Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (Kulia wanaoshuka ngazi), akizungumza jambo na Mbunge wa Kasulu Mjini, Mhe. Daniel Nsanzugwanko, baada ya kumalizika kwa mjadala wa mchana kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2017/2018, Bungeni Mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (MB), (kushoto), akijibu hoja mbalimbali za Waheshimiwa wabunge kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2017/2018, Bungeni Mjini Dodoma.
Baadhi ya Wabunge wakiwapongeza Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (Kulia) na Naibu Waziri wake Mhe. Dkt Ashatu Kijaji (Mb) (Katikati), baada ya kujibu hoja mbalimbali za Waheshimiwa wabunge kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2017/2018 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2017/2018, Bungeni Mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), akimpongeza Naibu Waziri wake, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, baada ya kuwasilisha kwa umahili mkubwa majibu ya serikali kutokana na hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge wakati wa kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2017/2018 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2017/2018, Bungeni Mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango, Mhe. Dkt Ashatu Kijaji (Mb), akizungumza na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri (kulia) pamoja na maafisa wengine waandamizi wa Tume hiyo baada ya kuwasilishwa kwa majibu ya hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2017/2018 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2017/2018, Bungeni Mjini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bibi Dorothy Mwanyika, akifurahia jambo na Kamishna wa Bajeti wa Wizara hiyo, Bw. John Cheyo, baada ya kujibiwa kwa hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2017/2018, Bungeni Mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (MB), (kushoto), akipongezwa na Mbunge wa Liwale, George Huruma Mkuchika, baada ya Waziri huyo kujibu hoja mbalimbali za Waheshimiwa wabunge kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2017/2018, Bungeni Mjini Dodoma.
Baadhi ya Maafisa waandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Tume ya Mipango, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (MB), na Naibu waziri wake Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) kujibu hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2017/2018, Bungeni Mjini Dodoma.
Kamisha wa Bajeti kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. John Cheyo (kulia), akibadilishana mawazo na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Joyce Ndalichako (katikati) na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba, nje ya ukumbi wa Bunge baada ya Serikali kupitia Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb) na Naibu Waziri wake Mhe. Dkt Ashatu Kijaji (Mb), kujibu hoja mbalimbali za Waheshimiwa wabunge kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2017/2018, Bungeni Mjini Dodoma.
(Picha zote na Benny Mwaipaja-Wizara ya Fedha na Mipango)
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
UFAFANUZI WA HOJA ZA WAHESHIMIWA WABUNGE WAKICHANGIA HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHE. DKT.
PHILIP I. MPANGO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO
WA TAIFA
KWA MWAKA 2017/18 NA MWONGOZO
WA KUANDAA
MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI
KWA
MWAKA 2017/18
DODOMA
NOVEMBA,
2016
A.
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii
kukushukuru wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha
majadiliano kwa ufanisi kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na
Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2017/18.
2.
Mheshimiwa Spika, napenda kutambua mchango mzuri
uliotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, chini ya Mwenyekiti wake
Mhe. Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini na Makamu Mwenyekiti,
Mhe. Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo. Ninatambua pia mchango wa
waziri kivuli na msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu wizara ya
Fedha na Mipango, Mhe. Halima James Mdee, Mbunge wa Kawe. Aidha, ninawashukuru
kwa dhati Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia mjadala huu kwa kuzungumza (45) na kwa maandishi (30).
3.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla mjadala ulikuwa
mzuri, baadhi ya maoni yakitolewa kwa hisia kali. Mimi naamini kwamba kwa
kuzingatia umuhimu wa uchumi katika nchi ni jambo jema tukachambua, tukabishana
na hatimaye turidhiane juu ya vipaumbele, mikakati na hatua stahiki za kukuz
auchumi kwa namna endelevu zitakazowezesha kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025.
4.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia kuwa
tumepokea michango na hoja nyingi sana kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge, naomba
niahidi hapa kuwa nitawasilisha Bungeni taarifa ya maandishi inayofafanua hoja zote
zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge.
B.
MAONI NA USHAURI
ULIOSISITIZWA NA WAHESHIMIWA WABUNGE WENGI
5.
