Na Daniel Mbega
JUMAMOSI
hii Februari 20, 2016 bingwa wa ‘kucheka na nyavu’ wa miaka yote Uingereza,
James Peter ‘Jimmy’ Greaves, atakuwa anasherehekea miaka 76 ya kuzaliwa kwake,
lakini kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kutakuwa na habari nyingine
wakati mahasimu wakuu wa soka Tanzania, Yanga na Simba watakapokuwa wakivaana
kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Timu
hizo zinapambana katika siku ya 51 ya mwaka, lakini ni baada ya siku ya 112
tangu zilipopambana mara ya mwisho – katika mchezo wa kwanza wa msimu wa
2015/2016 – Septemba 26, 2015 kwenye uwanja huo huo na Yanga wakaibuka washindi
kwa mabao 2-0 wakilipa kisasi cha kufungwa ‘bao la kizembe’ na pekee Machi 8,
mwaka huo lililopachikwa kimiani na Emmanuel Okwi.
Achana
na akina Alan Shearer, Wayne Rooney na Thierry Henry, mkongwe Greaves ndiye
mchezaji pekee aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye ligi ya juu (top flight)
wakati huo ikiwa Ligi Daraja la Kwanza, ambapo alipachika wavuni mabao 357
dhidi ya 260 ya Shearer.
Jambo
la kufurahisha zaidi, mabao 268 kati ya hayo yalifungwa na Greaves akiwa na
Tottenham Hotspurs pekee, wakati yale ya Shearer alifunga katika klabu za
Blackburn Robers na Newcastle United.
Greaves
pia ndiye mchezaji pekee katika ligi ya Uingereza kuibuka mfungaji bora kwa
misimu sita na alicheza ligi hiyo kati ya mwaka 1957 hadi 1972.
Kwamba
ni timu gani kati ya Yanga na Simba itakayosherehekea ushindi na kuungana na
Greaves kwenye ‘birthday’ yake Jumamosi hii ni jambo lililo gumu kutokana na
rekodi ya timu hizo mbili, ambazo kimsingi ndizo zilizoleta mwanga wa soka
nchini.
Tangu
Simba ilipozinduka kutoka katika kufanya vibaya kwenye ligi na hatimaye kukalia
usukani mpaka sasa, kumwekuwa na mhemko mkubwa baina ya timu hizo mbili,
mashabiki na wanachama wake wakitambiana kwamba timu yao itaibuka na ushindi.
Huku
zitasikika kelele za: “Amesimama kidedea, eeeh kidedea!” na kule: “Kitimtimu,
mtakiona leo, nyumba ya shetani mwendawazimu kaingiaje!”
Lakini
kelele hizo zitahitaji pia kuangalia matokeo ya uwanjani yakoje, vinginevyo
upande mmoja unaweza kuzizima.
Hapo
hakuna ugomvi, ni burudani ya jukwaani huku mashabiki wakiendelea kutazama
buradani nyingine ndani ya uwanja wakati vijana walio katika jezi nyeupe na
nyekundu wakipelekeshana puta na wenzao walio kwenye jezi za kijani na manjano.
Matokeo
baina ya mechi hizo daima huwa hayatabiriki na tangu Simba ‘walipoikanyaga’
Yanga kwa mabao 5-0 Mei 6, 2012, wamevuna ushindi mmoja tu wa Machi 8, 2015
wakati Okwi alipopachika bao la pekee huku kipa wa Yanga akiwa ametoka langoni.
Itakumbuka
kwamba, katika kipindi baada ya kipigo kile cha aibu kwa Yanga, timu hizo
zimekutana mara saba, Yanga ikishinda mara mbili na Simba mara moja, huku
zikitoka sare mechi nne.
Zilipokutana
Oktoba 3, 2012 zilitoka sare 1-1, mechi ya Mei 18, 2013 Yanga wakashinda 2-0,
Oktoba 20, 2013 timu zikatoka sare ya 3-3, Aprili 19, 2014 sare ya 1-1 na
Oktoba 18, 2014.
