Mzee Kassim Mapili wakati akiwa amelazwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili. Kulia ni Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania, Addo November.
Kassim Mapili akipiga gitaa la solo kwenye jukwaa la bendi ya Mjomba Mrisho Mpoto.
Na Daniel Mbega
“KIFO oooh kifoo, kifooo kifoooo, kifo
hakina huruma!” Naam. Ndivyo alivyoimba marehemu Ramazan Mtoro Ongalla ‘Dk.
Remmy’ wakati akiwa na bendi yake ya Super Matimila ‘Wana Bongo Beats’
akiomboleza kuhusu ‘kifo’, Fikra Pevu
inaripoti.
Kweli
kifo hakina huruma, kwa sababu kinaweza kumchukua yule umpendaye katika wakati
ambao bado unamhitaji.
Katika
albamu yao ya Nippon Banzai ya mwaka 1994, Zaiko Langa Langa ‘Nkolo Mboka’
wanasema ‘Liwa yo Moyibi’, yaani ‘Wewe kifo ni mwizi’! Hakika kifo ni
mwizi kwa sababu kinatokea bila taarifa, hakipigi hodi, kinashambulia na
kuwaacha watu wakiwa na majonzi na mpendwa wao.
Hakika
ndivyo ilivyotokea kwa mkongwe wa muziki nchini Tanzania, al-marhum Kassim Said
Mapili (79), ambaye amefikwa na mauti Februari 24, 2016 akiwa amelala mwenyewe
nyumbani kwake maeneo ya Tabata TIOT jijini Dar es Salaam, tena baada ya
kurejea kutoka kuangalia mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya Arsenal na
Barcelona.
Kifo
hakikumpa nafasi Mzee Mapili hata kuwaaga wapendwa wake. Tasnia ya muziki wa
dansi ikiwa imetetereka, hakika ilikuwa inamhitaji mkongwe huyu japo kwa
ushauri tu.
Anazikwa
leo Ijumaa, Februari 26, 2016 saa 10:00 jioni katika makaburi ya Kisutu jijini
Dar es Salaam.
Kwa
wadau wa muziki, hakuna asiyemfahamu Mzee Mapili, afande aliyevua magwanda ya
Polisi akiwa na cheo cha Sajini na kuanza kuzitumikia bendi za muziki wa dansi
za uraiani.
Alikuwa
hakosekani katika matukio mengi yaliyohusu jamii, na ndiyo maana hata wakati wa
mazishi ya mtangazaji na mchambuzi wa masuala ya muziki wa kituo cha Radio
Tumaini, Fred Mosha ‘Mkuu’, Jumatatu Februari 21, 2016 pale kwenye makaburi ya
Kinondoni, Mzee Mapili alipewa fursa ya kuzungumza machache na akamuimbia
akisikitika kuondoka kwake mapema.
Kinachosikitisha
zaidi ni kwamba, ilichukua takriban siku mbili kabla ya kubaini kwamba
mwanamuziki huyo alikuwa amefariki dunia.
Taarifa
za awali zilieleza kwamba, tangu aliporejea chumbani kwake Jumanne usiku baada
ya kutazama mechi ya Arsenal na Barcelona kwenye luninga, hakuweza kutoka nje
hadi Alhamisi Februari 25, 2016 wakati majirani walipolazimika kutoa taarifa
polisi ambao walivunja mlango wa chumba cha Mzee Mapili na kukuta
amekwishafariki.
Miezi
michache iliyopita Mzee Mapili alilazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
kutokana na kusumbuliwa na tatizo la moyo, lakini baadaye mwenyewe akasema
alikuwa anaendelea vizuri kutokana na kusaidiwa na msanii mkongwe anayeishi
Marekani, Salma Moshi, ambaye alimlipia Bima ya Afya na hivyo kusaidia kupata dawa
zote zinazohitajika bila ya matatizo.
“Lakini Mola, eee, kazi yake haina
makosa, na wala hairekebishwi na binadamu yeyote…” ndivyo
alipopata kuimba ‘Bulldozer’ Marijani Rajabu Marijani katika kibao cha ‘Rufaa
ya Kifo’. Mungu alitenda kazi yake kwa Mzee Mapili na kuwaachia wapendwa wake
simanzi kubwa.
Binafsi
namkumbuka Mzee Mapili kwa mengi, nikiwa nimefahamiana naye tangu mwaka 1994
hasa wakati wa maandalizi ya mashindano ya ‘Mkali wa Solo’ nchini Tanzania,
nilitambua kwamba mzee huyo alikuwa mcheshi, mchangamfu na mzungumzaji hasa,
wakati huo akiwa Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (Chamudata).
