Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 1 September 2016

ASKOFU KILAINI: SERIKALI YA MAGUFULI INA NIDHAMU YA KAZI NA UDHIBITI WA FEDHA



Methodius Kilaini, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba

NA IDARA YA HABARI- MAELEZO
Mhashamu Baba Askofu Methodius Kilaini, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, amesema Serikali ya Awamu ya Tano ina nidhamu ya kazi ya hali ya juu na udhibiti wa matumizi ya fedha za serikali .
 Hayo ameyasema askofu huyo wakati akifanya mahojiano na Idara ya Habari Maelezo, kwa njia ya simu. 

Askofu Kilaini aliainisha maeneo kadhaa yanayoifanya Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuonekana ni  ya kipekee, na kusisitiza kuwa ni yenye  utendaji  wa kusema na kutenda, ambao umefuta utani kutoka kwa jirani zetu Malawi na Kenya , kuwa ukitaka maneno nenda Tanzania, alisema Kilaini .
Aidha, Askofu Kilaini alieleza kuwa utendaji WA Serikali ya awamu ya Tano umegawanyika katika sehemu tatu ambazo ni nidhamu katika kazi, udhibiti wa fedha za serikali, dhana ya kusema na kutenda na kuwajibika kwa watumishi wa serikali.
Kilaini ameongeza ni dhahiri watumishi wa Serikali kuwajibika kuwahi makazini kufanya kazi bila kulalamika.  Akitoa mfano Askofu Kilaini alisema hapa Tanzania nidhamu ya kazi ilikuwa enzi za serikali ya awamu ya kwanza, nanukuu “angalia wakati wa Waziri Mkuu Marehemu Edward Moringe Sokoine na hata Mheshimiwa Lyatonga Mrema alijaribu lakaini haikuwa endelevu.
Akisisitiza juu ya nidhamu ya kazi Askofu Kilaini alieleza hali halisi ya shule za Msingi na Sekondari Mkoani Kagera, kuwa sasa walimu wanawahi kazini bila kutoa visingizio na kuingia darasani na kufundisha. Siku za nyuma walikuwa wakienda shule kwa muda wanaopenda na hakuna aliyekuwa anawajibika kuwauliza au hata kuwachukulia hatua.
Askofu kilaini aliwashangaa wanaobeza fedha za ruzuku kutoka serikalini inayopelekwa kwenye shule za Msingi na Sekondari akisema wanafanya makosa makubwa kubeza kwani, ukiacha wale waliosoma enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, shule hizo hazijawahi kuwa na ndoto ya kupata fedha kutoa serikalini, hivyo hiyo fedha ambayo wengine wanaibeza ni mkombozi mkubwa kwa shule zetu na nina uhakika kiwango cha elimu kitaboreka.
Muelekeo wa serikali kudhibiti fedha za serikali njambo kubwa sana angalia suala zima la watumishi hewa, fedha hizo zimepotea, zingeweza kufanya mambo makubwa kwa wananchi wanyonge vijijini. Ni lazima tumshukuru kwa jambo hili limesaidia kuwa makini kwa watumishi waliopewa dhamana na jambo husika. 
Akiongezea Askofu Kilaini alielezea dhana ya Rais wa Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli ya kunena na kutenda imempa heshima kubwa sana hasa nje ya mipaka ya Tanzania kama Kenya na Malawi ambao walikuwa wanaibeza Tanzania kuwa nchi ya maneno maneno bila kutekeleza sasa dhana hiyo haipo. Anachosema Rais anatenda na kusema hakika msemo wake wa HAPA KAZI TU ni dhana ya matendo.
Askofu Kilaini aliwaasa vyama vya upinzani kufanya maandamano hasi na sio chanya, alihoji wajiulize faida inayotokana na maamuzi wanayoyafanya kama yana tija kwa Taifa. Aliongeza kwa kusema maandamano hasi ni kama kupinga mauaji ya Albino unyanyasaji wa kijinsia na mambo kama hayo.

