Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) limepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa kifo cha
Msanii Mkongwe wa muziki wa dansi Kassim Mapili kilichotokea katikati ya wiki
hii nyumbani kwake Tabata jijini Dar es Salaam.
Kassim
Mapili ni msanii na mdau wa muda mrefu wa sekta ya Sanaa nchini. Amekuwa ni taa
na nuru ambayo katika kipindi chote cha uhai wake imeangaza na kutoa mwanga
angavu kwenye sekta ya Sanaa.
Mchango
wake katika muziki wa dansi na ule wa kiweledi katika kuandaa na kukuza bendi
na wasanii mbalimbali wa muziki wa dansi nchini hautasahaulika kamwe. Ni Msanii
aliyeacha alama kuu katika muziki wa bendi na amejitolea kwa kiasi kikubwa
katika kuufikisha muziki wa dansi ulipo leo.
Aidha,
pamoja na kuwa mwimbaji na mpigaji gitaa katika Bendi mbalimbali zikiwemo za
Kilwa Jazz, Polisi Jazz, Vijana Jazz na nyingine nyingi Mzee Kassim Mapili
alikuwa mstari wa mbele kujenga mfumo wa Utawala kwenye sekta ya Sanaa na
kuhakikisha wasanii wa muziki wa dansi wanakuwa na chombo cha kuwawakilisha na
kutetea maslahi yao.
Mwaka
1982 alikuwa miongoni mwa wasanii waliokutana Mjini Bagamoyo na kuunda Chama
cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA) ambacho hadi leo kinatetea na
kuwawakilisha wasanii wa muziki wa dansi.
Aidha,
Mzee Mapili amekuwa bega kwa bega na Baraza la Sanaa la Taifa katika programu
zake mbalimbali na utendaji kazi wa kila siku. Kwa mfano; amekuwa mmoja wa
wadau ambao wamekuwa wakishiriki kikamilifu kwenye Programu ya Jukwaa la Sanaa
inayoandaliwa na BASATA kwa kushirikiana na chama cha waandishi wa habari za
Sanaa na Utamaduni.
Baraza,
wasanii na wadau wote wa Sanaa hatuna budi kuendelea kuenzi mema yote
aliyotuachia marehemu Kassim Mapili hasa katika kutunga nyimbo za hamasa na
ujumbe makini na wenye mashiko kwa jamii yote ya Watanzania.
Hakika
pengo lililoachwa na Marehemu haliwezi kuzibika, kwani imekuwa ni kama mshumaa
uliyozimika ghafla wakati tukiingia kwenye giza.
Baraza
linatoa pole kwa familia ya Marehemu, chama cha muziki wa dansi, shirikisho la
muziki na wasanii wote kwa ujumla. Ni matumaini ya Baraza kwamba, tutaendelea
kuenzi mema yote yaliyotendwa na Marehemu, hasa kudumisha upendo na amani
katika tasnia yetu ya Sanaa na taifa kwa ujumla.
Bwana ametoa na Bwana
ametwaa, Amen
Godfrey Mngereza
KATIBU
MTENDAJI
No comments:
Post a Comment