Mheshimiwa Spika, yapo maoni/ushauri
mbalimbali uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge ambayo Serikali itazingatia katika
kuandaa Mpango wa Maendeleo na Bajeti
kwa Mwaka 2017/18. Ushauri huo ni:-
(i)
Serikali ijielekeze kubuni vyanzo vingine vya
mapato (Non-tax revenue) vitakavyosaidia kugharamia Bajeti ya Serikali;
(ii)
Serikali ipunguze kukopa zaidi kutoka vyanzo vya
ndani;
(iii)
Kukamilisha haraka zoezi la Sovereign Rating ili kuwezesha kukopa kutoka vyanzo vya nje;
(iv)
Ujenzi wa Reli ya Kati kutoka Dar – Tabora -
Kigoma (km 1,251) kwa Standard Gauge
na matawi yake;
(v)
TRA iandae mapema awamu ya pili ya ukusanyaji wa
kodi ya majengo katika halmashuri na miji midogo iliyosalia;
(vi)
Kutenga fedha za kutosha za matumizi mengineyo
(OC) kwa mafungu husika ili kuweza kugharamia mpango wa Serikali kuhamia Makao
Makuu – Dodoma hususan kwa upande wa malipo ya stahili za watumishi
watakaohamishwa;
(vii)
Kukamilisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ya
Serikali kwa njia za kielektroniki;
(viii)
Kuhamasisha na kuongeza matumizi ya mashine za EFD
na wananchi kwa ujumla kudai risiti
halali pale wanaponunua bidhaa;
(ix)
Kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato hususan bandari
bubu na biashara za magendo;
(x)
Kuboresha mazingira ya kufanya biashara na
uwekezaji ili kuiwezesha sekta binafsi kutoa mchango unaostahili katika kukuza
uchumi wa nchi yetu;
(xi)
Kuweka mkakati wa kujenga zahanati katika kila
kijiji na kituo cha afya kwa kila kata na kuimarisha upatikanaji wa madawa na
vifaa tiba,
(xii)
Kukamilisha utaratibu wa matumizi ya shilingi
milioni 50 kwa kila kijiji/mtaa/shehia na kuongeza kiasi kinachotengwa;
(xiii)
Kuendeleza maeneo ya viwanda vidogo, na EPZ/SEZ;
(xiv)
Kutoa kipaumbele kwa miradi ya makaa ya mawe -
Mchuchuma na chuma Liganga;
(xv)
Kuboresha elimu ya juu na kuongeza wigo wa utoaji
wa mikopo kwa wanafunzi; na
(xvi)
Kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara.
C.
UFAFANUZI WA HOJA MBALIMBALI
Hoja Na. 1: Uchumi una hali mbaya
(Umedorora) na kuna manung’uniko mengi ya wananchi mtaani.
Hali ya Uchumi (Januari – Juni 2016)
·
Ukuaji wa Pato la Taifa: 6.7% (Jan-Jun 2016) Vs 5.8%
(Jan-Jun 2015).
·
Sekta zilizokua zaidi: uchukuzi, uhifadhi wa mizigo
(17.4%), uchimbaji wa madini na gesi (13.7%), mawasiliano (13.0%) na sekta ya
fedha & bima (13.0%).
·
mfumuko wa bei: 6.5% (Jan 2016), 5.5% (Jun
2016) na 4.5% (Sept 2016).
·
Akiba ya fedha za kigeni: 4 months of imports cover
(USD 4.1 bn) Sept 2016
·
Urari wa Biashara ya Nje: current account deficit USD
601.8 (Jan – Sept 2016) Vs USD 1,207.7
(Jan – Sept 2015)
Mwenendo wa sekta ya kibenki (Januari – Septemba 2016).
·
Sekta imeendelea kukua na ina mitaji na ukwasi wa
kutosha.
a)
Mitaji ikilinganishwa na mali iliyowekezwa (Total
Capital to Total Risk Weighted Assets and Off-balance Sheet Exposures) ni 19.08%
Vs kiwango cha chini kinachotakiwa 12.0%.
b)
Mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslimu
ikilinganishwa na kiwango cha amana zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi
(liquid assets to demand liabilities) 34.18% Vs
kiwango cha chini kinachohitajika 20%.
But: mikopo chechefu imeongezeka
(6.7% Sept 2015, 9.1% Sept 2016)
Mabenki yaliyopata Hasara Jul – Sept 2016: CRDB & TIB Development Bank.
Sababu: mikopo chechefu
(provision for loan losses);
Twiga Bancorp imewekwa chini
ya uangalizi wa BOT;
NB: Crane Bank Ltd ya Uganda
imewekwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu Oct 2016; Imperial Bank Kenya, Oct
2015
Benki nyingi incl. CRDB na
TIB Devt, zimekuwa na mitaji na ukwasi wa kutosha. Matarajio ni kuwa benki hizi
zitafanya vizuri katika kipindi kilchobaki cha 2016/17.
Kwa mwaka ulioshia Sept 2016 Sekta ya Kibenki kwa
ujumla ilipata faida: pato kwa rasilimali (Return on Assets) 2.53%; pato
kwa mtaji (Return on Equity) 12.05%. Mtaji
na kiwango cha mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslimu Vs amana
zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi (liquid
assets to demand liabilities) viliendelea kuwa juu ya viwango
vinavyotakiwa.