Simba
inaingia uwanjani ikiwa haina mshambuliaji mwiba wa Yanga – Okwi – lakini Yanga
inao wachezaji wake wote wawili walioipa ushindi Septemba 26, 2015 ambao ni Amissi
Tambwe aliyefunga dakika ya 44 na Malimi Busungu aliyepachika dakika ya 79
ambaye pia ndiye aliyetoa pasi ya bao la kwanza.
Lakini
mechi hiyo ilishuhudia Mbuyi Twite akipewa kadi nyekundu baada ya kupokea kadi
ya pili ya njano kwa kuchelewesha muda.
Yanga,
bingwa mtetezi, ndiyo ina kibarua kigumu Zaidi kwa sababu licha ya kupitwa
mchezo mmoja na Simba, inahitaji kushinda mechi hiyo ili iweze kurejea
kileleni.
Simba
ina pointi 45 baada ya kushuka dimbani mara 19 wakati Yanga imecheza mechi 18
na ina pointi 43, hivyo ikiwa Yanga itashinda, basi itafikisha pointi 46 na
kuweka hai matumaini ya kutetea ubingwa wake.
Kupoteza
mechi hiyo kuna maana moja kwa Yanga, itakuwa imeuweka rehani ubingwa wake kwa
sababu Simba, ambayo tangu ilipomtimua kocha wake Dyran Kerr na kumwajiri
Mayanja Jackson imeshinda mechi sita mfululizo, ina hasira za kuukosa ubingwa
huo kwa misimu mitatu na sasa ndio wakati wake.
Matokeo
ya sare bado hayatainufaisha Yanga, lakini itakuwa ni faida kwa Simba ambayo
itakuwa na uhakika wa kuhamishia ushindani wake kwa Azam inayoshika nafasi ya
tatu ikiwa na mechi mbili mkononi na kukusanya pointi 42.
Mechi
baina ya timu hizi mbili kongwe katiba katika historia ya kandanda nchini huwa
zinatawaliwa na vituko vingi mno. Kuvunja nazi, kuoga maji ya maiti, kuruka
ukuta, kuingia uwanjani kinyumenyume na mengine kama hayo hutajwa kwamba ni
sehemu ya kuhanikiza ushindani.
Hata
hivyo, kwa sasa hawawezi kuruka ukuta kama ilivyokuwa miaka ile ya zamani, wala
hawawezi kuoga maji ya kuoshea maiti au kuvunja nazi hadharani, kwa sababu
Sheria za Soka haziruhusu ushirikina na timu hizo mbili zimekwishawahi kutozwa
faini kwa vitendo hivyo.
Safari
hii timu zote zinatokea visiwani – Simba ilikuwa imepiga kambi Unguja na Yanga,
baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 kwenye mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa
Afrika dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius, ilikwenda moja kwa moja
kisiwani Pemba.
Mechi
zao
Hii
itakuwa mechi ya 81 kuzikutanisha Simba na Yanga kwenye Ligi Kuu tangu mwaka
1965 ilipoanzishwa Ligi ya Taifa na aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Milan
Celebic.
Katika
kipindi chote hicho, msisimko wa kuelekea mechi hizi umekuwa mkubwa, bila
kujali nani anawania kitu gani.
Hata
hivyo, katika mechi 80 zilizopita, Watanzania wameshuhudia Yanga ikitawala
zaidi kwa kushinda mara 30, wakati Simba imeshinda mara 23. Timu hizo zimetoka
sare mara 27 huku mabao 165 yakifungwa. Kati ya mabao hayo, Yanga imefunga 89
na Simba imefunga 77. Ikumbukwe kwamba, mechi hizi hazihusishi mechi za Ligi ya
Muungano wala mashindano mengine.
