John Magufuli mara baada ya kupitishwa na CCM kugombea Urais Julai 12, 2015.
Na Daniel Mbega
KIMBUNGA
kimepita ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kwa kiasi kikubwa kimekitikisa
chama hicho kikongwe barani Afrika.
Kuondoka
kwa Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kwenda Chadema na hatimaye kuteuliwa
na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumeitikisa CCM hasa kutokana na wimbi
la makada wengi walioondoka pamoja naye.
Awali CCM
iliamini kwamba, baada ya kumaliza zoezi la kumpata mgombea wake wa urais Julai
12 mjini Dodoma, basi kazi ingekuwa rahisi zaidi, lakini kwa uhakika imekuwa
ngumu na kuiyumbisha ingawa badoina nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi mkuu wa
mwaka huu.
Blogu hii ya www.brotherdanny.com leo inachambua baadhi ya sababu 10 ambazo bado zinaipa nafasi kubwa CCM ya kushinda Oktoba licha ya vuguvugu kubwa la mabadiliko lililopo:
1. Ukongwe wake
Daima huwa
napenda kusema; “Ukubwa wa umri, ni ujana wa umahiri”. Kwa kawaida kadiri mtu
anavyozeeka ndivyo anavyozidi kuwa na busara na ndiyo sababu daima huwa
tunakimbilia kwa wazee ili kupata ushauri.
Ukiacha
Frelimo ya Msumbiji na ANC ya Afrika Kusini, CCM ndicho chama pekee kikongwe
zaidi Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambacho bado kipo madarakani.
Katika
uhai wake chama hiki kimesaidia ukombozi wanchi nyingi barani Afrika,
kimewapika na kuwatengeneza wanamapinduzi wengi ambao wamepata nab ado
wanaendeelea kuongoza nchi zao.
Kimesaidia
chaguzi nyingi barani humo, zikiwemo zile ambazo mageuzi yamefanyika, kutokana
na kujua propaganda.
Ukongwe
huo, wa kujua mbinu za jukwaani na za medani, bado unakipa kete nzuri zaidi za
kushinda uchaguzi na wimbi la sasa la upinzani linaweza kukikomaza zaidi.
2. Kukubalika vijijini
Licha ya
upinzani kuonekana kupata nguvu ghafla baada ya ujio wa Lowassa, lakini
inaonekana vyama hivyo vina nguvu zaidi kwenye miji ambako wimbi la mabadiliko
kwa vijana, hasa wasomi, ni kubwa.
Hata
hivyo, CCM inakubalika zaidi vijijini ambako ndiko waliko Watanzania takriban
asilimia 83. Sehemu nyingine huko vijijini bado wanaamini Rais wa Tanzaniani
Mwalimu Julius Nyerere na chama pekee cha siasa ni CCM, hivyo linapokuja suala
la upinzani hata hawajishughulishi nalo.
Nakumbuka
safari moja Chadema katika operesheni zao nyingi walikwenda na helikopta katika
Kijiji cha Songambele wilayani Kongwa katika Mkoa wa Dodoma. Umati mkubwa
ulifika pale na kuizunguka helikopta. Haukujishughulisha kabisa na hotuba ya
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyokuwa akiitoa.
Ikabidi
aulize: “Mmekuja kunisikiliza au kutazama helikopta?” Wakamjibu: “Tumekuja
kutazama helikopta!!” Akaingia kwenye helikopta na kuelekea Kibaigwa. Mkutano
ukaishia hapo. Iko mikoa ambako upinzani hauwezi kugusa, miongoni mwake ni Mkoa
wa Dodoma, ingawa kama watajitahidi safari hii wanaweza walau kupata hata jimbo
moja.
Kwa hiyo
ni wazi kwamba CCM, pamoja na mtikisiko uliotokea, siyo tu kwamba bado kina
wanachama wengi, bali kinakubalika sana vijijini ambako wananchi wanatambua
mchango wa chama hicho kuliko kelele nyingi za wapinzani, ambao wengi ama
hawajawahi kufika huko kunadi sera zao au bado wananchi wana mashaka ya
kuwakabidhi wapinzani serikali.