Riba za mikpo zimepungua: 16.18% Sept 2015 –
15.83% Sept 2016
Riba za amana zilibakia wastani wa 9.0%;
Tofauti
kati ya riba za mikopo na amana za mwaka mmoja ilipungua 1.77% pts (Sept 2016)
kutoka 3.32 % pts (Sept 2015);
Mwenendo
huu umeimarisha mazingira ya kufanya biashara na ushindani.
Viwango vya Ubadilishaji fedha
Hatua za kuimarisha thamani
ya Shilingi:
(i)
kuongeza mauzo ya bidhaa nje;
(ii)
kuimarisha uzalishaji wa nishati; na
(iii)
kupunguza matumizi ya fedha za kigeni yasiyo na
tija.
Wastani wa Shs. 2,172.38: USD
1 (Jan 2016), Shs. 2,180.54 (Jul 2016); Shs. 2,188.1: USD 1 (Sept 2016)
MWENENDO WA BAJETI YA SERIKALI
Ulipaji wa Madeni ya Ndani
6.
Mheshmiwa Spika, Katika kipindi cha Julai hadi
Oktoba 2016 Serikali imelipa madeni mbalimbali yaliyohakikiwa na Mkaguzi wa
Ndani Mkuu wa Serikali yenye jumla ya shilingi bilioni 187.521. Madeni haya
yanajumuisha madeni ya wakandarasi wa barabara, maji, umeme pamoja na wazabuni
mbalimbali. Aidha, madeni ya watumishi wa umma yanaendelea kulipwa kupitia
mafungu yao.
Ulipaji wa Deni la Nje
7.
Mheshimiwa Spika, Katika kipindi kuanzia
Novemba 2015 hadi kufikia Oktoba, 2016 Serikali imetumia jumla ya shilingi
bilioni 1,196.9 kwa ajili ya kulipia madeni ya nje. Kati ya kiasi hicho, malipo
ya mtaji ni shilingi bilioni 709.7 na malipo ya riba ni shilingi bilioni 487.2.
Malipo ya deni la Taifa yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na
mikopo mipya, kumalizika kwa kipindi cha kabla ya kuanza kulipa mtaji (Grace Period) kwa mikopo ya muda mrefu
pamoja na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Kimarekani.
8.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kulipa
kwa wakati mikopo yote ya nje inayoiva kwa mujibu wa mikataba. Kwa kuwa
kutofanya hivyo kutahatarisha mahusiano yaliyopo kati yetu na nchi wahisani,
taasisi za fedha za kimataifa na mabenki ya nje. Aidha, nchi isipolipa kwa
wakati inaweza kushitakiwa kwenye mahakama za kimataifa na kuisababishia nchi
hasara na kupelekea kutopata mikopo tena kutoka nje. Kadhalika, kutokulipa kwa
wakati kutasababisha Serikali kulipa gharama za ziada (penalty) kulingana na
makubaliano na hivyo kuongeza mzigo kwa taifa.
9.
Mheshmiwa Spika, Serikali imejiwekea mikakati
mbalimbali ili kuhakikisha kwamba Deni la Taifa linadhibitiwa na linaendelea
kuwa himilivu na linalipwa kwa wakati.
Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo
10.
Mheshmiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2016/17
jumla ya shilingi bilioni 25.0 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo
ambapo hadi kufikia mwezi Oktoba 2016 jumla ya shilingi bilioni 10.0
zimetolewa.
Ununuzi wa Chakula cha Hifadhi ya Taifa
11.
Mheshmiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2016/17
jumla ya shilingi bilioni 15.0 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa chakula cha
hifadhi ya Taifa ambapo hadi kufikia mwezi Oktoba 2016 jumla ya shilingi
bilioni 9.0 zimetolewa.
Utoaji wa Fedha za Mfuko wa Jimbo
12.
Mheshmiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2016/17
Serikali imetenga shilingi bilioni 10.4 kwa ajili ya Mfuko wa Kuchochea
Maendeleo Jimboni. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 9.0 ni kwa ajili ya
Tanzania Bara na shilingi bilioni 1.4 ni kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Serikali inatarajia kutoa fedha hizo mwezi Novemba 2016.
13.
Mheshmiwa Spika, katika nusu ya kwanza ya
mwaka 2016, kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa imeongezeka na kufikia asilimia 6.7
ikilinganishwa na asilimia 5.8 kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2015.
14.
