Mwandishi wa makala haya akiwa kwenye geti la kuingilia ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Manyara.
Simba majike wakiwa na watoto wao ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Manyara.
Simba akiwa amejipumzisha juu ya mti.
Na Daniel Mbega,
Manyara
HAWAFI kwa Ukimwi wala malaria, lakini Simba madume wametoweka katika
Hifadhi ya Taifa ya Manyara. Matokeo yake wameacha wajane na yatima.
Hadi kufikia mwaka 2013, hifadhi nzima inadaiwa ilikuwa na Simba dume
mmoja tu, wawili wengine walikimbia baada ya ‘kuzidiwa’ na utoaji wa huduma kwa
Simba majike.
Naam. Hayo ndiyo matokeo ya ujangili, janga la kitaifa ambalo kwa hakika
linatishia uwepo wa rasilimali za asili kwa faida ya wachache wanaotaka kuchuma
mahali wasipopanda.
Hali hiyo imesababisha hata kivutio kile maarufu cha kuwaona Simba
wanaokwea miti kutoweka, kwani walio wengi wanaogopa kukwea miti kwa hofu ya
kupopolewa na majangili.
“Nimekuja hapa kutaka kuwaona hao Simba wanaokwea miti, lakini sijamuona
hata mmoja,” anasema kwa masikitiko Sarah Evans, mtalii kutoka Uingereza.
Kwa miaka mingi, watalii kutoka ng’ambo wamekuwa wakivutiwa na tabia ya
Simba wa Manyara kukwea miti, ambapo hufanya hivyo kutokana na eneo hilo kuwa na
siafu wengi ambao wanawapa shida na hivyo kutafuta mahali salama juu ya miti
kujihifadhi.
Manyara, ambayo ni hifadhi pekee barani Afrika kuwa na Simba wanaopanda
miti, ipo ndani ya Bonde la Ufa ambalo kingo zake upande wa kaskazini na
magharibi zinaongeza mandhari zaidi, achilia mbali Ziwa Manyara upande wa
kusini.
Wanyama wanaopatikana ndani ya hifadhi hiyo ni pamoja na simba, nyati,
tembo, nyani, chui, pundamilia na wanyama wengine wanaokula majani, huku
ikisifika kwa wingi wa ndege hasa heroe na mnandi ambao huonekana katika
makundi makubwa na kufanya eneo hili la utalii kuwa na aina 400 za ndege
wanaovutia.
Chemchemi za maji moto ni maajabu mengine ndani ya hifadhi hiyo. Maji
hayo yanayobubujika kutoka ardhini huonekana yakitoa moshi kama vile maji yanayochemka
jikoni. Chemchem hizi za maji moto ya asili zimekuwa zikibubujika bila kukauka
kwa kipindi cha mamilioni ya miaka.
Mji mdogo wa Mto wa Mbu, ambao upo jirani na lango la kuingilia
hifadhini upande wa mashariki, ni kituo kikubwa cha biashara kinachotoa huduma
kwa wageni wanaotembelea hifadhi hiyo iliyoanzishwa rasmi mwaka 1960 na yenye
ukubwa wa kilometa za mraba 330 (kilometa za mraba 220 ni za eneo la Ziwa
Manyara – lenye urefu wa kilometa 40 na upana wa kilometa 13 – na kilometa za
mraba 110 ni nchi kavu), ikiwa umbali wa kilometa 126 kutoka
Arusha mjini. Kipindi kizuri cha kutembelea hifadhi hiyo ni kuanzia mwezi Juni
hadi Desemba baada ya mvua za masika.
Jina la hifadhi ya Taifa ya ziwa Manyara limetokana na neno lililotoholewa kutoka
katika lugha ya kabila la Wamaasai (Emanyara) lenye kumaanisha
mmea wa asili ujulikanao Kiswahili kama ‘Mnyaa’ au kwa kisayansi na
Kibotania Eurphorbia tirucalii
na kwa Kiingereza unafahamika kama Milk
bush au Finger Eurphorbia.
Hifadhi hiyo ina hadhi ya kimataifa na inatambuliwa na Shirika la umoja
wa mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na utamaduni (Unesco).
Lakini hatari ya ujangili inayosababisha vivutio vingi vya asili – hasa
wanyama – kutoweka, inaweza kuifanya hifadhi hiyo kuwa msitu usio na wanyama.
Meneja wa Program ya Ujirani Mwema wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa),
Ahmed Mbugi, anasema ujangili limekuwa janga kubwa, siyo kwa Tembo tu, bali
hata Simba.
Anasema, katika kipindi cha miaka mitatu tu (2008 hadi 2010), jumla ya
Simba waliouawa kijangili kwenye Hifadhi ya Manyara ni 62, huku madume wakiwa
ndio wengi.
“Mwaka 2008 waliuawa Simba 15, mwaka 2009 Simba waliouawa walikuwa 30 na
mwaka 2010 jumla ya Simba 17 waliuawa kwenye hifadhi hiyo. Majangili wanawinda
zaidi madume, matokeo yake hifadhi nzima ikabaki na Simba madume watatu tu,
lakini kwa sasa wawili wamekimbia hifadhini kwa sababu ya kuzidiwa na utoaji wa
huduma kwa majike, amebaki dume mmoja,” anasema Mbugi.
