Na Daniel Mbega
WAKATI
ambapo Yanga ya Tanzania na Vital’O ya Burundi zinacheza nyumbani Jumamosi hii
Februari 27, 2016 zikihitaji sare tu kutokana na ushindi katika mechi zao za
kwanza za Ligi ya Mabingwa Afrika, klabu za APR ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya
na Mafunzo ya Zanzibar ziko katika wakati mgumu.
Gor Mahia
ilikubali kipigo cha nyumbani Nairobi cha mabao 2-1 kutoka kwa CNaPS Sports ya
Madagascar katika mechi ya kwanza ya raundi ya awali, na sasa inahitaji miujiza
ili isonge mbele wakati zitakaporudiana mjini Antananarivo.
Mafunzo
yenyewe ina wakati mgumu Zaidi wa kuvuka mbele ya AS Vita Club baada ya kipigo
cha mabao 3-0 mjini Unguja na kuwang’oa wakongwe hao wa soka Afrika ni sawa na
kupanda mlima Kilimanjaro wakikimbia.
Yanga wao
wanacheza nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam dhidi ya Cercle
de Joachim wakijivunia ushindi wao wa bao 1-0 mjini Curepipe, lakini kama
hawatakuwa makini, wanaweza kuadhiriwa na mabingwa hao wa Mauritius.
Mabingwa hao
wa Tanzania Bara watawakosa wachezaji kadhaa mahiri akiwemo mfungaji wa bao
hilo pekee Mzimbabwe Donald Ngoma ambaye yuko Harare kwenda kumzika mdogo wake
aliyefariki kwa ajali ya gari.
Vital’O
watakuwa mjini Bujumbura kuwakaribisha Lioli ya Lesotho wakijivunia ushindi wao
wa ugenini wa mabao 2-1 ambapo sare yoyote itawavusha kwenda hatua inayofuata.
Mabingwa wa
Rwanda, maafande wa APR walilazwa kwa bao 1-0 na wenyeji Mbambane Swallows
nchini Swaziland, kwa hiyo kesho wanahitaji kushinda kwa Zaidi ya bao moja na
wasiruhusu bao ili waweze kusonga mbele.
Nao mabingwa
wa Uganda, Bunamwaya au Vipers, licha ya kushinda bao 1-0 jijini Kampala,
watakuwa na wakati mgumu mbele ya Enyimba ya Nigeria watakaporudiana kesho
mjini Aba.
Kama hakutakuwa
na namna ya jitihada, kuna uwezekano mkubwa wa Afrika Mashariki kupoteza timu
zaidi ya tatu ambazo hazitafuzu kwa raundi ya kwanza ya mashindano hayo.
Wakati
ambapo Ferroviario de Maputo ya Msumbiji imefuzu moja kwa moja raundi ya kwanza
baada ya wapinzani wao Centre Chiefs ya Botswana kujitoa, mechi nyingine za
Ligi ya Mabingwa Afrika wiki hii zinaonyesha kwamba, Warri ya Nigeria itakuwa
na kazi ndogo dhidi ya Praia Cruz ya Sao Tome & Princepe kutokana na
ushindi wake wa mabao 3-0 ugenini.
Aidha, Wydad
Casablanca ya Morocco inatakiwa kulinda ushindi wake wa mabao 2-0 ilioupata
nyumbani wiki mbili zilizopita dhidi ya Douanes Niamey ya Niger huku wakongwe
Union Douala kutoka Cameroon wakiwa nyumbani kwao mjini Douala watahitaji sare
tu kusonga mbele dhidi ya Nimba ya Liberia kwani katika mechi ya kwanza
Wacameroon hao walishinda 3-1 mjini Monrovia.
Al Ahly
Tripoli ya Libya inajivunia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Once Createurs
(Viumbe 11) ya Mali na zitakaporudiana katika uwanja huru Walibya watakuwa
wanataka kulinda ushindi wao ili wasonge mbele. Mechi yao ilichezwa jana Ijumaa, Februari 26, 2016.
Klabu kongwe
ya Ghana, Ashanti, iko ugenini wikiendi hii kukabiliana na MO Bejaia ya Algeria
na licha ya ushindi wao wa bao 1-0 ilioupata wiki mbili zilizopita, bado ina
kibarua kigumu dhidi ya Waarabu hao.
Asec Mimoas
wako nyumbani Abidjan kuwakabili Cotton Tchad ya Chad wakiwa na ushindi wa bao
1-0 katika mechi yao ya kwanza, lakini hilo haliwapia nafasi ya kutosha
kujihakikishia kusonga mbele kwenye mashindano hayo makubwa kabisa ya klabu
barani Afrika.
Tanda ya
Ivory Coast nayo iko nyumbani na leo hii Ijumaa inarudiana na Club Africain ya
Tunisia. Katika mechi ya kwanza, Tanda ilifungwa 2-0 ugenini.
St. Georges
ya Ethiopia iliyopata ushindi wa mabao 3-0, sasa itakuwa ugenini kuwakabili St.
