Wanasiasa wakuu waliokuwa wamezuiliwa.
Wanasiasa wanne wakuu
walioachiliwa na serikali ya Sudan Kusini, wamepokonywa hati zao za usafiri
walipokuwa wanajiandaa kuondoka nchini humo kusafiri hadi mjini Nairobi Kenya.
Mke wa marehemu John
Garanga, Rebecca Garang, ambaye anashikilia cheo cha juu katika chama cha SPLM
, ameambia mwandishi wa BBC Robert Kiptoo kuwa serikali haikutoa sababu ya
kuwapokonya hati za usafiri wanasiasa hao.
Serikali ya Sudan
Kusini iliwaachilia wanasiasa hao waliokamatwa kwa madai ya kuhusika na njama
ya mapinduzi dhidi ya serikali ya Rais Salva Kiir Disemba mwaka jana.
Waziri wa sheria
alisema kuwa serikali ilifutilia mbali kesi dhidi ya wanasiasa hao wanne wakuu
waliotuhumiwa kupanga njama ya mapinduzi ambayo yamesababisha vurugu za wenyewe
kwa wenyewe nchini humo.
Wanne hao akiwemo
aliyekuwa kiongozi wa chama cha SPLM, walikanusha madai ya kuhusika na njama ya
mapinduzi, na pia wamekanusha uhusiano wowote na mapigano yanayoendelea nchini
Sudan Kusini.
Kuachiliwa kwao
imekuwa moja ya matakwa makubwa ya waasi wanaopambana na serikali na ambao
wanadaiwa kuwaua mamia ya watu katika mji wa Bentiu kwa misingi ya ukabila.
Takriban watu milioni
moja wamelazimika kutoroka makwao tangu vita kuzuka Disemba mwaka jana.
Waziri wa sheria
Paulino Wanawilla alisema kesi hiyo imetupiliwa mbali kwa sababu ya kusaidia
juhudi za amani na mapatano katika nchi hiyo ambayo imetumbukia katika vita vya
wenyewe kwa wenyewe.
Wanne hao ni pamoja na
aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha (SPLM) Pagan Amum, aliyekuwa waziri wa
usalama Oyai Deng Ajak, aliyekuwa waziri wa ulinzi Majak D'Agoot na aliyekuwa
balozi wa nchi hiyo nchini Marekani Ezekiel Lol Gatkuoth.
CHANZO, BBCSWAHILI
No comments:
Post a Comment