3. Ukigeugeu wa wapinzani
Hii ni
silaha kubwa kwa CCM safari hii kuelekea uchaguzi mkuu na kitaitumia agenda
hiyo kuwamaliza wapinzani kutokana na ukigeugeu wao.
Kama
wapinzani ndio waliotangaza kwamba Lowassa ni fisadi, CCM wao watasema, pamoja
na kutomshughulikia kwa kukosa ushahidi, lakini waliamua kumwengua kwenye mbio
za urais kwa tuhuma hizo hizo zilizotajwa na wapinzani wenyewe.
Lakini
kinyume chake, wapinzani waliomwita fisadi, leo hii wamemtakasa na kumuona
anang’ara kama yakuti kiasi kwamba wameyageuka maneno na matamko yao wenyewe
ambayo kwa miaka kadhaa ulikuwa ni wimbo usio na vina, urari, mizani wala
kiitikio.
Ni silaha
hiyo hiyo ambayo wapinzani wenyewe awali walikuwa wamepanga kuimaliza CCM ikiwa
ingempitisha Lowassa kugombea.
Kwamba,
kama wapinzani wenyewe walijiapiza kutopokea ‘makapi’ ya CCM, iweje sasa
wamegeuka kuwa jalala ambalo mizoga na masazo yote yanatupwa humo?
4. Kujitenga kwa Slaa, Lipumba
Dk. Wilbrod Slaa,
Katibu Mkuu wa Chadema, ametengwa rasmi na chama chake baada ya yeye mwenyewe
kujitenga tangu chama hicho kilipotangaza kumkaribisha Lowassa. Hajaonekana na
hajazungumza lolote licha ya mwenyekiti wake, Mbowe, kusikika akisema kwamba
Ukawa utaendelea na kwamba Dk. Slaa amepumzika.
Kimya chake
kinaonyesha kwamba mambo hayako sawa na inaelezwa kwamba Dk. Slaa alipinga sana
kukaribishwa kwa Lowassa ndani ya chama hicho lakini Mbowe na wenzake
wakamkatalia.
Nafsi inamsuta Dk.
Slaa kwa sababu ni yeye ambaye Jumamosi ya Septemba 15, 2007 alisimama jukwaani
pale Mwembeyanga, Temeke na kumtaja Lowassa katika ile Orodha ya Mafisadi
kwamba ni fisadi anayeitafuna nchi, sasa akiwa ndani wanawezaje kuketi pamoja?
Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Nguyulu Ibrahim Haruna Lipumba, naye amejivua wadhifa huo aliodumua nao
tangu mwaka 1994 walipomtoa James Mapalala kwenye mkutano ule wa Mkonge Hotel,
Tanga.
Sababu amezitaja,
kwamba wenzake, hasa Chadema, wamekiuka makubaliano waliyojiwekea wakati
wanaunda umoja huo wa kutowapokea mafisadi, ambao sasa wameonekana kunyenyekewa
zaidi.
Kabla ya hapo
alikuwa amejitenga baada ya kuona kuna dalili za kumkaribisha Lowassa, ndiyo
maana akatangaza kwamba angegombea urais kupitia CUF, lakini alirejeshwa siku
moja tu kabla ya Lowassa kutambulishwa rasmi.
Nafsi yake
imemsuta, kama alivyosema mwenyewe, kwamba maazimio yalikuwa kutowapokea hao
mafisadi, kinyume chake wanachama wengi wamekimbilia huko Ukawa, na hasa
Chadema.
Dk. Slaa na
Lipumba bado ni wanasiasa wenye nguvu na wana wafuasi wengi. Hoja alizozitoa
Lipumba zinaweza kuwa na mantiki siyo tu kwa wanachama wa CUF, bali hata kwa
Watanzania wengine ambao walikuwa wamezolewa na kimbunga hicho.
Slaa naye hajasema
lolote, lakini ukimya wake umekwishaleta ufa mkubwa ndani ya Ukawa na hata kama
leo atatokea na kutamka kwamba yuko pamoja na umoja huo, tayari atakuwa
ameyumbisha harakati.
5. Nguvu ya fedha
Licha ya ukweli kwamba Chadema na
Ukawa safari wako vizuri kifedha kutokana na ujio wa Lowassa ambaye bado
anaweza kuwatumia ‘marafiki zake kumchangia’, lakini CCM bado ina nguvu ya
fedha, ambacho ni kigezo muhimu katika kufanikisha kampeni na kupata ushindi
katika siasa za ushindani.