Mheshimiwa Spika, manung’uniko mtaani yapo na
kwa kiasi kikubwa yametokana na jitihada na hatua zilizochukuliwa na Serikali
kurudisha nchi kwenye utaratibu wa nidhamu ya kazi katika Utumishi wa Umma,
kurejesha nidhamu ya matumizi/kuondoa matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima,
kupambana na wizi/ubadhirifu wa fedha na mali za umma, kuhimiza ulipaji kodi na
ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi n.k. Hata hivyo, Serikali inaamini kuwa
hatua hizi ni kwa maslahi mapana ya Taifa na maumivu ni ya kipindi cha mpito
cha kuweka mambo sawa/kurejesha mifumo kwenye utaratibu unaokubalika na
endelevu. “There is no game without pain”.
15.
Mheshimiwa Spika, upo utaratibu wa Serikali, Taasisi
binafsi na Mashirika ya Kimataifa kufanya tathmini ya uchumi wa nchi na kutoa
maoni yao juu ya kile walichokiona. Shirika la Fedha la Kiamtaifa – IMF ambalo
lilikuwa hapa wiki moja iliyopita, limekamilisha tathmini ya mwenendo wa uchumi
wa nchi yetu ambapo kiujumla wameridhika na hali ya uchumi wa Tanzania.
Hoja Na. 2: Misingi ya Mpango (premises)
iliyowekwa inatujengea kushindwa.
16.
Mheshimiwa Spika, neno ‘Misingi’ katika Mapendekezo ya Mpango lililenga
kumaanisha “assumptions”. Hakika
Serikali inajua kwamba hali halisi ya mazingia wezeshi kwa uwekezaji nchini na
nafasi ya Tanzania kama ilivyotathminiwa na Benki ya Dunia katika Doing
Business report. Serikali inajua utabiri
wa hali ya hewa na maoteo ya upungufu wa chakula n.k. We are not naïve. Assumptions si lazima ziwe halisi bali
ziliwekwa hapa kurahisisha uwekaji wa malengo kwa mwaka 2017/18. Utaratibu huu ni wa kawaida kabisa kwa
wachumi. Mathalani tunapotaka kuchambua
biashara baina ya mataifa tunaweka assumption kwamba dunia ina nchi 2 tu
zinafanya biashara ili kurahisisha uchambuzi japo kila mtu anafahamu dunia ina
nchi nyingi zinafanya biashara baina yao.
Hoja na 3: Fedha kutopelekwa kwenye Halmashauri kwa wakati
17.
Mheshmiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/17
Mamlaka za Serikali za Mitaa ziliidhinishiwa bajeti ya shilingi bilioni
5,434.7. Kati ya kiasi hicho shilingi bilioni 3,593.9 ni kwa ajili ya
mishahara, shilingi bilioni 598.2 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC)
ikijumuisha shilingi bilioni 266.2 za mapato yatokanayo na vyanzo vya ndani vya
Halmashauri na shilingi bilioni 332.0 ni
ruzuku kutoka Serikali Kuu. Aidha, shilingi bilioni 1,242.6 ni kwa ajili ya
miradi ya maendeleo ambapo shilingi bilioni 588.5 ni fedha za nje na shilingi
bilioni 654.1 ni fedha za ndani ikijumuisha shilingi bilioni 399.2 zinazotokana
na mapato ya ndani ya Halmashauri na shilingi bilioni 254.9 ni ruzuku kutoka
Serikali Kuu.
18.
Mheshmiwa Spika, katika kipindi cha Julai hadi
Oktoba 2016, fedha zilizotolewa zinajumuisha mishahara shilingi bilioni 1,181.0
sawa na asilimia 33, matumizi mengineyo shilingi bilioni 192.8 sawa na asilimia
32.2 na fedha za maendeleo shilingi bilioni 177.3 sawa na asilimia 14.3. Aidha,
mbali na fedha za ruzuku kutoka Serikali Kuu na makusanyo ya ndani ya
Halmashauri kiasi cha shilingi bilioni 271 zilitumika kutekeleza miradi ya maji
vijijini (shilingi bilioni 51.1), umeme vijijini (shilingi bilioni 132.4),
Mfuko wa barabara (shilingi bilioni 78.1) na utoaji wa pembejeo kwa wakulima
(shilingi bilioni 10.0) katika Halmashauri mbalimbali nchini.
Hoja Na. 4: Mradi
wa Mchuchuma na Liganga uko kwenye Mpango wa maendeleo kila mwaka lakini
utekelezaji wake haujaanza
19.