Hali hiyo, anasema, “…Imesababisha kuwepo kwa wajane na yatima wengi kwa
wanyama hao, hali inayotishia kutokuwepo kwa ongezeko lao kwa miaka ijayo kwani
dume mmoja naye anaweza kuchoka na hata kufa. Pengine hata wadogo waliopo sasa,
watakapokua hawataweza kuzaliana kwa vile wanyama hao hawawezi kujamiiana
kutoka familia moja.”
Lakini mauaji hayo hayakuwapata Simba tu, kwani katika kipindi hicho pia
watu 58 waliuawa na wanyama hao wakali, “…wengi wakiwa katika harakati ya
kuwawinda Simba kwenye makazi yao,” anaongeza Mbugi.
Hali inaonekana kuwa mbaya katika Hifadhi ya Manyara kuhusu uwepo wa
Tembo ambapo katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2009, jumla Tembo 104 waliuawa
kijangili.
“Binadamu waliojeruhiwa na Tembo katika kipindi hicho walikuwa 63,” anasema Mbugi na kuongeza kwamba wengi
kati ya watu hao ni wale wanaofanya shughuli zao katika ushoroba wa Tembo.
Mbugi anasema hali hiyo imeifanya Tanapa kuongeza juhudi katika mpango
wa ujirani mwema kwa kuwashirikisha wanajamii wanaoishi pembezoni mwa hifadhi
zote huku shirika likisaidia miradi mbalimbali ya kijamii.
“Miradi hii wanaibua wananchi wenyewe, hatuwezi kwenda kuwajengea vyoo
wakati mahitaji yao ni zahanati. Kwa kufanya hivi tunataka kujenga ushirikiano
wa karibu na kuwaelimisha wanajamii kwamba maliasili hizi ni za Watanzania
wote,” anasema.
Tanapa, kupitia program hiyo, inachangia asilimia 70 kwenye miradi yote
ya kijamii, wakati asilimia 30 ni nguvukazi za wananchi husika na Mbugi
anasema, “…Katika kipindi cha miaka 10, yaani kuanzia 2003/2004 – 2012/2013,
shirika hilo limetoa jumla ya Shs. 13,848,784,463.19 kusaidia miradi 1,003 ya
jamii.
Katika mwaka wa fedha 2003/2004, Tanapa ilifadhili miradi 94
iliyogharimu Shs. 805,821,034.24; mwaka 2004/2005 jumla ya Shs. 618,502,682.95
zilitumika katika miradi 60; mwaka 2005/06 jumla ya Shs. 865,860,778 zilitumika katika miradi
65; mwaka 2006/07 jumla ya Shs. 1,212,619,300 zilitumika katika miradi 90;
mwaka 2007/08 walitumia Shs. 3,447,154,353 katika miradi 141; na mwaka 2008/09
walitumia Shs. 1,736,751,235 katika miradi 87.
Aidha, kwa mwaka wa fedha 2009/10
walifadhili miradi 98 iliyogharimu Shs. 2,320,893,785; mwaka 2010/11 walitumia
Shs. 536,136,868 kugharamia miradi 33; mwaka 2011/12 walitumia Shs. 744,244,212
kugharamia miradi 26 na mwaka 2012/13 walitumia Shs. 1,560,800,212 katika
miradi 36 ya jamii.
Fedha hizo, anasema, zinatokana na asiliamia ya mapato yatokanayo na
hifadhi hizo, “…hasa baada ya kutoa gharama za bajeti ya idara husika.”
Ufadhili huo wa Tanapa, anasema Mbugi, umesaidia kupunguza migogoro
baina ya hifadhi na wananchi na pia umepromoti uhifadhi wa mazingira huku
mpango ukisaidia kuibua ajira kwa kusaidia makundi mbalimbali ya jamii.
Mpango wa Ujirani Mwema, awali ukijulikana zaidi kama Huduma za Uhifadhi
kwa Jamii (CCS) ulianzishwa mwaka 1985 kufuatia mkutano uliofanyika Seronera
ambao ulikuwa na madhumuni ya kujadili masuala ya Mpango wa Ikolojia katika
Hifadhi ya Serengeti.
Katika mkutano huo ilielezwa kwamba, wanyama wengi walikuwa wanatoweka
kwa sababu ya uwindaji haramu ambapo ilibainishwa kwamba Nyati walikuwa
wamepungua kutoka 70,000 hadi 40,000 katika hifadhi hiyo.
“Tembo walikuwa wamepungua kutoka 2,500 hadi 500 wakati Faru walipungua
kutoka 1,000 hadi 20 tu,” anasema Mbugi na kuongeza kwamba hali hiyo
ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na ujangili uliofanywa na wananchi wa maeneo
yanayozunguka hifadhi kwa matumizi ya nyumbani na biashara.
Anaongeza kwamba, malengo ya program hiyo ni kuongeza uhusiano mwema
kati ya hifadhi na jamii na kuhakikisha maslahi ya Tanapa yanahubiriwa katika
ngazi zote kwa kutoa taarifa katika vijiji husika.
Mpaka sasa Tanapa inasimamia hifadhi 15 ambazo ni Arusha, Gombe, Katavi,
Kilimanjaro, Kitulo, Mahale, Lake Manyara, Mikumi, Mkomazi, Ruaha, Rubondo,
Saadani, Serengeti, Tarangire, na Udzungwa.
Hifadhi zote hizo zinazungukwa na jumla ya mikoa 28, wilaya 52 na vijiji
536 huku hifadhi za Kilimanjaro na Serengeti zikizungukwa na vijiji 88 kila
moja.
0656-331974
No comments:
Post a Comment