Bila fedha katu huwezi kufika kila
kona ya nchi, na maeneo mengi hayafikiki kirahisi ila kwa gharama kubwa.
Kama chama kinataka kuungwa mkono, ni
lazima viongozi na wagombea watembelee maeneo mbalimbali nchini kujinadi kwa
wananchi.
Vyama vyote vinavyoshiriki katika
uchaguzi vinakidhi kigezo hiki, ingawa kuna tofauti kubwa. Vyama vitatu kati ya
vinne vinavyounda Ukawa vinapata ruzuku kutoka serikalini kutokana na kuwa na
wabunge.
Lakini CCM ndiyo inayoongoza kwa
kupewa kiasi kikubwa cha fedha kama ruzuku, kwani inapata takriban Shs. 800
milioni kwa mwezi, Chadema inapata Shs. 203.6 milioni, CUF inapata Shs. 117.4
milioni na NCCR-Mageuzi Shs. 10 milioni.
Ukiachilia mbali fedha za ruzuku,
bado CCM ina vitegauchumi vingi na wafadhili wengi wakiwamo wafanyabiashara
wakubwa nchini, tofauti na wapinzani.
6. Mtandao
wa wanachama
Pamoja na kwamba CCM bado inakubalika
katika maeneo mengi vijijini na licha ya wanachama kuondoka, lakini chama hicho
bado kina mtaji wa wanachama nchi nzima kutokana na mtandao wake imara
uliojengwa tangu kipindi cha mfumo wa chama kimoja.
Mfumo wa CCM ni kuanzia ngazi ya
shina (mabalozi wa nyumba kumi), mtindo unaokiwekea mazingira mazuri ya
kujikusanyia wanachama wa uhakika katika maeneo mengi ya nchi, hususan vijijini
ambako upinzani umeshindwa kupenya kwa kiasi kikubwa.
Japokuwa Chadema imeiga mfumo huo
wa mashina, lakini mafanikio yake hayawezi kulinganishwa
na CCM.
7. Demokrasia ndani ya vyama
Pamoja na madai ya matumizi makubwa
ya fedha na vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi, mfumo wa uongozi wa CCM unaonekana
kuwa wa kidemokrasia zaidi kulinganisha na ule wa vyama vya upinzani.
CCM pekee ndicho chama ambacho viongozi
wake wana utamaduni wa kuachiana madaraka kwa njia ya kidemokrasia kila
baada ya miaka fulani.
Wakati CCM ikiweka bayana katika
Katiba yake vipindi viwili vya uongozi, kwa vyama vya upinzani hakuonekani
kuwapo kwa demokrasia hiyo, baadhi yao tangu vianzishwe viongozi wa kitaifa ni
walewale.
Vyama vyote vinavyounda Ukawa havina
ukomo wa madaraka na viongozi wake wote wa taifa, wamedumu kwenye
uongozi kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano.
Tazama CUF, ambako kama Ukawa
wasingevuruga makubaliano, basi Lipumba angeendelea kuwa mwenyekiti kwa kipindi
kirefu zaidi licha ya kuongoza chama hicho kwa miaka 16 sasa.
Ndani ya Chadema kumekuwa na tuhuma
za ubabe na ‘u-kanda’ na inapotokea mtu mwingine anataka kugombea uongozi,
huanza kushambuliwa kama ilivyotokea kwa Zitto Kabwe mwaka 2009. Tuhuma zilizotolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho aliyejiuzulu, Dk. Wilbrod Slaa, zimetia ufa mkubwa kwenye chama na umoja huo kwa ujumla, licha ya viongozi wa Chadema kufumba macho na kujibu hoja kwa 'masimango'. Hoja za Dk. Slaa hazijajibiwa mpaka sasa, wafuasi wa mageuzi wanatukana badala ya kujibu.
NCCR nako mambo ni yale yale. Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu wameachia ngazi kwa sababu makubaliano ndani ya Ukawa yamekiukwa. Chadema imepewa majimbo mengi na chama hicho kina majimbo machache.