Mahojiano hayo yaliyofanywa na Idara ya Habari – MAELEZO ilipata fursa ya kufamya mahojiano na Mhashamu Baba Askofu Methodius Kilaini Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba yaliyofanyika kwa njia ya simu tarehe 27/08/2016 Juu ya Utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kama yafuatavyo:
SWALI: Baba Askofu; Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani tangu mwezi Novemba 2015 kwa sasa takriban miezi kumi. Je, unalipi la kueleza wananchi juu ya utendaji wa serikali hii?
JIBU: Mimi binafsi nadhani na watu wengi wanafurahia utendaji wa Mheshimiwa Rais ambapo ni utendaji wenye upya wenye kuelekea mahali papya kwa ufupi Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ana muelekeo wake ambao utatufikisha mahali pazuri. Unajua kulikuwa na utani kutoka kwa majirani zetu Kenya na Malawi wanatutania wakisema ukitaka maneno nenda Tanzania ambao hawafanyi kazi, kwa sasa utani huo hauna nafasi.Utendaji huu ninautazama katika maeneo ya fuatayo:
(a) Nidhamu katika kazi kwa sasa inaonekana, siku za nyuma nidhamu ilipotea kabisa nidhamu hii ninayoiongelea ilikuwepo wakati wa utawala wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hapo katikati tulipoteza nidhamu hii akitoa mfano alisema kwa  sasa walimu wanawahi mashuleni na kuingia darasani kufundisha,.  Watumisi wote kwa ujumla wanaenda kazini wanawahi na wanakaa kazini na kufanya kazi. Hapo nyuma walimu  wamekuwa wakienda mashuleni wanavyotaka hawafundishi na hakuna mtu wa kuwawajibisha juu ya hilo, ukiangalia wakati wa awamu ya kwanza Waziri Mkuu Marehemu Edward Sokoine kulikuwa na nidhamu ya kazi ya hali ya juu. Hata nyakati za Mrema alijaribu hata kuondoa viti kwa wale wanaochelewa maofisini lakini bahati mbaya halikupata uungwaji mkono likaishia hivi hivi Bila kazi huwezi kupata maendeleo hivyo ni lazima tufanye kazi kwa bidii na nidhamu.
(b)                     Udhibiti wa fedha ambazo zilikuwa nyingi mitaani, pia fedha hiyo ilipatikana kwa kazi za kubabaisha. Napenda kukiri sasa ipo nidhamu ya fedha ya Serikali. Hapo nyuma nidhamu ya fedha  ilikuwa haipo mfano Wizara, Taasisi na Idara za serikali zilikuwa zinatafuta njia za kula fedha ya serikali bila tija kama kufanya semina , makongamano, warsha baada ya hapo wanahalalisha kugawana fedha wanavyopenda. Semina siku moja wataandika siku tatu, watakodi ukumbi wa hoteli wa bei ya juu sana bila sababu na matumizi mengine yasiyo ya lazima.

