Vijana wanalipwa kukata miti hiyo na kuisafirisha hadi kiwandani
Katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi iliyopita, jamii ya Njemps iliyoko kaunti ya Baringo nchini Kenya imekuwa ikifuatilia kwa makini kesi iliyowasilisha mahakamani dhidi ya serikali.
Jamii hiyo ilikuwa imeishitaki serikali kwa kuanzisha upanzi wa mti unaojulikana kama Proposis Juliflora au Mathenge.
Wawakilishi wa jamii hiyo hata waliwasilisha mbuzi mahakamani kudhihirisha athari za mmea huo, sio tu kwa ardhi yao bali hata kwa mifugo.
Wakazi walikuwa wanadungwa na miiba ya mmea huyo nao mbuzi kuharibiwa meno. Vidonda vya miiba ya mmea huyo huchukua muda mrefu kupona.
Lakini sasa hali ni tofauti, jamii hii inapata fedha nyingi baada ya mradi wa kuzalisha nishati ya umeme kwa kutumia mti wa Mathenge kuanzishwa mjini Marigat.
Mmea huo ulikuwa umepandwa maeneo hayo na serikali ili, kuzuia mmonyoko wa udongo.
Mwandishi wa BBC Robert Kiptoo aliyezuru eneo la Loboi, karibu na Ziwa Bogoria anasema kwa muda mrefu, mmea wa Mathenge umekuwa ukiliwa na mifugo, kutokana na kiangazi.
Lakini baada ya muda athari zake kuanza kujitokeza, uligeuka kuwa adui hadi sasa ambapo sasa mtazamo wao umebadilika baada ya kuanza kupata manufaa kutoka kwa mmea huo.
Vijana sasa wamepata ajira baada ya kampuni ya Cummins Cogeneration kuanzisha kiwanda cha kuzalisha umeme kwa kutumia mmea huo karibu na mji wa Marigat.
“Miti kama hii hapa imelala hapa ndiyo wakulima wamekata. Sisi vijana tumepata kazi nzuri sana.Tunaajiri kama vijana kumi na kwa kila siku tunalipa kila mtu Sh400,” anasema McCathy Kunjali, mwekahazina wa kundi moja la vijana.
Bi Jamima Jerop, mhandishi mkuu katika kiwanda cha Cummins anasema: “Kuwepo kwa kiwanda hiki kutafaa sana. Wananchi watapata kazi mbalimbali. Wakulima wanaouza miti pia watapata pesa na kujikimu kimaisha,”
Mfumo huo wa kutumia miti kuzalisha umeme ndio ya kwanza barani na endapo mradi huu utafanikiwa kwa kiasi cha juu, basi matatizo ya upungufu wa umeme nchini Kenya huenda yakapungua.
CREDIT: BBC
No comments:
Post a Comment