Msimamo
kamili wa Yanga na Simba:
Yanga 80 30 27 23 89 – 77
Simba 80 23 27 30 77 - 89
Azam,
ambayo Jumapili Februari 14, 2016 ilipata kipigo cha kwanza iliponyukwa na
Coastal Union bao 1-0 jijini Tanga, Jumamosi hii itakuwa ugenini kwa Mbeya City
kwenye Uwanja wa Sokoine ikitaka kufufua matumaini ya kunyakua ubingwa huo kwa
mara ya pili.
Lakini
Mbeya City nayo inaonekana kuwa imara tangu ilipomuajiri mchezaji wa zamani wa
Malawi, Kinnah Phiri, ambapo Februari 14, 2016 iliichabanga Toto African mabao
5-1 hapo hapo Mbeya.
Majimaji,
ambayo inashika nafasi ya pili kutoka mkiani, itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar
mjini Songea huku ‘Wakata Miwa’ hao kutoka Turiani wakihitaji ushindi
kujiimarisha Zaidi kwenye nafasi ya nne nyuma ya Azam.
Maafande
wa Mgambo Shooting walio katika nafasi ya 11 huku wakiugulia kipigo cha bao 1-0
kutoka kwa African Sports ‘Wana Kimanumanu’ Februari 13, 2016, watawakaribisha ‘Wajelajela
Gwaa’ Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Wakatisha
tiketi wa Shinyanga, Stand United, ambao Februari 13, 2016 walizabuliwa mabao
2-1 na Simba kwenye uwanja wao wa nyumba – Kambarage – Jumamosi hii
wanawakaribisha maafande wa JKT Ruvu Stars wakihitaji ushindi ili kuondoka
katika nafasi ya saba waliko na pointi 29.
‘Wana
Kishamapanda’ Toto African wao watakuwa nyumbani kuwakaribisha jirani zao wa
Kagera Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, wakitaka kuwaaminisha mashabiki wao
kwamba wako vizuri na wanaweza kuwapiku Mbeya City katika nafasi ya nane ambako
wanafungana kwa pointi 21. Kagera Sugar iko nafasi ya 14 na inahitaji ushindi
ili iepukane na balaa la kushuka daraja msimu huu.
Mwadui
inayoshika nafasi ya sita, itaikaribisha Coastal Union ambayo inashika nafasi
ya 13 na iko kwenye hatari ya kushuka daraja kama ilivyo kwa ndugu zao African
Sports ambao Jumamosi hii watakuwa ugenini kwa Ndanda kwenye Uwanja wa
Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Ratiba ya mechi za Jumamosi 20/02/2016:
Majimaji
- Mtibwa Sugar
Mbeya
City - Azzam
Mgambo
- Tanzania Prisons
Stand
U. - Ruvu Stars
Toto
Africans - Kagera Sugar
Young
Africans - Simba
Mwadui
- Coastal Union
Ndanda
- African Sports FC
Msimamo ulivyo sasa:
P W D L G Pts
1. Simba 19 14 3 2 35:11 45
2. Young Africans 18 13 4 1 42:9 43
3. Azzam 17 13 3 1 31:11 42
4. Mtibwa Sugar 18 9 6 3 21:12 33
5. Tanzania Prisons 18 8 6 4 18:17 30
6. Mwadui 19 8 5 6 19:16 29
7. Stand U. 18 9 2 7 18:15 29
8. Mbeya City 19 5 6 8 20:23 21
9. Toto Africans 19 5 6 8 18:27 21
10. Ndanda 19 4 8 7 17:19 20
11. Mgambo 19 4 5 10 15:24 17
12. Coastal Union 19 3 7 9 12:20 16
13. Kagera Sugar 19 4 4 11 10:22 16
14. African Sports FC 19 4 4 11 6:19 16
15. Majimaji 19 4 4 11 11:32 16
16. Ruvu Stars 19 3 5 11 18:34 14
CREDIT: FIKRAPEVU
No comments:
Post a Comment