Kwa Mheshimiwa Rais Magufuli ameweza kuziba mianya yote kama vile kubaini watumishi hewa na kuelekeza fedha zilizookolewa kupelekwa maeneo muhimu kwa maendeleo ya wananchi kama shule za kata ambao hawakuwahi kufikiri katika maisha yao wanaweza kupata fedha za ruzuku ya serikali, watu wamekuwa wakisema fedha hizo ni kidogo lakini wakumbuke shule hizo hazijawahi kupata kitu kama hicho walikuwa wakilumbana na wazazi kutoa fedha na matokeo yake wanafunzi wengi waliacha shule kwa sababu wazazi walishindwa kulipa karo ya shule.
      Nina hakika kwa sasa elimu itaboreka na kujijenga kidogo kidogo, hakuna    haja ya kubeza juu ya jambo hili. Wale wanaobeza wanafanya dhambi kubwa wasubiri waone nini matokeo ya utaratibu huu.
(c) Dhana ya kusema na kutenda Tanzania ilikuwa inabezwa na majirani zetu kama Kenya Malawi kuwa ni nchi ya maneno maneno tu , lakini kwa sasa Mheshimiwa Rais amerudisha dhana ya kusema na kutenda hapo hapo. Mfano lengo la kuhamia Dodoma ni la miaka mingi tangu 1973, lakini ametamka na kuanza kutenda na kutoa muda maalum wa kutekeleza jambo hilo. Kama halijatekelezwa hatua zinachukuliwa na linaonekana na hata hao majirani zetu wanaona na wamekubali kuwa sasa Tanzania ni Hapa Kazi tu .Lakini nisieleweke vibaya kuwa labda awamu zilizopita hazikufanya kitu la hasha, kila awamu ilifanya kazi yake na Mheshimiwa Magufuli anaendeleza kazi nzuri iliyofanywa na watangulizi wake.
(d)Utendaji wa kazi kwa watumishi wa serikali kama umeharibu unapaswa kuondoka sio kuhamishiwa mahala pengine. Wasimuelewe vibaya Rais, bali ukiondolewa ridhika na toa fursa kwa watu wengine, wapishe wengine watekeleze na wewe utapata nafasi ya kujifunza.
Watumishi wa serikali kuendelea kung’ang’ania kukaa kwenye nafasi za madaraka hata pale umri unapofikia. Tuna vijana wengi wapo mitaani hawana kazi wanahitaji ajira hawa wazee wakiondoka kwa wakati na vijana watajaza nafasi zao, maendeleo yataonekana na malalamiko yatapungua. Hii ni fursa pekee kwa vijana tofauti na Ulaya vijana wakuchukua hizo nafasi hawapo ni wa kutafuta.
SWALI: Nini maoni yako kuhusu mwelekeo wa nchi kwa sasa?
JIBU: Muelekeo wa nchi kwa sasa ni mzuri, uongozi wowote ule wa nchi mara baada ya uchaguzi walioingia madarakani hujipanga na kujaribu mambo mapya, ndio maana wanapewa awamu mbili ili wajipange kisha waweze kutekeleza kile walichoahidi wananchi.  Mheshimiwa Rais hataki kufanya kazi kwa mazoea kuna mambo mengi mapya anajipanga tumpe nafasi  
Kwa sasa anaangalia pale alipo kama kuna makosa anarekebisha kabla ya kuanza kazi. nadhani tumpe nafasi anayostahili ili afanye kazi na baadhi ya mambo mengi ameshaanza kutekeleza kwa kukusanya fedha za mlipa kodi, ambapo zamani tulikuwa tunachangia. Mfano hapa Bukoba naona kwenye hospitali zetu angalau sasa dawa zinapatikana, wananchi watambue utekelezaji huu utaanza kuboreka polepole sio kwa mara moja kwa hiyo wanapopata changamoto ndani ya utekelezaji wa ahadi za Rais waziseme kwa nguvu zote ili zitatuliwe tuweze kusonga mbele . Pole pole utekelezaji huo utaboreka.
Reli ya kati aliahidi kuijenga kwa viwango vya kimataifa (Standard Gauge) tunaona ameshaanza kutekeleza wanajenga kwa vipande vipande lakini mwisho wa siku tutafika angalau sasa kila kisemwacho kinaonekana
Mheshimiwa Rais ameahidi kununua Ndege kweli ametimiza, ameahidi,   kuleta   Meli, utaratibu umeshaanza nina hakika tutapiga hatua kubwa sana baada ya muda mfupi ujao.  
SWALI: Kuna maeneo ambayo yanawagusa moja kwa moja wananchi katika maisha yao ya kila siku na Mhe. Rais aliahidi kuyafanyia kazi kwa nguvu zote je hili limeanza kutekelezwa? Ni upi mtazamo wako kuhusu utekelezaji huo?
JIBU: Mheshimiwa Rais ameanza kutekeleza, watu wanalalamika hatuna hiki hatuna hiki lakini ameanza na anatekeleza, mfano shule za msingi na sekondari elimu bure ameanza polepole, amepeleka fedha kila mahali penye shule ya msingi na sekondari. Kwa upande wa afya zahanati zetu, hospitali zinaboreshwa pole pole Reli ya kati ni uti wa mgongo, nina uhakika polepole atafanya bila ya kuanza A huwezi kufika Z, kilichohitajika ni kukata mzizi wa kutokufanya.
Inaonekana kama hakipo lakini kipo kinaendelea na mwisho kitaonekana. Nafurahi kwa kuwa dhana ya kunena na kutenda ipo tutafika tunapotarajia na huu ndio mtazamo wangu kwa serikali ya awamu ya tano.
SWALI: Ili kuijenga Tanzania iliyo bora ni vema kukubali changamoto zote zinazojitokeza  na kuzifanyia kazi. Una lipi la kusema kuhusu madai ya Vyama vya Siasa nchini kunyimwa uhuru wa demokrasia?