Mheshimiwa Spika, Sio kweli kuwa utekelezaji wa Mradi wa Makaa
ya Mawe, Mchuchuma na Chuma Liganga haujaanza. Utekelezaji wa mradi huu utakaogharimu
Dola za Marekani bilioni 3 umeanza na kufikia hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja
na:
·
Kukamilika kwa upembuzi yakinifu wa mradi ikiwa ni pamoja na kutambua kiasi cha
mashapo ya makaa ya mawe na chuma, usanifu wa migodi na kiwanda cha chuma na
kituo cha kuzalisha umeme;
·
kupatikana kwa leseni za uchimbaji na matumizi ya madini, leseni ya matumizi ya maji
na leseni ya uzingativu wa mazingira;
·
Kukamilika pia kwa mkakati wa ushirikishi wa wananchi wanaouzunguka mradi na njia ya kusafirishia umeme;
·
Kukamilika kwa ujenzi barabara kwa kiwango cha changarawe ili kuruhusu usafirishaji
wa mitambo kwenda kwenye eneo la mradi;
·
kuendelea na
usanifu wa ujenzi wa reli ya liganga hadi Mtwara na uwezekano wa kuiunganisha
na reli ya TAZARA na kuendelea na usanifu katika bandari ya Mtwara; na
·
kukamilika kwa tathmini ya fidia kwa wananchi watakaopisha eneo la mradi imekamilika.
Hoja Na. 5:
Utaratibu wa Taasisi za Umma kuweka fedha zao katika Mabenki ya kibiashara
urejeshwe ili kuwezesha mabenki kukopesha fedha hizo kwa wafanyabishara na pia
kuziwezesha Taasisi hizo kunufaika na riba zitokanazo na amana.
20.
Mheshimiwa Spika, uamuzi wa Serikali kuzitaka
taasisi za umma kufungua akaunti ya mapato Benki Kuu utaendelea kubaki kama
ulivyo. Utaratibu uliokuwa umejengeka ulizinufaisha benki chache na haukuwa na
maslahi mapana kwa Taifa. Benki hizo zimekuwa zikipata faida kwa kutumia migongo ya maskini na hivyo sasa
basi! Benki zifanye kazi kwa kurejesha ushindani.
Mfano:
Taasisi moja ilikuwa na amana za
muda maalum (fixed deposit) za shilingi bilioni 440 ambazo ziliwekwa katika
baadhi ya benki. Kiasi hiki kilizaa faida ya shilingi bilioni 17 ambayo
inamaanisha riba ya wastani wa asilimia 4 kwa mwaka. Ijapokuwa ukweli ni
kwamba, amana za chini ya shilingi milioni 100 zinakuwa na riba ya kati ya
asilimia 8 na 10 na kiasi cha amana kinapokuwa kikubwa zaidi riba inaongezeka
hadi kufikia asilimia 15. Kama riba ingekuwa asilimia 13, taasisi hiyo ingepata
faida ya bilioni 57.2 kabla ya kodi. Hivyo, kwa taasisi hiyo moja tu,
watanzania wamekuwa wakiibiwa shilingi bilioni 40 kila mwaka.
Si hivyo tu, fedha hizo (bilioni
440) zilizokuwa katika benki za biashara zilitumika kuikopesha Serikali kupitia
hati fungani kwa riba ya asilimia 15, hivyo wananchi hulipa benki hizi riba ya
hadi shilingi bilioni 66 kwa fedha ambazo ni za kwao wenyewe. Maana yake ni
kuwa, wananchi waliendelea kulipa riba kwa fedha zao wenyewe sawa na hasara ya
shilingi bilioni 106 kwa mwaka. Hatuwezi kuendelea na utaratibu huu.
Benki na baadhi ya watanzania
waliozoea kupiga dili sasa basi! Benki
ambazo zimekuwa zikipata faida kwa
kutumia migongo ya maskini sasa basi! Benki zifanye kazi kurejesha ushindani.
Mheshimiwa Rais alisema hadharani na ukweli utabaki hivyo, kwamba hizo fedha hazitarudi.
Hoja Na. 6:
Serikali ielekeze benki kushusha riba kutoka asilimia 18 hdi 13 kwa
wafanyabiashara wadogo na wakubwa ili kuongeza mzunguko wa fedha katika uchumi.
(Riba za mikopo bado ziko juu, Serikali ielekeze benki kushusha riba hizo)
21.
Mheshimiwa Spika, Ni kweli riba za mikopo ni
kubwa hasa zile zinazotozwa na Taasisi ndogondogo za fedha (microfinance).
Katika Sekta ya Huduma Ndogo Ndogo za Fedha (Microfinance) kuna benki, taasisi
na asasi za fedha zilizo rasmi na zisizo rasmi ambazo zinatoa huduma za kifedha
kwa wateja wadogo wadogo. Pia kuna taasisi na asasi za kifedha ambazo zinatoa
huduma za mikopo kwa kutumia mitaji binafsi bila kukusanya na kupokea amana za
wateja.
22.
