Na Ahmad Mmow, Lindi
Wingi wa vizuizi vya ukaguzi barabarani umetajwa kusababisha rushwa na usumbufu kwa wafanyabiashara wanaosafarisha mazao ya misitu.
Hayo yalielezwa jana na wafanyabiashara wa mbao na magogo kwenye warsha ya wafanya biashara wa mbao na magogo wa uwanda wa Selous hadi Ruvuma, iliyofanyika jana katika manispaa ya Lindi.
Wakizungumza kwenye warsha hiyo iliyoandaliwa na mashirika ya kiraia ya Jumuiko la Maliasili Tanzania(TNRF), Mtandao wa Kijamii wa Usimamizi wa Misitu(MJUMITA) uhifadhi, usimamizi na maendeleo ya mpingo(MCDI) kupitia kampeni ya mama misitu inayofadhiliwa na serikali ya Finland kupitia ofisi za WWF zilizopo nchini, walisema vizuizi hivyo vinasababisha rushwa, usumbufu na kuwapotezea muda.
Frank Nganyanyuka alisema wingi wavizuizi unasababisha wafanyabiashara hao kupoteza muda mwingi barabarani.
Alisema kutoka Nachingwea hadi Dar-es-Salaam kuna vizuizi takribani 19, ambavyo vinasababisha wachelewe barabarani
"Wastani kila eneo lenye kizuizi tunatumia saa moja, maana yake siku mzima inakwisha kwa ajili ya kusimama, vizuizi vipunguzwe havinafaida zaidi ya kuchochea rushwa tu," alisema Nganyuka.
Mfanyabiashara Mikidadi Kinogeandanga wa Lindi, alisema licha ya kuchelewa lakini pia maofisa waliopo katika vizuizi hivyo niwasumbufu na hawaziamini nyaraka ziliandikwa na maofisa wenzao wa kule zilikotoka mbao na bidhaa nyingine za misitu. Alihoji nisababu gani zinazosababisha wasiwaamini wenzao ambao wanadhamana na mamlaka kama yao.
Alibainisha ili kuepuka kuchelewa wanajikuta wanarahisha usumbufu kwa kutoa chochote, kwa madai bila kufanya hivyo wanasumbuliwa hata kama hawakiuki, sheria, taratibu na kanuni.
"Malendego, Jaribu, Kimanzichana sijui wapi, niusumbufu tupu, lakini yote hayo nikutaka rushwa tu," alisema Kinogeandanga.
Ali Kinunga anayefanyia biashara yake wilayani Kilwa, licha kuyalalamikia wingi wa vizuizi alilaumu serikali kutowashirikisha wafanyabiasha wa mazao ya misitu ili kupata maoni yao kabla ya kupitisha sheria ambazo baadhi yake siyo rafiki na zinawaumiza.
Alitolea mfano mabadiliko ya tozo mbalimbali ambayo yamekuwa yakiwaumiza. Kwamadai kuwa wanaotengeneza kanuni na sheria hawajui matatizo na vikwazo wanavyokutanavyo wafanyabiashara. Badala yake wamekuwa wakitoa maagizo tu.
Naye Bakili Kilete anayefanyia biashara yake katika wilaya hiyo ya Kilwa, alisema sheria zinazohusu misitu siyo rafiki kwa wafanyabiashara ikiwamo na uwepo wa vizuizi vingi visivyo natija kwa serikali na wafanyabiashara.
"Usumbufu na wingi watozo unasababisha tutafute njia nyingine ili tupate faida, maana kwa sheria zilizopo kama utataka utii na kutekeleza huwezi kufanyabiashara hii," alisema Kilete.
Akijibu malalamiko ya wafanyabiashara hao, mratibu wa usimamizi shirikishi wa misitu nchini, Joseph Kigula, alisema sababu ya kuwepo vizuizi vingi ni kwasababu baadhi ya wafanyabiashara sio waaminifu.
Akibainisha kuwa wafanyabiashara wangekuwa waaminifu kusingekuwa na sababu ya kuwa na vizuizi vingi.
No comments:
Post a Comment