MJADALA wa Bunge Maalum la Katiba, hasa kuhusu muundo wa
Muungano bado unavuta hisia za wengi kutokana na yanayozungumzwa.
Tunapoadhimisha miaka 50 ya Muungano huo, mambo mengi yanazidi
kuelezwa, japo siyo mapya kwa vile yamekwishawahi kuelezwa katika Tume
mbalimbali huko nyuma kama ya Jaji Robert Kisanga, Jaji Francis Nyalali na Jaji
Joseph Warioba.
Mzee Warioba pia katika Tume ya Marekebisho ya Katiba
aliwasilisha maoni kama yale yale, na safari hii yakiwa yametolewa mapendekezo
lukuki ambayo kwayo ndiyo yaliyozaa mjadala mkubwa ndani ya Bunge Maalum.
Kubwa lililojitokeza ni kwa Wajumbe wengi wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) kutamka hadharani kwamba wao wanataka muundo wa Muungano wa
Serikali Mbili na siyo Tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Warioba.
Wengi wao wamekejeli hata takwimu zilizotumiwa na Tume hiyo
kwamba siyo sahihi na hazibebi mawazo ya Watanzania wote ambao kwa mujibu wa
Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 wamefikia milioni 44.
Kila anayesimama kupinga takwimu hizo, anasema ‘yeye
amezungumza na wananchi anaowawakilisha, ambao wanataka serikali mbili’. Kati
ya hao, hajaonekana hata mtu mmoja aliyethubutu, japo kwa bahati mbaya, naye
kutoa takwimu zake kwamba watu anaowazungumzia ni wangapi na alifanya ama
kukusanya wapi takwimu hizo na kwa utaratibu upi.
Badala yake kinachoonekana katika Bunge hilo Maalum ni hoja
za nguvu, ambazo kwa namna moja ama nyingine, ndizo zilizowafanya Wajumbe
wanaounda kundi la UKAWA wakaamua kususia vikao hivyo kwa maelezo kwamba CCM
‘imepora rasimu’ na inataka matakwa yake ndiyo yasikilizwe.
Wimbi kubwa la kuhusu muundo wa Muungano lilipotokea mwaka
1993 baada ya aliyekuwa Mbunge wa Chunya wakati huo, Njelu Kasaka, kutoa hoja
binafsi ya kutaka Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano, mambo mengi
yalisemwa.
CCM ilibaini kwamba nguvu za wabunge waliokuwa wanaunda
Kundi la G55 (baadaye likawa G65) zilikuwa kubwa ikatambua kwamba Muungano
ulikuwa mashakani.
Ndiyo maana mwaka 1994 CCM ikaendesha kura ya maoni kwa
wanachama wake – siyo Watanzania takriban milioni 30 wa wakati huo – ili kupata
msimamo wa muundo wa serikali.
Wakati huo wapo waliotaka iwepo Serikali ya Tanganyika ndani
ya Muungano, hivyo ziwepo serikali tatu. Wapo waliotaka ziendelee kubaki
serikali mbili, lakini pia walikuwepo waliotaka ibaki serikali moja tu. Hoja
zilikuwa nzito na zilihusisha maslahi ya Watanzania wote.
Waliokuwa
wakitetea Muungano ilionekana waliutetea kwa lugha kali ya hasira, ghadhabu na
hata vitisho vya kuwafukuza wenzao kwenye Chama. Waliodai Utanganyika nao
walidai kwa lugha hiyo hiyo ya ukali, wakijibu mapigo.
Wakati huo CCM ilikuwa na wanachama 3,506,355,
lakini walioulizwa kwenye Kura ya Maoni walikuwa 1,349,501 tu, sawa na
asilimia 33.49 ya wanachama wote nchi nzima.
Wanachana 833,317 ambao ni asilimia 61.75 ya wanachama
1,349,501 waliopiga kura walipendekea serikali mbili, wanachama 394,189 sawa na asilimia 29.21
walipendekeza serikali moja, na wanachama 111,604 ambao ni asilimia 8.27
walitaka serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano. Kura za maoni zilizoharibika
zilikuwa asilimia 0.67 ambazo ni za wanachama 9,042.
Tulielezwa baada ya kura hizo za maoni, ambazo hatujui
kulikuwa na uwazi kiasi gani, kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi
imekubaliana kwamba muundo wa Muungano uendelee ule ule wa serikali mbili,
lakini wakielekea kwenye serikali moja! Narudia - Serikali Moja!
Hakuna anayejua kama kura hizo zilikuwa sahihi au la, kwa
sababu walioitisha ni wanaCCM wenyewe, waliozisimamia ni viongozi wa CCM, waliohesabu ni hao hao, na
waliotangaza ni wenyewe!
Nakumbuka
aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara wakati huo, Joseph Butiku alikaririwa Jumanne,
Agosti 23, 1994 kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam wakati akishiriki
mjadala wa hoja ya serikali ya kufuta Azimio la Bunge la mwaka 1993 la kuanzishwa
kwa serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano na kusema Chama kilikuwa kimeamua
kuendelea na serikali mbili.
"...
Huu ndio msimamo wa Chama; serikali mbili kuelekea serikali moja na kama Waziri
Mkuu hataki, shauri yake, kama Rais wa Zanzibar hataki, shauri yake, maana
Chama cha Mapinduzi kina utaratibu wa kuliongoza taifa hili..."
alinukuliwa akisema.
Jambao ambalo CCM walilisahau, na ambalo wanaendelea
kutolitambua ni kwamba, suala hili ni nyeti na linawagusa wote, wananchi wa
Tanzania kwa ujumla wao, bila kujali itikadi zao za siasa.
Kusema kwamba wanaCCM Tanzania wanataka serikali mbili
halafu kuchukulia kama ndio uamuzi wa Watanzania wote ni makosa na kinyume na
demokrasia, kwa sababu kama mwaka 1994 wanachama wake hawakufika hata milioni
4, itakuwaje kwa sasa ambapo tayari kuna vyama vingi?
Kama wanapinga takwimu za Warioba ambazo zinawakilisha maoni
ya wengine yaliyochukuliwa katika utaratibu unaojulikana kisheria, kwa nini Watanzania waamini takwimu zao ambazo zimetolewa kwa
maslahi ya chama?
Sasa kilichotokea wakati ule mwaka 1994 ndicho
kinachoonekana katika Bunge Maalum la Katiba ambalo linatarajiwa kuahirishwa Ijumaa ya
tarehe 25 Aprili 2014 kupisha Bunge la Bajeti.
Kuna haja ya kutafakari. Sisi sote ni Watanzania na
tuipiganie nchi yetu kwa pamoja, tusitangulize mbele maslahi binafsi.
Huu ni mtazamo wangu, na kumbukumbu zangu, nijibuni kwa hoja.
Nawasilisha.
Ndugu yenu,
Daniel Mbega
Iringa, Tanzania
0656 331974
No comments:
Post a Comment