Michel United ya Shelisheli wakati Zesco ya Zambia Ijumaa Februari 26, 2016
inacheza mjini Juba na wenyeji Al-Ghazal ya Sudan Kusini huku ikitambia ushindi
wake wa mabao 2-0.
Volcan Club ya
Comoro inakwenda kukamilisha ratiba mjini Johannesburg baada ya kukubali kipigo
cha mabao 4-0 nyumbani dhidi ya Kaizer Chiefs wakati Douanes ya Senegal itakuwa
na kazi ngumu ugenini mjini Conakry, Guinea dhidi ya Horoya baada ya miamba
hiyo kutoka sare tasa wiki mbili zilizopita.
Bobo-Dioulasso
watakuwa nyumbani Burkina Faso kukabiliana na Stade Malien ya Mali ambapo licha
ya kufungwa 3-1, wanajivunia bao lao la ugenini na hivyo wanahitaji ushindi wa
mabao 2-0 tu wasonge mbele.
Kazi ni
ngumu kwa Mangasport ya Gabon itakayokuwa ugenini huko Brazzaville kuwakabili Etoile
du Congo baada ya kutoka suluhu mechi ya kwanza, lakini kwa klabu ya CRD Libolo
ya Angola, kazi yao itakuwa rahisi dhidi ya Micomeseng ya Guinea ya Ikweta
mjini Malabo kufuatia ushindi wao wamabao 5-1.
Chicken Inn ya
Zimbabwe ilishinda 1-0 dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, lakini
inahitaji kukaza msuli kuitoa timu hiyo ngumu ya Afrika Kusini ambayo itakuwa
na faida ya kucheza nyumbani, kama ilivyo kwa Olympique Khouribga ya Morocco
inayocheza na Gamtel ya Gambia. Olympique ilishinda 2-1 mchezo wa kwanza.
Katika Kombe
la Shirikisho, hali ni ngumu kwa Bandari ya Kenya, Atletico Olympic ya Burundi
n ahata SC Villa ya Uganda licha ya timu hiyo kushinda bao 1-0 ugenini wiki
mbili zilizopita.
Villa
itakuwa nyumbani kucheza na al-Khartoum ya Sudan, wakati Bandari iliyokubali
kipigo cha mabao 2-0, sasa itahitaji kuifunga mabao mengi St. Eloi Lupopo ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Atletico
Olympic ya Burundi ilipigwa bao 1-0 na Fomboni ya Comoro mjini Moroni, lakini
sasa inapocheza nyumbani inahitaji ushindi ili isonge mbele.
Polisi ya
Rwanda ndiyo iko kwenye nafasi nzuri ya kuvuka dhidi ya Atlabara ya Sudan
Kusini kufuatia ushindi wake wa mabao 3-1. Timu hizo zitacheza mjini Juba.
Kawkab
Marrakech ya Morocco itakuwa ugenini kwa USFA ya Burkina Faso, lakini ushindi
wake wa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza unawaweka kwenye nafasi nzuri ya
kusonga mbele ikiwa hawatafanya mzaha kwenye mechi hiyo ya marudiano.
Mechi
nyingine zinaonyesha kwamba Nasarawa ya Nigeria itakumbana na Generation
ugenini huko Senegal. Katika mechi ya kwanza Nasarawa ilishinda 2-1.
Africa
Sports ya Ivory Coast, ikichagizwa na ushindi wake wa ugenini wa mabao 2-1,
itaikaribisha Diables Noirs ya Congo, wakati USFAS Bamako ya Mali itakuwa inagangamala
kutafuta ushindi wa nyumbani dhidi ya Sporting Gagnoa ya Ivory Coast baada ya
kufungwa 2-0.
USM de Loum
ya Cameroon na Deportivo Mongomo ya Guinea ya Ikweta zina kibarua kigumu baada
ya kutoka sare tasa katika mechi ya kwanza, wakati Vita Club Mokanda ya Congo
Brazzaville inahitaji miujiza ugenini kwa Akwa ya Nigeria baada ya kuruhusu
kipigo cha bao 1-0 katika mechi ya kwanza.
Renaissance ya
Chad iko ugenini kwa New Star ya Cameroon, lakini inajivunia ushindi wake wa
bao 1-0, wakati Ajax Cape Town itakuwa nyumbani kucheza na Sagrada ya Angola
huku ikiwa na ushindi wa mabao 2-1 wa ugenini.
Defence ya
Ethiopia iliruhusu kufungwa nyumbani mabao 3-1 na Misr Elmaqasah, sasa
inahitaji nguvu za ziada kushinda ugenini huku Harare City ikihitaji sare
ugenini kwa Adema ya Magadascar kufuatia ushindi wake wa mabao 3-2. Ikizembea
tu na jamaa wakapata bao moja, basi itakuwa imetolewa.
Kazi
inaonekana kuwa mteremko kwa Bidvest Wits ya Afrika Kusini inayocheza nyumbani
dhidi ya Lightstars ya Shelisheli, kwani katika mechi ya kwanza Wasauzi hao
walishinda mabao 3-0 ugenini.
CREDIT SOURCE: FIKRA PEVU
No comments:
Post a Comment