Kama kawaida, kila anayeondoka ndani ya Ukawa, ama anayekosoa mwenendo mzima, ama ataambiwa amehongwa, amenunuliwa au anatumiwa na 'maCCM' kama wenyewe wanavyoita. Uhuru wa kidemokrasia haupo, na mtaji wanaojivunia wa vijana ambao wengi wao umri wao ni mdogo kuliko hata umri wa mfumo wa vyama vingi, ndio unawapa kiburi wapinzani hawa kiasi kwamba, hoja za msingi zinapuuzwa na wanachotaka ni mabadiliko tu - siyo kingine.
Hii ni turufu kwa CCM, kwa sababu wanaoondoka nao wana wafuasi wao, wanaweza kuwa wameondoka nao na hata kama hawataipigia kura CCM, bado watavipigia vyama vingine na hivyo kupunguza idadi ya kura za Ukawa.
8.
Hakuna Tume huru
Kilio cha muda mrefu cha kuwepo kwa Tume huru ya
Uchaguzi bado hakijapatiwa majibu na kwa vile CCM ndiyo imeshika Dola na Tume
hiyo iko chini ya serikali yake, kushindwa kwa wapinzani kwenye urais itakuwa
ndoto ambayo itahitaji miujiza ili iwe ya kweli.
Rais ni wa CCM na ndiye anayeteua viongozi wa Tume,
ambao wanalipwa na serikali hiyo hiyo ingawa fedha hizo ni kodi za wananchi.
Huwezi kutegemea kwamba kutakuwa na haki sawa kwa asilimia zote kamaambavyo
ingekuwepo Tume huru. Hiki ni kitanzi kwa wapinzani linapokuja suala la kwenda
Magogoni.
9.
Mahusiano ya kimataifa
Ingawa zipo propaganda kwamba mataifa mengi, hasa ya
Ulaya, ‘yameichoka’ CCM, bado hakuna ukweli wowote kwa sababu chama hicho
kimejenga misingi ya muda mrefu ya mahusiano mazuri ya kimataifa.
Chadema au Ukawa wanaweza kuwa na vyama washirika
katika baadhi ya mataifa ya Ulaya, lakini CCM ina ushirika mzuri na serikali,
siyo vyama pekee, jambo ambalo ni mtaji mwingine mnono hasa linapokuja suala la
uchaguzi kama hili.
Kama ilivyo kwa wapinzani, ambao vyama washirika
lazima vitakuwa na maslahi fulani, vivyo hivyo kwa CCM kuna mataifa ambayo
mpaka sasa yana maslahi ndani ya Tanzania kutokana na uwekezaji katika sekta
mbalimbali, iwe serikali zamataifa hayo ama kampuni zinazotoka huko.
Urusi imewekeza kwenye Uranium, Canada imewekeza
kwenye dhahabu, Afrika Kusini kwenye miradi mingi ikiwemo Tanzanite, Marekani
na Uingereza kwenye mafuta na gesi kama ilivyo kwa China ambayo pia imewekeza
kwenye chuma na makaa ya mawe.
Kwa kuzingatia uwekezaji huo, mataifa haya hayawezi
kuwa na uhakika wa serikali ijayo ya wapinzani ikiwa maslahi yao yatakuwa
salama au la, na kwa vile wapinzani wamekuwa wakipiga kelele kuhusu mikataba ya
uwekezaji, siyo rahisi kwao kuamini kwamba watakuwa salama.
10.
Muungano
Hoja ya kudumishwa kwa Muuungano itanadiwa zaidi na
CCM hasa Zanzibar na kuwaeleza kwamba ikiwa wapinzani watachukua madaraka, basi
Muungano utavunjika. Na ikiwa Muungano wa Zanzibar na Tanganyika utavunjika,
basi hata Zanzibar haitakuwepo kwa sababu itagawanyika kuwa Pemba na Unguja!
Haya yako dhahiri na yangeweza kunadiwa zaidi kama
zoezi la Kura ya Maoni kuhusu Katiba Pendekezwa lingekuwepo, kwani wapo wengi
wanaotamani Serikali Tatu ndani ya Muungano lakini siyo muundo kama wa sasa.
Tusubiri na tuone kitakachotokea.
0656-331974
No comments:
Post a Comment