Shirikisho la Mpira wa Miguu wa Miguu Tanzania (TFF), limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kagera (KRFA), Msafiri Ramadhani Msafiri.
Taarifa za kifo hicho kilichotokea usiku wa kuamkia Novemba 15, mwaka huu akiwa njiani kwenda Hospitali ya Milagwe, Kampala nchini Uganda, imetolewa na Katibu Mkuu wa KRFA, Saloum Chama ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji TFF.
Msiba huo umegusa familia ya mpira wa miguu akiwamo Rais wa TFF, Jamal Malinzi aliyemwelezea marehemu Msafiri alikuwa ni kiongozi mahiri na mwenye msimamo katika uamuzi wake.
“Ni msiba mwingine mzito kwenye tasnia ya habari,” amesema Malinzi na kuongeza kuwa weledi wake katika uongozi utabaki kuwa alama kwa sisi tulio hai na kutakiwa kuenzi.
Katika salamu zake za rambirambi, Malinzi ametuma kwa familia nzima ya mpira wa miguu Mkoa wa Kagera, familia, ndugu na jamaa huku akiwataka kuwa watulivu wakati huu mgumu wa kuomboleza kifo cha Msafiri anayetarajiwa kuzikwa leo kwenye makaburi ya Manispaa ya Kagera.
Enzi zake, marehemu Msafiri kabla ya kuingia kwenye uongozi, alipata kuchezea Kurugenzi ya Bukoba, Balimi pia ya Bukoba mkoani Kagera ambako pia alichezea timu ya Mkoa katika mashindano ya taifa.
Mbali ya kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Msafiri pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Karagwe kati ya mwaka 1999 hadi 2006.
No comments:
Post a Comment