Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto meza kuu) akizungumza na Watendaji
Wakuu wa Idara ya Uhamiaji nchini (kushoto) pamoja na Wakuu wa Idara wa Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi (kulia), kuhusu masuala mbalimbali ya utendaji wa
kazi ndani ya Idara hiyo na Wizara kiujumla. Kikao hicho kilifanyika katika
Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Kulia meza kuu ni
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Injinia Hamad Masauni. Wakwanza upande wa kulia ni
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Simba Yahya, na wakwanza upande wa
kushoto ni Kaimu Kamishna wa Uhamiaji, Victoria Lembeli. Picha zote na Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Balozi Simba Yahya akizungumza
jambo katika kikao kazi alichokiitisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles
Kitwanga (kushoto meza kuu) kuzungumza na Watendaji Wakuu wa Idara ya Uhamiaji
nchini pamoja na Wakuu wa Idara wa Wizara yake, kuhusu masuala mbalimbali ya
utendaji kazi ndani ya Idara hiyo na Wizara kiujumla. Kikao hicho kilifanyika
katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Kulia meza
kuu ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Injinia Hamad Masauni. Wakwanza upande wa
kushoto ni Kaimu Kamishna wa Uhamiaji, Victoria Lembeli. Picha na Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi.
Kaimu
Kamishna wa Idara ya Uhamiaji, Victoria Lembeli (wapili upande wa kushoto) akimfafanulia
jambo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto meza kuu)
kuhusu masuala mbalimbali ya kikazi ndani ya Idara yake katika Kikao kazi cha Watendaji
Wakuu wa Idara ya Uhamiaji pamoja na Wakuu wa Idara wa Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Nchi, kilichoitishwa na Waziri Kitwanga na kufanyika katika Ukumbi wa
Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Wakwanza upande wa kulia ni Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, balozi Simba Yahya. Picha na Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi.
Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto meza kuu), Naibu Waziri wa
Wizara hiyo, Injinia Hamad Masauni (kulia meza kuu) wakifurahi jambo pamoja na Watendaji
Wakuu wa Idara ya Uhamiaji (kushoto) na Wakuu wa Idara wa Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi (kulia), wakati wa kikao cha kujadili masuala mbalimbali ya
utendaji kazi ndani ya Idara hiyo na Wizara kiujumla. Kikao hicho kilifanyika
katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam leo. Wakwanza
upande wa kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Simba Yahya, na
wakwanza upande wa kushoto ni Kaimu Kamishna wa Uhamiaji, Victoria Lembeli. Picha
zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
*****************************************************************************
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Charles Kitwanga ameagiza yafanywe mabadiliko
makubwa katika Vitengo mbalimbali vya Idara ya Uhamiaji ili kuboresha huduma na
kuimarisha uadilifu katika Vitengo hivyo.
Mheshimiwa
Kitwanga ametoa maagizo hayo leo wakati alipofanya kikao na Viongozi wa Idara
ya Uhamiaji ambapo pia kilihudhuriwa na Viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi, wakiwemo Wakuu wa Idara na Vitengo vya Wizara. Kikao hicho kilifanyika katika Makao Makuu ya
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Katika
kikao hicho, Mheshimiwa Kitwanga ameagiza watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji
walioko Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, wahamishwe na kupelekwa maeneo mengine
nchini, wakiwemo wale wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Wengine
watakaohamishwa ni kutoka Kitengo cha Pasipoti, Uhasibu, Hati za Ukaazi na
Kitengo cha Upelelezi, vyote vya Makao Makuu ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam.
Aidha
ameagiza pia kuwa Wakuu wote wa Vitengo vya Upelelezi vya wilaya zilizopo
jijini Dar es Salaam, na pia wale wa Vituo vya Tunduma, Mtukula, Holili na Kasumulo,
wahamishiwe maeneo mengine, na pia watumishi wote waliokaa kwa zaidi ya miaka
mitatu katika Vituo hivyo.
Amesema
hatua hii inayochukuliwa sasa ni mwanzo
tu wa mabadiliko makubwa yatakayofanywa katika Idara ya Uhamiaji ili kuboresha
huduma zinazotolewa na Idara hii ambayo ni moja ya Idara muhimu za Serikali.
Amesema
katika kuisafisha Idara hii, uangalifu mkubwa utachukuliwa ili kuhakikisha kuwa
hakuna mtumishi anayeonewa wala kupendelewa, lakini lengo kubwa ni kuvunja mtandao wa wapokea rushwa na wale
wasiowajibika.
Amesema
kufuatana na utafiti uliofanywa hivi karibuni umeonyesha kuwa matatizo ya
rushwa katika Idara ya Uhamiaji yanashika nafasi ya kwanza kwa kuwa na asilimia
30, asilimia 20 ni uongozi mbovu na asilimia 20 ni matumizi mabaya ya madaraka.
Asilimia 15 inahusisha vitendea kazi wa mifumo hafifu ya kufanya kazi, asilimia
10 huduma mbovu na asilimia 5 ukabila na upendeleo.
Amewataka
Viongozi na watumishi wote wa Idara ya Uhamiaji kufanya kazi zao kwa kuzingatia
sheria, kanuni na maadili ya kazi na waepuke vitendo vya kupokea rushwa na
kusaidia wahamiaji haramu na wauza madawa ya kulevya.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali –
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
23 Februari, 2016
No comments:
Post a Comment