Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linawataka
wasanii wote kuwa makini na wakuzaji Sanaa (Mapromota) au baadhi ya wanaojiita
wadau wa Sanaa ambao wamekuwa wakitumia njia za kiulaghai na utapeli katika
kujipatia faida na manufaa kupitia mgongo wa Wasanii.
Baraza linatoa angalizo hili kufuatia kuwepo kwa
ongezeko la matukio ya baadhi ya watu wanaojiita wadau wa Sanaa ambao wamekuwa
wakiwadanganya wasanii na kuwalaghai kwa kuwaahidi fursa mbalimbali kama za
maonesho ya ndani na nje ya nchi ambazo hata hivyo zimekuwa zikiishia katika
kuwaletea wasanii matatizo kiuchumi na kijamii.
Aidha, watu hao wamekuwa wakitumia majina ya
viongozi wa Serikali kuwatapaeli wasanii na kujipatia fedha isivyo halali.
BASATA linapenda kuwakumbusha wasanii kwamba kabla
hawajaingia makubaliano yoyote na mtu, asasi au kampuni yoyote wawasiliane na
wanasheria au watoe taarifa Ofisi za Utamaduni za wilaya au manispaa zilizo
karibu nao ili kuhakikisha wanaepuka ulaghai na udanganyifu kutoka kwa watu hao
wasio waaminifu.
Aidha, kwa wasanii walioko Dar es Salaam BASATA linawaelekeza
kufika Ofisi zake zilizoko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Slaam ili wapate
msaada wa kisheria na kujiridhisha kama makubaliano yao ni halali na ya
uhakika.
Mwisho kabisa, BASATA linapenda kuwakumbusha
wasanii kwa ujumla kwamba, tangu Januari Mosi mwaka 2013 tasbia za muziki na
filamu ni rasmi hivyo Wasanii wote hawana budi kusajiliwa na Baraza la Sanaa la
Taifa (BASATA) na wanafanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za
uendeshaji wa kazi za Sanaa nchini.
Aidha, kila msanii anawajibika kuhakikisha
anafanya kazi na mtu, watu, asasi au kampuni iliyo na vibali halali vya
kuendesha shughuli za Sanaa na si vinginevyo.
Sanaa ni Kazi, Tuitunze, Kuikuza na Kuithamini
Godfrey
L. Mngereza
Katibu Mtendaji - BASATA
No comments:
Post a Comment