PUBLIC
NOTICE
BASATA
LATAKA KUONDOLEWA/KUSITISHWA MARA MOJA KUCHEZWA KWA NYIMBO ZOTE ZENYE
KUKENGEUKA MAADILI, SHERIA NA TARATIBU
Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) linawaagiza wasanii, wamiliki na waendeshaji wa wavuti, tovuti na
vyombo vya habari hususan radio na runinga kuondoa na kuacha mara moja kurusha
au kutangaza au kucheza nyimbo zote zenye maudhui ya kashfa, matusi, kejeli,
udhalilishaji ambazo zinahatarisha kuigawa jamii ya kitanzania katika misingi
yoyote hasa katika kipindi hiki Taifa linapoendelea na kampeni za kisiasa na
kujiandaa na uchaguzi mkuu.
Kwa mujibu wa kifungu namba
118 (a-d) cha Sheria ya Bunge namba 9 ya Mawasiliano ya Mtandao ya mwaka 2010
ni marufuku kwa njia yoyote kwa mtu au chombo chochote kutengeneza, kuzalisha,
kusambaza au kutangaza ujumbe ambao una mlengo wa matusi, dharau, uzushi au
jinai kwa lengo la kutukana, kutisha, kusumbua au kushusha hadhi ya mtu
mwingine.
Aidha, Sheria ya Bunge
namba 4 ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 kifungu cha 45 (1) (a-c) kinatoa
mamlaka kwa taasisi au mtu yeyote anayebaini uvunjifu wa Sheria katika mitandao
kutoa notisi kwa yeyote yule anayesambaza au kutangaza ujumbe au maudhui
yanayovunja sheria za nchi kuacha mara moja au vinginevyo hatua za kisheria
zitachukuliwa dhidi ya yeyote anayekaidi.
Ni kwa msingi huu, BASATA
linawaagiza wasanii, wamiliki wa wavuti, tovuti na wale wenye akaunti kwenye
mitandao ya kijamii kama sound cloud, U-Tube, ITunes nk. kuondoa ndani ya siku
saba (7) kuanzia siku ya kwanza ya taarifa hii nyimbo zote zinazokengeuka
maadili na kubeba mlengo wa matusi, kashfa, kejeli na udhalilishaji wa watu wa
kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa kisiasa na kitaifa.
Aidha, BASATA
linawakumbusha tena Wasanii wote nchini kuacha mara moja kubuni na kutengeneza
kazi za Sanaa zenye kuashiria kuigawa jamii katika misingi yoyote ya kibaguzi
na zaidi kutumia Sanaa kubomoa jamii badala ya kuijenga.
BASATA linawasisitiza
wamiliki wa vyombo vya habari hususan radio na runinga pia watangazaji na Ma
DJs kuhakikisha hawawi chanzo cha kusambaza maudhui yoyote ya Sanaa yenye
mlengo wa kuibua chuki, matusi, kashfa na mgawanyiko wa Taifa.
BASATA kwa mamlaka yake chini
ya Sheria namba 23 ya mwaka 1984 na yale ya Sheria ya Mawasiliano ya Posta na
Mitandao ya mwaka 2010 na ile ya Makosa ya mitandao ya mwaka 2015 kwa
kushirikiana na vyombo vya dola halitasita kuchukua hatua kali za kisheria na
kinidhamu kwa wasanii, wamiliki wa wavuti, tovuti na vyombo vya habari ambavyo
vitaendelea kutangaza na kusambaza nyimbo zenye mwelekeo wa kuhatarisha
usalama, umoja na mshikamano wa Taifa.
BASATA likiwa ni msimamizi
na mratibu wa sekta ya Sanaa nchini linatambua kwamba Sanaa ikitumiwa kwa
ukengeufu inaweza kuwa chanzo kikuu cha machafuko, mivurugano na kupotea kwa
amani nchini. Hivyo umakini unahitajika miongoni mwa wasanii katika kuzingatia
weledi, maadili, uzalendo kwa taifa na kuitumia Sanaa kama chombo cha kujenga
jamii yenye kuzingatia maadili.
SANAA NI KAZI TUIKUZE,
TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey
L. Mngereza
KATIBU
MTENDAJI, BASATA
No comments:
Post a Comment