PRESS RELEASE
Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Reggae Production
House iliyo chini ya Msanii Mkongwe wa reggae Innocent Nganyagwa limeandaa programu
maalum kwa ajili ya kurudisha hadhi ya muziki wa reggae nchini.
Programu
hiyo ambayo itafanyika makao makuu ya BASATA yaliyoko Ilala Sharif Shamba
jijini Dar es Salaam Jumatatu ya Tarehe 28/09/2015 kuanzia saa 4:00 hadi saa 6:30
Mchana kupitia Programu ya Jukwaa la Sanaa, itakuwa mahsusi kwa ajili ya
kuurudisha muziki wa reggae jukwaani, kujadili mwelekeo wa muziki huu na kuja
na mikakati bora ya kuurudishia hadhi yake.
Ieleweke
kwamba katika siku za karibuni muziki huu wa reggae umekuwa umeganda na
kutokupiga hatua kubwa hali ambayo imewafanya wadau wa muziki kukosa burudani
ambayo wamekuwa wakiipata huko nyuma kupitia kwa wasanii wakongwe kama Innocent
Nganyagwa, Innocent Garinoma, Justine Kalikawe na wengineo.
Changamoto
kubwa si tu ni muziki huu kutochezwa kwenye vyombo vya habari bali pia kuna
changamoto ya wasanii wenyewe kutokubadilika na kutengeneza muziki unaokwenda
sambamba na soko pia hitaji la mashabiki.
Ni
nia ya BASATA kuona wasanii na wadau wote wa muziki nchini wanahudhuria programu
hii mahsusi kwa lengo la kujadiliana kwa pamoja hatma ya muziki wa reggae,
kupata historia ya jinsi ulivyokuwa huko nyuma, kutazama na kuburudika Jukwaani
na muziki wa mmoja wa wasanii wakongwe wa muziki huu.
BASATA
linaamini kwamba baada ya programu hii wasanii wa reggae na wadau kwa ujumla
watakuwa na mwanzo mpya katika kurudisha hadhi ya muziki wa reggae nchini na
kuhakikisha unaendelea kudumu.
Sanaa ni Kazi, tuikuze, tuitunze na
kuithamini
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI BASATA
No comments:
Post a Comment