Umaskini wa kutisha umepungua kiasi kwani jamii nyingi kama Wamasai nao wanashiriki kilimo. (Picha hii ni kwa hisani ya Umaskini Tanzania Blog).
Watoto wengi wameandikishwa, lakini changamoto ya vyumba vya madarasa, madawati, vitabu na nyumba za walimu inakwamisha ubora wa elimu.
Afya ya uzazi ina changamoto kubwa, akinamama wanalazimika kulala chini ama kuchangia kitanda kimoja wagonjwa watatu.
Huduma ya maji nayo bado ina changamoto.
Na Daniel Mbega
KUANZIA leo Septemba 25 hadi 27, wakuu wa nchi 193 wanachama
wa Umoja wa Mataifa wanakutana jijini New York, Marekani katika mkutano muhimu
uliobatizwa jina la Agenda kwa Maendeleo Endelevu kuelekea mwaka 2030 (2030 Agenda for Sustainable
Development).
Katika mkutano huo, nchi
wanachama wa watapitisha Agenda kwa Maendeleo Endelevu 2030, ambayo inahusisha jumla
ya Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu (SDG) ambayo ni kukomesha umaskini,
kuhamasisha usawa na kupinga uonevu, na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi
kufikia mwaka 2030.
Malengo
haya Endelevu, ambayo pia yanafahamika kama Malengo ya Ulimwengu, yamejikita
katika Malengo nane ya Maendeleo Milenia (MDG) katika kupambana na umaskini ambayo
ulimwengu uliazimia kutafikia kwa mwaka 2015.
Malengo ya
Milenia ambayo yalipitishwa Septemba 2000, yalilenga katika kupunguza umaskini,
njaa, maradhi, uwiano wa kijinsia, na upatikanaji wa maji safi na salama.
Mafanikio
makubwa yamepatikana kupitia MDG, na kuonyesha umuhimu wa kunganisha agenda
hizo baina ya malengo na matarajio, na ingawa yamesaidia kuwainua mamilioni ya
wananchi kote ulimwenguni kutoka kwenye lindi la umaskini na kuwapatia unafuu,
lakini bado kuna umuhimu wa kwenda mbele zaidi.
Tanzania
inaelezwa kwamba ni moja ya nchi zilizofanya vizuri katika Malengo ya Maendeleo
ya Milenia hata kabla ya mwaka 2015 ingawa bado inakabiliwa na changamoto
katika baadhi ya maeneo kupitia kwenye program mbalimbali kama
MKUKUTA, MKURABITA, uwezeshaji wa mikopo kwenye SACCOS, mipango ya elimu kama MMEM,
MMES na MEMKWA, na huduma za kijamii kama Bima ya Afya, Sera ya Hifadhi Jamii,
Miradi ya maji kwa kuzingatia pia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2000-2025.
Katika kupunguza
umaskini, Tanzania imefanikiwa kwa takriban asilimia 19.5 na katika kupunguza
idadi ya watoto chini ya miaka mitano wenye uzito mdogo imefanikiwa kwa
asilimia 14.4 tu, hivyo juhudi zaidi zinatakiwa wakati wakuu watakaporidhia
malengo mapya.
Baadhi ya
malengo ambayo Tanzania imefanya vizuri ni pamoja na lengo namba mbili linalohusu fursa ya elimu ya
msingi kwa watoto wote, ambapo Ripoti ya Malengo ya Milenia inaeleza kwamba,
lengo hilo limefanikiwa kutoka asilimia 54.2 mwaka 1990 hadi 89.71 mwaka 2013.
Lengo la
tatu ni kuondoa utofauti wa jinsia katika elimu ya msingi na sekondari ifikapo
2025 na kwa ngazi zote za elimu ifikapo 2015, nalo limefanikiwa kwa elimu ya
msingi kufikia asilimia 98 mwaka 2010 na asilimia 102 mwaka 2013 na elimu ya
sekondari asilimia 105 mwaka 2013.
Wanawake wameendelea
kupata fursa sawa za kijinsia na kuwezeshwa, ambapo kuna ongezeko la wanawake
katika vyombo vya utoaji maamuzi kama vile Bunge na Baraza la Wawakilishi,
kwani kwa mara ya kwanza Bunge la 10 limeongozwa na mwanamke – kwanza akiwa
Naibu Spika kwa miaka mitano na baadaye akiwa Spika kamili, na sasa kama Chama
cha Mapinduzi kitafanikiwa kuingia madarakani, Tanzania itaweka rekodi mpya kwa
kuwa na Makamu wa Rais mwanamke kwa mara ya kwanza.
Kumekuwa
na mafanikio ya kuridhisha katika upunguzaji wa vifo vya watoto wachanga chini
ya miaka mitano kwa pande zote mbili za Muungano, ingawa bado watoto
wanaendelea kupoteza maisha kwa maradhi yanazulikia kama vile malaria na kuharisha.