Ni
wakati huo aliponieleza kwamba, wimbo alioutunga akiwa na bendi ya Polisi Jazz
‘Wana Vangavanga’ mwaka 1978 ndio uliomtambulisha mwanamuziki aliyekuja kuwa
mahiri nchini Tanzania, Shaban Ally Mhoja
Kishiwa, ambaye alijulikana zaidi kwa jina la TX Moshi William.
“Nilikuwa kiongozi na mpiga solo, si kwamba
sikuweza kuuimba, lakini niliona nikimpa kijana yule kutokana na sauti yake
ilivyokuwa, wakati huo akiwa kijana wa miaka 20,” nakumbuka alinieleza hivyo
Mzee Mapili wakati wakiwa wanafanya mazoezi kwa ajili ya mashindano ya ‘Mkali
wa Solo’ yaliyokuwa yakiratibiwa na Juma Mbizo. Wapiga solo wengine walikuwa
Remmy Ongala, Komandoo Hamza Kalala, Michael Bilal, Shaaban Yohana ‘Wanted’ na
wengineo.
Mzee
Mapili alianza muziki kabla hata Tanganyika haijapata uhuru na alikuwa na
mwingi wa vipaji kuanzia kutunga, kuimba na kupiga gitaa.
Alizaliwa
katika Kijiji cha Lipuyu kilichopo Tarafa ya Lionya, Wilaya Nachingwea mkoani Lindi
mwaka 1937 ambako alipata elimu ya msingi sambamba na ya Qur’an.
Ni
wakati akiwa madrasa ndipo alipoibuka kuwa mahiri wa kughani kaswida katika Madrasa
yake na ndiko alikoyapata mapenzi ya kuimba.
Jina
lake lilianza kutajwa Zaidi kwenye ulimwengu wa muziki mara tu alipojiunga na
bendi ya White Jazz iliyokuwa mjini Lindi mwaka 1958 chini ya uongozi wa Hamisi Seif Mayocha. Muda mfupi
baadaye sifa zake zikazagaa sehemu mbalimbali hadi mikoa ya jirani. Mwaka 1959
akajiunga na bendi ya Mtwara Jazz wakati huo.
Ushindani
wa bendi katika kumuwania mwanamuziki huyo ulikuwa mkubwa, kwani bendi ya
Holulu ya mjini Mtwara, nayo ikaona ni bora inyakue ‘kifaa’ hicho. Mapili
akashawishika na maslahi aliyoahidiwa, akajiunga nayo mwaka 1962.
Wakati
huo tayari Tanganyika ilikuwa imepata uhuru, hivyo chama tawala cha TANU
kikaanzisha vikundi vya vijana ili kukitangaza zaidi. Mwaka 1963 Mzee Mapili
akachukuliwa na bendi ya Jamhuri Jazz ya mjini Lindi iliyokuwa inamilikiwa na
Umoja wa Vijana wa TANU (TANU Youth League -TYL).
Kazi
nzuri aliyoifanya kwenye bendi ya Jamhuri ikawashawishi viongozi wa TYL
wamechukue akaasisi bendi nyingine ya vijana huko Tunduru mkoani Ruvuma mwaka 1964.
Lakini mwaka 1965 maslahi yakampeleka kwenye bendi ya Luck Star iliyokuwa
na maskani yake Kilwa Masoko mkoani Lindi. Hakudumu na bendi hiyo, miezi
michache baadaye akanyakuliwa na Kilwa Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Ahmed
Kipande ambako aliibuka na nyimbo kama ‘Ewe Mola Tunakuomba Ubariki Afrika’, ‘Dunia Kukaa Wawili Wawili’,
‘Dolie Mimi Nakwambia’, ‘Sikutegemea’ na ‘Yatanikabili’.
Jeshi
la Kujenga Taifa (JKT) lilianzisha bendi mbili za muziki wa dansi za JKT Mgulani
‘Kimbunga Stereo’ na JKT Mafinga ‘Kimulimuli Jazz’. Kutokana na sifa za Mzee
Mapili kuenea sana, JKT wakamchukua kuwa muasisi wa bendi ya JKT Mgulani,
jijini Dar es Salaam mwaka huo wa 1965 akiwa na akina Athumani Omari, Msenda Saidi, Vinyama Kiss
Rajabu.