JIBU: Madai ni kitu ambacho unatakiwa kukiangalia kwa uangalifu.Serikali ina mamlaka ya kuamua, kutenda na kutawala, haki ya vyama vya siasa kufanya kazi ya kuikosoa serikali katika hali chanya, sio hasi ni lazima kama watanzaniia tupendane na kuwa kitu kimoja na kufanya kazi kwa pamoja, kwa kuwa tunajemga nchi yetu sote. Tukumbuke mihimili mitatu Serikali, Mahakama na Bunge, hivi vyote vinapashwa kushirikiana na kuwa na uhusiano mzuri.
Uhusino kati ya serikali na vyama vya siasa vyama vya siasa kuikosoa serikali kwa mtazamo chanya serikali pia ijue vyama vya siasa ni lazima vipewe nafasi ya kuongea na serikali itimize wajibu wake
Serikali, vyama vya siasa lazima waelewe kuwa tunajenga nchi moja ya Tanzania, nchi hii ikibomoka tutabomoka wote hakuna atakaye nufaika na ukosoaji hasi ambao hauna manufaa kwa nchi ya yetu.  Hivyo wanasiasa waongee, kuongea, kwa maana ya vyama vya siasa kukutana na serikali na serikali uitimizwe wajibu wake   Serikali mamlaka ya kuamua na kutawala.
Mahakama, lazima Itoe haki bila kuingiliwa, Wabunge ni wawakilishi wa wanannchi na sehemu mahususi ya kuongea ni Bungeni. Wanasiasa wanaotoka kwa watu wanaowakilisha watu lazima wawasilishe matakwa wa wananchi, lakini wakumbuke umuhimu wa kukutana na kuongea badala ya kuleta vurugu ambazo wananchi hawakuwatuma hiyo haikubaliki.
SWALI:  Watanzania kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiishi kwa kuvumiliana na kuchukuliana bila kujali imani zao itikadi za kisiasa na makabila yao. Hivi karibuni uvumilivu huo umepungua na kukaribia kutoweka kabisa. Wewe kama kiongozi wa kiroho unaona nini kifanyike ili kulinusuru Taifa na migogoro ambayo imeanza kujitokeza?
JIBU: Tunu ya Tanzania ni uzalendo, umoja na amani, tumshukuru Baba wa Taifa kutuwekea misingi hii kwa kweli alifanya kazi kubwa katika kuimarisha umoja wa Tanzania. Misingi hii imewekwa bila kujali dini zetu itikadi zetu na makabila yetu.
Mfano viongozi wa dini tulijitahidi sana kupitia Baraza la Maaskofu wakati huo nikiwa Katibu wa Baraza hilo tuliunda baraza La maridhiano katika dini zetu zote tulizonazo, tukashirikiana kutatua matatizo madogo madogo yaliyokuwa yanajitokeza kwa kweli tulifaniikiwa. Hata sasa lipo Baraza la maridhiano kwa dini zote linafanya kazi nzuri sana sana, hili linatusaidia kutatua migogoo yote inayojitokeza katika jamii, serikali na vyama vya siasa.
SWALI: Unatoa ushauri gani juu ya changamoto unaziona kwa sasa ili Taifa liweze kusonga mbele na kutimiza azma ya Mhe Rais ya kuwatumikia wananchi kwa kuboresha maisha yao.
JIBU: Ili tuende pamoja tunahitaji kuwa kitu kiimoja ninaomba chama tawala, vyama vingine vya siasa na Bunge kuwa na lengo moja.
(a) Serikali ifanye kazi yake ya kutawala na sisi ni lazima kutoa ushirikiano  kwa watawala wetu, tusiwaache wenyewe tuwape ushirikiano.  Kila mmoja apewe nafasi yake, tufanye kazi  vyombo vya dola tuvisaidie ili tuweze kuishi kwa usalama mfano mimi nipo hapa kwa sababu kuna vyombo vya usalama vinavyonilinda. Ukiona vyombo vya usalama vinashambuliwa ujue tupo katika hali mbaya sana tusiruhusu hali  hii ianze kuota mizizi.  Usalama ukikosekana wote tutaangamia usalama wetu hauna mjadala.
(b)                        Kwa wale ambao sio wana siasa tusaidie kutoa maoni yetu kwa serikali ukifanya vizuri katika nafasi yako lazima utachaguliwa tu na ukifanya vibaya watakutoa. Nashukuru sana kwa wabunge wa upinzani kwa kukubali kurudi bungeni.
(c)  Kuhusu maaandamano, nadhani tufanye maandamano lakini yawe maandamano chanya yanayoleta maendeleo, Mfano kupinga ukatili kwa Albino na sio maandamano ya kupinga serikali hata kwa jambo lililo jema. Kazi ya vyama vya siasa ni kukosoa, kuisimamia serikali itekeleze majukumu yake na kutunga sheria sio kuhamasisha maandamano yasiyo na tija.
(d) Nashukuru sana kusikia wapinzani wanarudi Bungeni kuendelea na shughuli zao, wananchi wanatoa  maoni yao ili yaweze  kufanyiwa kazi na serikali, tunapashwa tuongee kwa uwazi na uhuru. Tuna vyombo vingi sana vya kutoa maoni yetu na yatawafikia wahusika ambao lazima wayafanyie kazi hakuna haja ya kufanya maandamano yasiyo na tija.
SWALI: Ushauri wako kwa Serikali, Vyama ya siasa na watanzania kwa ujumla?
JIBU: Serikali isikilize watu,kuchukua maoni yao na kuyafanyia kazi. Serikali ifanye kazi kwa bidii kuwaletea maendeleo wananchi, changamoto zipo ila wazifanyie kazi na kusonga mbele.
Vyama vya siasa vinatakiwa kushauri na kukosoa ikiwa ni pamoja na kuisimamia serikali katika utekelezaji kwa kile walichoahidi na kupitishwa ndani ya Bunge tukufu.



Wananchi wenzangu wa Tanzania tumuunge mkono mheshimiwa Rais    tufanye kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo nasema  “Hapa kazi tu”  Hapa kazi tu

No comments:

Post a Comment