Kwa upane
mwingine, lengo namba tano kuhusu upunguzaji wa vifo vya wanawake wajawazito bado
lina changamoto nyingi zinazochangiwa na uhaba wa wataalamu na ukosefu wa wa huduma za upasuaji
wa dharura, japokuwa serikali imejitahidi kulifanyia kazi kwa kuviwezesha vituo
vya afya kuvipatia vifaa na wataalam.
Kuhusu
lengo la sita linalohusu huduma za afya, bado kuna changamoto nyingi hasa katika
kukabiliana na maambukizi ya virusi vinavyosambabisha ugonjwa wa ukimwi,
malaria na kifua kikuu, magonjwa ambayo yanagusa sehemu kubwa ya jamii,
mafanikio hapa ni asilimia 6.9 tu.
Malengo haya
mapya yamejikita katika kutokomeza umaskini katika namna zake zote kila mahali
duniani licha ya idadi ya watu wanaoishi katika umaskini wa kutupwa kupungua
kwa zaidi ya nusu – kutoka watu 1.9 bilioni mwaka 1990 hadi watu 836 milioni
mwaka 2015, kwani wapo wengi ambao bado wanaendelea kuhangaika kupata huduma za
msingi za kibinadamu.
Ulimwenguni
kote, zaidi ya watu milioni 800 wanaishi kwa kipato cha chini ya Dola 1.25 kwa
siku; wengi wanakosa chakula bora, mai safi na salama. Kukua kwa uchumi kwa
kasi katika nchi kama China na India kumewatoa wengi kwenye umaskini, lakini
maendeleo pia yamekuwa hayana uwiano sawa. Wanawake wana uwezekano wa kuishi
kwenye umaskini mkubwa kuliko wanaume kwa sababu ya kukosa fursa ya kazi yenye
mshahara, elimu na rasilimali.
Mafanikio pia
yamekuwa madogo katika baadhi ya maeneo, kama Asia Kusini na nchi za Kusini mwa
Jangwa la Sahara, ambayo yana asilimia 80 ya idadi ya watu wote ulimwenguni
wanaoishi katika umaskini mkubwa. Idadi hii inategemewa kuongezeka kutokana na
mabadiliko ya hali ya hewa, migogoro na uhaba wa chakula.
Kutokomeza
njaa, kufanikiwa katika usalama wa chakula na kuboresha lishe na kukuza kilimo
endelevu kutasaidia kukuza uchumi na kuongeza tija katika mazao ya kilimo kama
ilivyoonekana katika miongo miwili iliyopita. Nchi nyingi zinazoendelea ambazo
zilikuwa zinakabiliwa na majanga ya njaa sasa zinaweza kujivunia usalama wa
chakula.
Hata hivyo,
zaidi ya watoto milioni 90 walio chini ya miaka mitano bado wako katika hatari
ya uzito mdogo na mtu mmoja kati ya wanne anashinda na kulala na njaa barani
Afrika.
Malengo
Endelevu ya Maendeleo yamejikita katika kuhakikisha aina zote za njaa
zinakomeshwa ifikapo mwaka 2030 na kuhakikisha watu wote hasa watoto wakipata
mlo stahili.
Kwa maana
nyingine, kilimo kinapaswa kuimarishwa na serikali ijayo ya Tanzania ili kiweze
kukidhi matakwa ya malengo haya.
Malengo
mapya pia yameikita kuhakikisha jamii inakuwa na afya bora kwa kuzingatia
kwamba Malengo ya Milenia yamesaidia kupunguza vifo vya watoto, kuboresha afya
ya uzazi na mapambano dhidi ya magonjwa ya Ukimwi, malaria na kifua kikuu kwa
asilimia 30 tangu mwaka 2000.
Baada ya
kufanikiwa kuandikisha watoto wengi shuleni, sasa ni wakati wa kujikita katika
utoaji wa elimu bora. Hiyo ndiyo njia pekee ya kuwapatia unafuu wa maisha
wananchi kimaendeleo badala ya kuwa na bora elimu ambapo watoto wengine
wanaingia sekondari wakiwa hawajui kusoma, kuandika wala kuhesabu.
Lakini pia
serikali kupitia malengo hayo mapya, zitajikita katika kuwawezesha wanawake na
kuhamasisha uwiano wa kijinsia ni muhimu kwa kuchochea maendeleo, hivyo
serikali zote safari hii zitajikita katika kuhakikisha zinakomesha aina zote za
ubaguzi dhidi ya wanawake. Kwa sasa, inaelezwa kwamba wanawake wana asilimia 41
katika ajira za mshahara kulinganisha na asilimia 35 mwaka 1990. Bado kuna
changamoto katika utumikishwaji wa wanawake katika maeneo mengi.