Ushindani wa bendi katika Majeshi, ukaanza. Jeshi la Polisi nalo
likamhitaji ajiunge nalo. Alikubali kwenda kuasisi bendi yao ya Polisi Jazz ‘Wana
Vangavanga’ baada ya kupata ajira rasmi Desemba 15, 1965 na kupewa namba ya kazi B 3710 ambako alikuwa na
akina Ali Omari Kayanda, Kassim Mponda, Manzi Matumla, Abdu Ali Mwalugembe,
Plimo Gandam, Bosco Mfundiri, Juma Ubao na Kitwana Majaliwa. Polisi Jazz ilikuwa
ikipiga muziki wake katika ukumbi wa Polisi Barracks, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya nyimbo
alizotunga akiwa na Polisi Jazz ni pamoja na ‘Dunia ni Watu’, ‘Kashinagali
Ugupina’, ‘Lijelalwa Ngwamba’, ‘Ashijajani Mweshimajani Mwe’ na ‘Nataka Uoe Mke
Uwe Mume wa Nyumbani’.
Wakati
akiwa ndani ya Jeshi la Polisi, Mzee Mapili aliteuliwa kufundisha bendi ya Wanawake
iliyojulikana kama Woman Jazz Band Desemba 23, 1965. Bendi hiyo ilikuwa inamilikiwa
na TYL ambapo alisafiri nayo kwenda Kenya, kwenye sherehe za siku ya Kenyatta (Kenyatta
Day). Jomo Kenyatta ndiye alikuwa rais wa kwanza wa Kenya.
Mei
1966 Mzee Mapili alipata pigo baada ya kuondokewa na baba yake mzazi Mzee Said
Amri Makolela, aliyeuawa wakati akipambana na Nyati porini.
Kuvunjika
kwa bendi ya Woman Jazz mwaka 1974, ndio
ulikuwa mwanzo wa kuanzishwa kwa Vijana Jazz
baada ya kuwakusanya vijana wa wakati huo akina Hemed Maneti (Kilosa
Jazz), Hassan Dalali (Mwenyekiti wa
zamani wa Simba), Manitu Mussa, ‘Komandoo’ Hamza Kalala Chakupele, Abdallah Kwesa, Agrey Ndumbaro na wengineo.
Kassim
Mapili alistaafu Jeshi la Polisi Mei 5, 1981 akiwa na cheo cha Sajini na mara
baada ya kustaafu akajiunga na bendi ya Tanzania Stars Ushirika Jazz iliyokuwa
inamilikiwa na Muungano wa Vyama vya Ushirika Tanzania (CUT).
Baada ya kuingia uraiani
ndipo alianza kuongoza vyama mbalimbali vya muziki nchini ambapo baada ya
kuhudhuria semina ya Baraza la Muziki Tanzania (Bamuta) mwaka 1982 alichaguliwa
kuwa mwenyekiti wa mpito wa chama kipya kilichoanzishwa yaani Chama cha Muziki
wa Dansi Tanzania (Chamudata) kabla ya kuchaguliwa na kuwa mwenyekiti wake wa
kwanza mwaka 1984.
Chini ya uongozi wake
ndipo walikusanywa wanamuziki 57 kuunda bendi ya Tanzania All Stars mwaka 1986
ambao walitunda nyimbo zilizokuwa na mafanikio ya kisiasa siyo tu Tanzania bali
hata Afrika kwa ujumla. Wanamuziki hao walitunga nyimbo kama ‘Hayati Samora
Machel’, ‘Azimio la Arusha’ wimbo uliokuja kujulikana nchini Tanzania kama
fagio la chuma uliokuwa ukimsifu Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi
ukiwaonya wazembe kwamba wangepitiwa na ‘fagio la chuma’.
Kila
panapofanyika jambo la manufaa katika muziki hapa nchini, Mzee Mapili amekuwa
akishirikishwa kikamilifu. Amekuwa akitoa michango ya mawazo yenye busara
katika tasnia ya muziki kwa nyakati tofauti.
Kwa
ujumla historia ya mwanamuziki huyo aliyeitwa mbele za haki ni ndefu, akiwa
ameshiriki kuanzishwa kwa bendi kadhaa ikiwemo Shikamoo Jazz inayoongozwa na
Salum Zahoro.
Mwenyezi
Mungu ailaze roho yake mahai pema peponi. AMINA.
CREDIT SOURCE: FIKRA PEVU
No comments:
Post a Comment