Mheshimiwa Spika, Taasisi na asasi hizo
zimeongezeka kwa kiasi kikubwa na zimekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya ujasiriamali
na ukuaji wa uchumi wa wananchi na mikopo ya taasisi hizo kwa kiasi kikubwa
inategemewa na watanzania walio wengi.
23.
Mheshimiwa Spika, Taasisi na asasi hizo
zinapata leseni kutoka katika mamlaka tofauti ikiwemo BRELA, Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
RITA, na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Utaratibu huo umesababisha
usimamizi na ufuatiliaji wa taasisi hizo kuwa mgumu. Kutokana na hali hii
zimejitokeza changamoto nyingi na mapungufu kadhaa katika sekta ya
“Microfinance”, ikiwa ni pamoja na kutozwa riba kubwa na kuwa na mikataba yenye
mapungufu mengi. Hii inatokana na wakopeshaji kwenye sekta hii kutokuwa na
usimamizi imara na elimu ndogo ya maswala ya fedha kwa wateja walio wengi
(financial illiteracy).
24.
Mheshimiwa Spika, Serikali inakiri kuwepo na
malalamiko kwa wananchi wengi nchini kuhusiana na uendeshaji wa biashara
inayofanywa na asasi hizo kama vile viwango vya juu vya riba na ada pamoja na
utaratibu mbaya wa ukusanyaji wa marejesho (loan repayment). Hali hii inatokana
na ukweli kwamba hakuna mamlaka rasmi na halali ya kisheria yenye wajibu wa
kutoa leseni, kuratibu, kusimamia na kuhakikisha ulinzi wa wateja (consumer
protection) katika taasisi hizi za fedha.
25.
Mheshimiwa Spika, Katika kutatua mapungufu na
changamoto hizi na kwa kuzingatia maendeleo yaliyojitokeza katika huduma za
fedha kwa wateja wadogo wadogo, Serikali imekamilisha na kuidhinisha Sera ya
Taifa ya ‘Microfinance’ na hatua za ukamilishaji wa sheria ya Microfinance
zinaendelea.
26.
Mheshimiwa Spika, Sheria hiyo itaunda mfumo
mahususi wa kusimamia na kuratibu shughuli za taasisi na asasi za fedha zilizo
na zisizo rasmi ambazo zinatoa huduma za kifedha kwa wateja wadogo wadogo
ambazo haziko chini ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
27.
Mheshimiwa Spika, Kwa upande mwingine, benki
na taasisi za fedha zinazosimamiwa kisheria na Benki Kuu ya Tanzania,
zimeendelea kuwa na viwango bora vya riba katika kipindi cha mwaka ulioishia
mwezi Septemba 2016.
28.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuweka riba elekezi, uzoefu wa nchi nyingi unaonesha kwamba viwango
vya riba huamuliwa na nguvu ya soko. Ni dhamira ya Serikali kuona riba za benki
zinazotozwa katika mikopo zinapungu. Hivyo, Serikali itaendelea kuweka
mazingira mazuri yatakayosaidia kuleta ushindani utakaopelekea viwango vya riba
hizo kuwa nafuu zaidi. Aidha, ikumbukwe kwamba kuna madhara ya kuweka viwango
elekezi vya riba ikiwa ni pamoja na uwezekano wa benki kupunguza mikopo kwa
sekta binafsi ikiwa kiwango hicho elekezi kitakuwa chini zaidi ya riba ya
dhamana na hati fungani za serikali; kuongezeka kwa mikopo chechefu na kupungua
kwa ushindani katika sekta ya benki na ufanisi katika utekelezaji wa sera ya
fedha.
Hoja Na. 7: TRA
wanatumia vitisho, mabavu na mifumo kandamizi katika kukusanya kodi
29.
Mheshimiwa spika, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
inaendelea na jitihada za kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi analipa
kodi stahiki na kwa wakati. TRA inatekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi
kulingana na taratibu zilizoainishwa katika sheria na kanuni za kodi.
30.
Mheshimiwa spika, mlipakodi anakadiriwa kodi
ya kulipa na kupewa muda wa kuilipa kodi hiyo. Endapo kodi hiyo itakukuwa
haijalipwa katika muda ulioonyeshwa kwenye taarifa ya madai (Notice of
Assesment), TRA huchukua jukumu la kumkumbusha mhusika (reminder notice) na
kumtahadharisha hatua zitakazochukuliwa endapo kodi hiyo itaendelea kutolipwa
mpaka tarehe iliyooneshwa kwenye reminder
notice. Hatua zinazochukuliwa kwa mlipa kodi aliyekaidi ni kama vile: kukamatwa
mali zake na kuuzwa kwa njia ya mnada; na kuiagiza benki ya mlipa kodi
kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti yake kwenda TRA ili kulipia deni hilo.
