Na Daniel Mbega
MABINGWA watetezi
wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga, wamerejea kile walichokifanya
mwaka 1996 katika utawala mpya wa Serikali baada ya kuwachapa mahasimu wao
Simba kwa mabao 2-0 na kurejea kileleni.
Hii ni mechi yao
ya kwanza tangu Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli kuingia
madarakani na wameupata ushindi kama ule ule wa mwaka 1996.
Rekodi zinaonyesha
kwamba, Februari 25, 1996 katika mechi yao ya kwanza katika utawala mpya wa
Awamu ya Tatu chini ya Benjamin Mkapa, Yanga iliitandika Simba mabao 2-0 kwenye
Ligi Daraja la Kwanza (kabla haijawa Ligi Kuu).
Bao la Donald
Ngoma la dakika ya 39 na lile na Amissi Tambwe katika dakika ya 72 yalitosha
kuipa Yanga ushindi wa mabao 2-0 kama ule ilioupata siku 112 zilizopita, yaani
Septemba 26, 2015.
Simba walicheza
wakiwa pungufu baada ya mchezaji wake Abdi Banda kupigwa kadi nyekundu, hatua
iliyodhoofisha zaidi nguvu ya Wekundu wa Msimbazi.
Kwa kawaida Yanga imekuwa na bahati ya kuanza
vyema mechi dhidi ya watani wao wa jadi katika utawala mpya wa serikali, kwani
kumbukumbu zinaonyesha kwamba, mechi yao ya kwanza kabisa kwenye Ligi ya Taifa
katika utawala wa Rais Julius Nyerere Juni 7, 1965, Yanga ilishinda kwa
bao 1-0, mechi ambayo hata hivyo ilivunjika dakika ya 80 kutokana na kutanda
kwa giza kwenye Uwanja wa Ilala (sasa Kumbukumbu ya Karume).
Katika awamu ya pili ya Alhaj Ali Hassan
Mwinyi, mechi ya kwanza ya mahasimu hao ilishuhudia sare ya bao 1-1 Machi 15,
1986 na mechi yao ya kwanza ya ligi chini ya Jakaya Kikwete katika awamu ya nne
Machi 26, 2006 timu hizo zilitoka suluhu.
Hata hivyo, timu
hizo ziko nguvu sawa katika ‘kumaliza na Serikali’ kwani Yanga ilimaliza
utawala wa Mwalimu Nyerere kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba Agosti 10,
1985 na ikaupata ushindi kama huo katika mechi ya mwisho chini ya utawala wa
Kikwete Septemba 26, 2015.
Simba nayo
ilimaliza utawala wa Mwinyi kwa ushindi wa mabao 2-1 Oktoba 4, 1995 na
ikamaliza utawala wa Mkapa kwa ushindi wa mabao 2-0 Agosti 21, 2005.
Kwa ushindi huo wa leo, Yanga
imerejea kileleni kwa kufikisha pointi 46 dhidi ya 45 za Simba, lakini ikiwa na
mechi moja mkononi.
Aidha, vijana hao wa Jangwani
wamefikisha mabao 44 ya kufungwa na kufungwa mabao 9 tu, wakati Simba wamefunga
mabao 35 na kufungwa 13.
No comments:
Post a Comment