Kocha na mchezaji mahiri wa zamani wa Timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mohammed Msomali amezikwa leo Septemba 9, 2016 kwenye makaburi ya Kola yaliopo barabara ya zamani ya Dar es Salaam-Morogoro.
Mbali ya wajumbe mbalimbali wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) waliohudhuria mazishi hayo kwa upande wa TFF iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi katika maziko hayo ya Msomali aliyefikwa na umauti akiwa na umri wa miaka 74.
Kocha Mohammed Msomali anaelezwa kuwa ‘gwiji’ la kandanda la Tanzania, alifariki dunia jana Septemba 08, 2016 saa saba mchana akiwa nyumbani kwake akisubiri kupata mlo wa mchana.
Katika nafasi ya kucheza, historia inaonesha kuwa Msomali nyota yake ilianza kuonekana kwenye timu mahiri ya Cosmopolitan ya Dar es Salaam kabla ya kuchezea klabu nyingine za Young Africans pia ya Dar es Salaam, Mseto ya Morogoro, Timu ya Mkoa wa Morogoro ‘Moro Stars’ na Timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kadhalika timu ya Bara ambayo ni maarufu kwa jina la Kilimanjaro Stars.
Wakati wa uhai wake, Msomali amepata kuzifundisha Mseto na Tumbaku za Morogoro ambayo aliipa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara (Klabu Bingwa Tanzania) mwaka 1975. Pia alizinoa Young Africans, Timu ya Mkoa wa Morogoro ‘Moro Stars’ na kwa muda mrefu timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ sambamba na ile ya Bara ambayo ni maarufu kwa jina la Kilimanjaro Stars.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Mzee Mohammed Msomali mahala pema peponi.
No comments:
Post a Comment