Mgeni Rasmi Mkuu
wa Kitengo cha Uratibu wa Misaada ya Maendeleo na Mashirikiano ya Kimataifa
ambaye pia ni Mchumi Mkuu Bi. Magret Ndaba akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano
wa wadau wa sekta ya mbolea nchini kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya
Kilimo, Chakula na Ushirika Bibi Sophia Kaduma leo jijini Dar es salaam.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa wadau wa sekta ya mbolea nchini wakifuatilia
mkutano wa wadau hao ulifanyika leo jiji Dar es Salaam.
Mgeni Rasmi Mkuu wa
Kitengo cha Uratibu wa Misaada ya Maendeleo na Mashirikiano ya Kimataifa ambaye
pia ni Mchumi Mkuu Bi. Magret Ndaba akiwawa katika picha ya pamoja na washiriki
wa mkutano wa wadau wa sekta ya mbolea nchini mara baada ya ufunguzi wa mkutano
huo leo jijini Dar es salaam.
(Picha na Eleuteri
Mangi- MAELEZO)
Na Eleuteri
Mangi-MAELEZO
8/9/2015.
Wadau wa sekta ya
mbolea nchini wameaswa kujadiliana kwa kina changamoto zinazoikumba sekta hiyo na
kuzipatia ufumbuzi ili kuinua sekta ya kilimo iwe na tija katika uzalishaji wa
mazao mbalimbali nchini.
Kauli hiyo imetolewa na
Mkuu wa Kitengo cha Uratibu wa Misaada ya Maendeleo na Mashirikiano ya
Kimataifa ambaye pia ni Mchumi Mkuu Bi. Magret Ndaba wakati wa ufunguzi wa
mkutano wa wadau wa sekta ya mbolea nchini kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika Bibi Sophia Kaduma leo jijini Dar es salaam.
“Unajua mbolea kazi yake ni kurutubisha
udongo, ni vema iwafikie wakulima ambao ni walengwa kwa wakati na kwa bei
nafuu” alisema Bi. Magret.
Bi. Magret alisema kuwa
washiriki wa mkutano huo wajikite kujadili vitu vinavyokinza utumiaji wa mbolea
kumfikia mkulima waviibue na wajadili kwa pamoja kwa kushirikiana Serikali na
sekta binafsi lengo likiwa ni mbolea kuwafikia wakulima kwa wakati na kwa bei
nafuu ili kilimo kiwe cha tija kwa wakulima na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na masuala ya
mbolea (AFAP) Dkt. Andrew Msolla alisema kuwa mkutano huo ni wa kwanza
kufanyika hapa nchini kwa kuwashirikisha wadau wa sekta hiyo ya mbolea.
Dkt. Msolla alisema
kuwa Azimio la Abuja nchini Nigeria lililowekwa mwaka 2006 lilizitaka nchi zote
za Afrika kuzingatia matumizi sahihi ya mbolea kwa hekta ambapo inatakiwa kuwa
ni kilogram 50 kwa hekta moja.
“Mwaka 2006 matumizi ya
mbolea kwa nchi za Afrika yalikuwa ni kilogram 8 kwa hekta ambapo hadi sasa Tanzania
inatumia kilogram 19.6 ambazo ni chini ya makubaliano ndiyo maana hasa ya
mkutano wetu wa leo” alisema Dkt. Msolla.
Naye Mkuu wa Shirikisho
la Mapinduzi ya Kijani katika Kilimo Afrika (AGRA) nchini Tanzania Dkt. Mary
Mgonja alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi sita za kipaumbele katika
mapinduzi ya kijani kati ya 17 za Afrika zilizo katika shirikisho hilo.
Kwa mujibu wa Dkt.
Mary, nchi nyingine za kipaumbele katika shirikisho hilo ni Msumbiji, Ethiopia,
kwa ukanda wa Afrika ya Mashariki pamoja na Ghana, Burkina Faso na Mali kwa
ukanda wa Afrika ya Magharibi.
Akichanganua changamoto
zinazoikabili sekta ya mbolea nchini, Meneja Mkuu wa Chama cha Makampuni
yanayoingiza mbolea nchini Bw. Salum Mkumba alisema kuwa zipo changamoto kuu
sita zinazoikabili sekta hiyo nchini.
Changamoto hizo ni
uwepo wa taasisi nyingi za udhibiti wa mbolea, namna ya usajili wa mbolea
ambapo ili isajiliwe ni lazima ifanyiwe majaribio kwa muda wa miaka mitatu,
mfumo wa ruzuku ya mbolea ambao hubadilika mara kwa mara na kuathiri wakulima,
suala la namna ya kusafirisha mbolea ambapo hutumika magari badala ya reli
pamoja na mikopo kwa wakulima yenye riba kubwa.
Bw. Salum Mkumba
alisema kuwa mkutano huo umeazimia kutatua changamoto hizo zinazoikabili sekta
ya mbolea kwa kushirikisha sekta binafsi na Serikali kwa kuweka sheria, kanuni
na taratibu ambazo zitamsaidia mkulima mdogo na hatimaye kuwa na tija kwa mtu
mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Mkutano huo wa siku moja ulikuwa na washiriki
zaidi ya 70 kutoka sehemu mbalimbali nchini ukijumuisha wahadhiri kutoka Chuo Kikuu
cha Kilimo cha Sokoine kilichopo Mkoani Morogoro na Chuo Kikuu cha Dar es
salaam, sekta binafsi zinazoshughulika na masuala ya mbolea, wahisani na wadau
wa maendeleo kutoka nchi mbalimbali pamoja na wakulima.
No comments:
Post a Comment