Hatua hizi zipo kwa mujibu wa sheria na si vitisho, mabavu wala mifumo
kandamizi kwa wafanyabiashara. Ni vizuri walipakodi wakazingatia sheria na
kulipa kodi kwa hiari ili kuepuka usumbufu.
Hoja Na. 8: Serikali
inasema kuwa imeokoa shilingi bilioni 19 kwa kuondoa watumishi hewa kwenye
mfumo wa maliopo. Taarifa ya gharama za watumishi ya Benki Kuu ya Juni 2015
ilionyesha malipo ya mishahara
yaliongezeka kutoka bilioni 456 hadi shilingi bilioni 534 Juni 2016 ambalo ni
ongezeko la bilioni 78. Ongezeko hili limetoka wapi wakati Serikali
imesimamisha ajira mpya na kuondoa watumishi hewa?
31.
Mheshimiwa spika, Zoezi la kufuta watumishi
hewa kufuatia agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
lilianza Mwezi Machi, 2016. Hata hivyo, pamoja na kufutwa kwa watumishi hewa
malipo ya mishahara katika kipindi cha
Juni 2015 hadi Juni 2016 yameongezeko kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo:
·
Nyongeza ya mishahara iliyoanza kutumika Julai,
2015 ambapo jumla ya Shilingi bilioni 59 ziliongezeka kwa mwezi;
·
Watumishi 25,517 waliajiriwa katika kipindi hicho
wenye mshahara wa Shilingi bilioni 16.4 kwa mwezi;
·
Uwianishaji wa mishahara ya watumishi wa Vyuo
Vikuu ambapo jumla ya Shilingi bilioni 2.9 ziliongezeka;
·
Ongezeko la posho zinazoambatana na mishahara
shilingi bilioni 6.1 kwa mwezi kwa vyombo vya ulinzi na usalama;
·
Upandishwaji vyeo kwa watumishi mbalimbali; na
·
Uwianishaji wa maeneo ya kimishahara ambapo
kuanzia mwezi Februari, 2016 mishahara ya shilingi bilioni 33 iliyokuwa
inalipwa kupitia kwenye kasma ya matumizi mengineyo ilianza kulipwa kupitia
kwenye kasma ya mishahara.
32.
Mheshimiwa spika, Hivyo, endapo watumishi hewa
wasingeondolewa matumizi ya Serikali katika eneo la mishahara yangekewa makubwa
zaidi ya kiasi hicho kilicholipwa mwezi Juni, 2016.
Hoja Na. 9: Riba
kubwa zinazotozwa na mabenki ni kandamizi na
zinaumiza wanyonge
33.
Mheshimiwa spika, Katika mwaka ulioshia mwezi Septemba 2016,
riba za mikopo za mabenki zimekuwa zikipungua wakati zile za amana kuimarika
kwa viwango tofauti. Riba za mikopo zilipungua hadi kufikia wastani wa asilimia
15.83 mwezi Septemba 2016 kutoka asilimia 16.18 mwezi Septemba 2015. Wakati huo
huo, riba za amana zilibakia katika kiwango cha wastani wa asilimia 9.0. Aidha,
riba za mikopo ya mwaka mmoja ilipungua kutoka wastani wa asilimia 14.27 hadi
asilimia 13.23, wakati riba za amana za mwaka mmoja ziliongezeka kutoka asilimia
10.95 hadi asilimia 11.46. Hali hii ilifanya tofauti kati ya riba za mikopo na
amana za mwaka mmoja ipungue hadi kufikia wastani wa asilimia 1.77 mwezi
Septemba 2016 kutoka asilimia 3.32 mwezi Septemba 2015. Mwenendo huu wa viwango
vya riba unaonesha kuendelea kuimarika kwa mazingira ya kufanya biashara na
ushindani nchini hivyo kuvutia zaidi uwekezaji wa sekta binafsi. Aidha, hii
inaashiria kuimarika kwa ushindani wa Mabenki ili kuvutia wateja.
MAJIBU
YA HOJA ZA WAHESHIMIWA WABUNGE WAKATI WA KUJADILI MAPENDEKEZO YA MPANGO WA
MAENDELEO WA TAIFA KWA MWAKA 2017/18 NA MWONGOZO WA KUANDAA MPANGO NA BAJETI YA
SERIKALI KWA MWAKA 2017/18
NA.
|
MTOA HOJA
|
HOJA
|
UFAFANUZI WA
HOJA
|
KAMBI RASMI YA
UPINZANI BUNGENI
|
|||
1.
|
|
TRA inavuka lengo kutokana
na kukusanya maduhuli na kuyahesabu kama sehemu ya mapato ya kodi.
|
Maelezo yaliyotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni siyo sahihi.