Uhaba wa
maji unawaathiri asilimia 40 ya watu ulimwenguni kote, idadi kubwa ambayo inaweza
kuongezeka kutokana na ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi. Japokuwa
watu bilioni 2.1 wamepata maji tangu mwaka 1990, lakini changamoto ya
upatikanaji wake bado ni kubwa katika maeneo mengi ulimwenguni.
Mnamo mwaka
2011, nchi 41 zilikubwa na uhaba mkubwa wa maji; kumi kati ya hizo zinakaribia
kukausha hata vyanzo vyake na sasa zinategemea vyanzo visivyo rasmi. Serikali zote
ulimwenguni sasa zinatakiwa kubuni mbinu ambazo zitasaidia upatikanaji wa maji
safi na salama.
Suala na
nishati limepewa kipaumbele katika malengo mapya ya maendeleo ambapo serikali
zote zinapaswa kuhakikisha nishati ya gharama nafuu, ya uhakika, endelevu na ya
kisasa inapatikana kwa wote. Kati ya mwaka 1990 na 2010, idadi ya watu
wanaotumia umeme meongezeka hadi kufikia bilioni 1.7, lakini kwa kadiri idadi
ya watu inavyoongezeka duniani, mahitaji nayo yatakuwa makubwa.
Tanzania bado
inaendelea kuhangaikia kuhakikisha nishati ya umeme wa uhakika inapatikana na
kuondokana na mgawo ambao umeathiri uchumi kwa kiasi kikubwa. Hii ndiyo sababu
imetoa kipaumbele katika uzalishaji wa umeme wa gesi, mitambo ambayo tayari
imekwishaunganishwa kwenye gridi ya taifa.
Kwa ujumla,
malengo yote haya 17 yakipewa kipaumbele katika serikali ijayo hapa Tanzania,
kuna uwezekano mkubwa wa kupiga hatua kutoka pale yalipoishia Malengo ya
Milenia na kuleta maendeleo zaidi kwa jamii ya Watanzania kwa kuzingatia pia
Dira ya Taifa ya Maendeleo ya miaka 25 (kutoka mwaka 2000-2025) pamoja na
mikakati mingine ya kupambana na umaskini kama MKUKUTA II na MKURABITA.
Muhtasari:
Malengo ya Maendeleo ya Milenia
(2000-2015)
Mwezi
Septemba 2000, wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa walikutana jijini
New York na kupitisha Azimio la Umoja wa Mataifa la Milenia kwa kupunguza
umaskini uliokithiri baada ya miaka 15.
Malengo nane
yalipitishwa, ambayo ni:
1.
Kupunguza umaskini uliokithiri na njaa
2.
Kuhakikisha upatikanaji wa elimu ya msingi
3.
Kuhamasisha usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake
4.
Kupunguza vifo vya watoto
5.
Kuboresha afya ya uzazi
6.
Kupambana na Ukimwi, malaria na maradhi mengine
7. Kutunza
mazingira
8.
Kuendeleza ushirikiano wa kidunia kwa maendeleo
Malengo Endelevu ya Maendeleo
(2015-2030)
Hii ndiyo
agenda mpya ya maendeleo ya ulimwengu kwa sasa na wakuu wa mataifa zaidi ya 160
wanakutana leo hii kujadili, kupitisha na hatimaye kuridhia malengo hayo.
Paul Ladd,
Mkurugenzi wa Timu ya UNDP kuelekea kwenye Agenda ya Maendeleo 2015, anasema
Agenda hiyo inahusisha Malengo mapya 17 ya Maendeleo Endelevu, ambayo ndiyo
yatakuwa mwongozo kwa sera na ufadhili kwa miaka mingine 15 ijayo, yakianza na
ahadi ya kihistoria ya kutokomeza umaskini kila mahali duniani.
Malengo haya
mapya yanapaswa kumalizika kazi ya Malengo ya Milenia ambayo yameleta mafanikio
katika mataifa mengi duniani, Tanzania ikiwa miongoni mwao.
Malengo haya
mapya ya maendeleo hayajawekwa kwa mataifa maskini na yanayoendelea tu, bali
mataifa yote ulimwenguni, kuhamasisha amani na kushirikisha jamii, kutengeneza
ajira nzuri na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Malengo
hayo mapya ni:
1: Hakuna
umaskini
2: Kutokomeza
njaa
3: Afya
bora na ustawi
4: Elimu
bora
5: Uwiano
wa kijinsia
6: Maji safi
na salama
7: Nishati
rahisi na safi
8: Kazi
nzuri na ukuaji wauchumi
9: Viwanda,
ubunifu, miundombinu
10: Kupunguza
uwiano usio sawa
11: Miji
na jamii endelevu
12: Uwajibikaji
13: Hatua
za kutunza mazingira
14: Maisha
chini ya maji
15: Maisha
katika ardhi
16: Amani,
haki na taasisi imara
17: Ushirikiano
katika malengo
0656-331974
No comments:
Post a Comment