakaodumisha umoja wetu, mshikamano wetu
na amani iliyopo, ni muundo wa Serikali mbili na si vinginevyo.
Tunapinga muundo wa Serikali tatu kwasababu utaongeza gharama kubwa za
uendeshaji na kusababisha mzigo mkubwa wa ulipaji kodi kwa wananchi.
Hivi
sasa tupo katika muundo wa Serikali mbili tu, lakini hali ya kiuchumi
kwa wananchi wa kawaida siyo ya kuridhisha. Je, tutakapoongeza idadi ya
Serikali hadi ziwe tatu hali ya maisha itakuwaje? Mbali ya suala la
gharama lakini pia tunaamini kuwa usalama wa muungano huu upo ndani ya
Serikali mbili. Kinyume chake, muungano huu utavunjika na kusambaratika.
Kitu ambacho hatupendi kitokee.
Mwisho:
Sisi
Wazanzibari tunaoishi Bara tutaendelea kuufurahia Muungano wetu na kuwa
pamoja na wale ambao wanautakia mema Muungano wetu. Tunawasihi na
kuwaomba Watanzania wenzetu kuwapuuza Viongozi wa UKAWA kwa jambo lolote
watakaloambiwa kwa nia ya kuwachukia Viongozi wetu wanaoongoza nchi hii
pamoja na bunge linaloendelea, ni wazi hawana nia njema na Taifa letu,
machafuko yatakapotokea wao ndio watakuwa wa kwanza kukimbia nchi hii na
matokeo yake wananchi wa kawaida ndio watakaopatwa na matatizo.
Tunamuomba
mwenyezi Mungu kuendelea kuulinda Muungano wetu pamoja na Viongozi wetu
wakiongozwa na Rais wetu Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Dr. Alli
Mohamed Shein
Mungu ibariki Tanzania
……………………………….
SWALEHE OMARY
MWENYEKITI
No comments:
Post a Comment