Maelezo sahihi ni kuwa mapato ya kodi yanayokusanywa na TRA hutolewa
taarifa peke yake. Mapato yasiyo ya kodi (maduhuli) kwa Mashirika ya Umma na
Taasisi za Serikali yanayokusanywa na Taasisi husika na kutolewa taarifa na
Msajili wa Hazina. Mapato yanayokusanywa na Wizara hutolewa taarifa na Wizara
husika.
|
WAHESHIMIWA WABUNGE
|
|||
2.
|
Mhe. Josephat
Sinkamba Kandege
|
Pamoja na lengo
zuri la kuongeza mapato ya ndani ili ku kugharamia sehemu kubwa ya bajeti,
Serikali ihakikishe kuwa vyanzo vipya vya kodi vinavyopendekezwa katika bajeti ya mwaka wa Fedha 2017/18
havitakuwa kero kwa wafanyabiashara na wananchi wote kwa
ujumla.
|
·
Serikali inaendelea kutekeleza azma yake ya kupunguza
kodi zinazoleta kero kwa wananchi na kuharibu mpango mkakati wa Serikali
kuchochea ari ya ulipaji kodi kwa hiari.
·
Aidha, Serikali imejikita katika kuimarisha mkakati wa
kuboresha usimamizi na utawala wa kodi ili wafanyabiashara na wananchi waweze kulipa kodi zilizopo kwa hiari kwa
maendeleo ya taifa lao.
|
3.
|
Mhe. Ahmed Ally
Salum
|
Mabenki
yanapata hasara kutokana na kupungua mzunguko wa fedha. Serikali ichukue
hatua kwani endapo mabenki yatafungwa kutakuwa na athari katika uchumi wa
nchi
|
·
Katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2016, baadhi ya
mabenki ya biashara yalipata faida ndogo na baadhi zilipata hasara
ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliotangulia. Hali hii imeathiri
kasi ya utoaji mikopo na hivyo kupunguza mzunguko wa fedha. Miongoni mwa
sababu zilizochangia hali hiyo ni pamoja na Serikali kubaini watumishi hewa
ambao miongoni mwao walikopa kwenye mabenki na hivyo kusababisha kuwepo kwa
mikopo chechefu; serikali kuhamisha fedha za mashirika ya umma kutoka katika
mabenki ambazo zilikuwa zinatumika kukopeshea; na hatua ya serikali ya kubana
matumizi yasiyo ya lazima kama vile kufanya mikutano katika mahoteli. Aidha,
fedha zilizotumika kugaramia mikopo chechefu (provision for loan losses)
zilipelekea baadhi ya benki kupata hasara na nyingine kupata faida kidogo.
·
Hata hivyo, hali hii ni ya mpito na Serikali inashauri
mabenki ya biashara kubuni mikakati ya kuongeza amana zao ili kuongeza uwezo
wa kukopesha. Aidha, mabenki ya biashara yanatakiwa kuendelea kutumia mfumo wa
upashanaji taarifa za wakopaji (Credit Reference System) ili kupunguza
uwezekano wa kuongezeka kwa mikopo chechefu.
|
HITIMISHO
34.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru
Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia na kutupatia ushauri kuhusu vipaumbele na mambo muhimu ya kuzingatia
katika kazi inayofuata ya kuandaa Mpango na Bajeti ya Mwaka 2017/18.
35.
Mheshimiwa Spika, napenda niliahidi Bunge lako
Tukufu kwamba, Serikali itazingatia ushauri tuliopokea kwa kadri
inavyowezekana. Hakika haitawezekana kuzingatia kila kitu kilichosemwa hapa.
Baadhi yataendelea kuzingatiwa katika mipango ya maendeleo itakayofuata. Ili Bunge
lione wazi kwamba Serikali inasikia na inathamini ushauri mzuri wa Waheshimiwa
Wabunge, inakusudia kuweka bayana katika kitabu cha Mpango utakapokamilika
muhtasari wa ushauri uliozingatiwa, na ule tunaoona unafaa uzingatiwe katika
mipango itakayofuata na yale ambayo bado yanahitaji kuchambuliwa kwa kina kabla
ya kuzingatiwa kwenye mipango.
36.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya awamu ya Tano imedhamiria
kujenga Tanzania mpya ili kuwaondoa
watanzania kwenye lindi la umaskini haraka. Uamuzi huu unahitaji kuachana na
mazoea, unahitaji sacrifice na unahitaji tufanye kazi kwa bidii,
nidhamu na uadilifu. Tunataka uchumi ambao wananchi wengi wananufaika nao.
Nirudie tena, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli inajali
wafanyabiashara lakini budi sheria za nchi zizingatiwe.
37.
Mhe. Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment