Simon Mwakifwamba
Na Shamimu Nyaki-Maelezo.
Kufuatia uchaguzi uliofanyika jana jijini Dar es Salaam wa kutafuta viongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) viongozi wapya wamepatikana ambao ni Rais, Makamu wa Rais, pamoja na Wajumbe kumi wa Bodi watakaongoza Shirikisho hilo kwa kipindi cha miaka minne.Akisoma matokeo ya uchaguzi huo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Filamu Tanzania Bw. Nico Mathew amesema kuwa, idadi ya wajumbe waliojiandikisha kupiga kura ilikuwa ni 69 lakini waliopiga kura ni 52 ambapo Bw. Simon Mwakifwamba aliekuwa anagombea nafasi ya Urais kwa awamu ya pili alipata kura 47 kati ya 52 zilizopigwa na wanachama wa vyama mbalimbali vya tasnia hiyo na Makamu wake Bw. Deo Sanga alipata kura 49 kati ya 52.
Wajumbe wa Bodi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Adam Juma Mikidadi, John Kalaghe, Irene Sanga, Juma Issa, Michael Sangu, Single Mtambalike, Hussein Athumani, Ummi Mohamed, Nazir Masila pamoja na Alli Mohamed.
Akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo Rais Mteule Bw. Simon Mwakifwamba ameahidi kuendelea kukuza tasnia ya filamu nchini kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali na wadau wa Filamu ili kuweza kuvuka mipaka ya ndani ya nchi kwa manufaa ya wasanii na Taifa.
“Asanteni sana kwa kuniamini tena kwa awamu nyingine naahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na nyie kwa weledi, ubora na uhitaji ili tufanikiwe zaidi”, alisema Mwakifwamba.
Ameongeza kuwa katika awamu hii ya miaka minne ameandaa vipaumbele vitano ambavyo ni Kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha Sera ya Filamu inapatikana, kupata elimu kuhusu tasnia kwa wasanii, kuanzisha mfuko wa maendeleo ya Filamu, na usambazaji bora wa Filamu hapa nchini ili wasanii wanufaike na kazi zao.
Uchaguzi wa shirikisho hilo umefanyika kutokana na viongozi waliokuwepo kumaliza muda wao kwa mujibu wa Katiba ya Shirikisho hilo ambapo viongozi waliopatikana wameahidi kuleta mabadiliko chanya katika tasnia ya Filamu nchini.
No comments:
Post a Comment